Mamilioni kuamua hatma ya Tanzania Uchaguzi Mkuu 2025 leo

October 29, 2025 1:01 am · Waandishi Wetu
Share
Tweet
Copy Link
  • Wapiga kura milioni 37.6 wanatarajiwa kujitokeza leo kupiga kura zao
  • Uchaguzi wa urais wafanyika bila wagombea kutoka vyama vikuu vya upinzani Tanzania.

Dar es Salaam. Mamilioni ya wapiga kura Tanzania wanatarajiwa kupiga kura katika uchaguzi wa saba tangu kuanza kwa mfumo wa vyama vingi hatua itakayowawezesha kuchagua viongozi watakaowaongoza kwa miaka mitano ijayo. 

Katika uchaguzi huu, unaofanyika Oktoba 29, wapiga kura 37.6 milioni watakuwa na fursa ya kumchagua rais, mbunge, mjumbe wa baraza la wawakilishi (kwa Zanzibar) na madiwani. 

Uchaguzi huu unaofanyika bila ushiriki wa wagombea wa urais kutoka vyama viwili vikubwa vya upinzani nchini ambavyo ni Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na ACT-Wazalendo.

Chadema, chama kikuu cha upinzani nchini mpaka sasa, hakitashiriki uchaguzi huo kutokana na kutokukubaliana na mfumo wa uchaguzi na baada ya kuondolewa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kushiriki kutokana na kutosaini kanuni za maadili ya uchaguzi. 

Vyama 17 kuchuana na CCM

Mgombea urais wa ACT-Wazalendo, Luhaga Mpina yeye aliondolewa na INEC baada ya kupokea pingamizi kutoka kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kutokana na madai kuwa uteuzi wake ndani ya chama haukufuata taratibu. 

Vyama 18 vinashiriki na kuufanya uchaguzi huu kuwa ndio uchaguzi uliohusisha vyama vingi zaidi na kusimamisha wagombea katika nafasi mbalimbali za uwakilishi.

Samia Suluhu Hassan, mgombea urais wa Chama cha Mapinduzi (CCM) anarusha karata yake ya kuwania kipindi kingine cha miaka mitano baada ya kuiongoza Tanzania tangu Machi 2021 baada ya kifo cha mtangulizi wake Dk John Magufuli. 

Hata hivyo, Rais Samia atakuwa na upinzani kutoka kwa wagombea wengine 16 wa urais kutoka kwenye vyama vingine vidogo na vyenye ushawishi mdogo vikiwemo vya CUF, NLD na NCCR-Mageuzi.

Vyama vinavyoshiriki uchaguzi vinasema mabadiliko yanayopigiwa chapuo yanaweza kufanyika mara baada ya uchaguzi kumalizika kwa kuwa mabadiliko hupitia mchakato maalumu.

‘Mwamko mkubwa kwa vijana’

Mchambuzi wa masuala ya siasa nchini Tanzania Abdulkarim Atiki ameiambia Nukta Habari kuwa uchaguzi wa 2025 umeonesha mwamko mkubwa wa vijana ikilinganishwa na miaka iliyopita.

“Vijana wengi wamejitokeza kushiriki mijadala, kampeni, na hata kugombea nafasi mbalimbali. Hii ni dalili njema ya kizazi kipya kinachotaka kushiriki katika maamuzi ya taifa,” amesema Atiki.

Shirika la ushauri wa masuala ya uchumi duniani la Oxford Economics limeeleza kwenye taarifa yake kwa vyombo vya habari kuwa uchaguzi huu unakipa CCM uhakika wa kushinda urais na viti vingi vya ubunge kutokana na upinzani dhaifu.

“Japo kuna wagombea wengine 16 wa urais, bado chama kikuu cha upinzani kimetengwa katika uchaguzi huo,” amesema Mchambuzi wa siasa wa Oxford Economics, Jervin Naidoo.

Milioni 37.6 kuamua hatma ya Tanzania

Kwa mujibu wa INEC Watanzania waliojiandikisha kupiga kura 2025 ni milioni 37.6 wakiwemo milioni 36.6 kutoka Tanzania Bara na 996,303  kutoka Zanzibar.

Uchambuzi zaidi wa takwimu hizo za wapiga kura unabainisha kuwa idadi hiyo ni ongezeko la asilimia 26 ikilinganishwa na wapiga kura milioni 29.8 waliojiandikisha mwaka 2020

Kati ya waliojiandikisha wanawake ni milioni 18.9 sawa na asilimia 50.31 na wanaume ni milioni 18.7.

Katika idadi ya waliojiandikisha watu wenye ulemavu ni 49,174 sawa na takribani asilimia 0.13 ya jumla ya wapiga kura.

Vituo kufunguliwa Saa 1:00 asubuhi

Jumla ya vituo vya kupigia kura 99,895 vitakuwa wazi kuanzia saa moja kamili asubuhi na kufungwa saa10 kamili jioni.

Itakumbukwa kuwa idadi hiyo ya vituo vya kupigia kura ni mpya baada ya ZEC kufanya marekebisho ya vituo vya kupigia kura ambapo awali vilitangazwa 99,911.

Katika mgawanyo huo, Tanzania Bara itakuwa na vituo 97,348 na Tanzania Zanzibar vitakuwa na 2,547.

Idadi hiyo ya vituo 99,895 ni sawa na ongezeko la asilimia 22.47 ya vituo vya kupigia kura 81,567 vilivyotumika katika Uchaguzi Mkuu 2020.

INEC imeeleza kuwa inatarajia matokeo ya urais kutolewa ndani ya Saa 72 baada ya kukamilika upigaji kura. Hata hivyo, kwa mujibu wa katiba, matokeo ya urais hayawezi kupingwa mahakamani. 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Follow Us on TikTok

Subscribe to Our YouTube Channel

Subscribe

Loading videos...

Loading videos...

Loading videos...

Enable Notifications OK No thanks