Kwa nini mchango wa sekta ya misitu ni mdogo katika pato la Taifa?

September 29, 2022 11:47 am · Abdushakur
Share
Tweet
Copy Link

Muonekano wa vitalu vya miche ya miti katika shamba la msitu wa Sao Hill, mkoani Iringa. Shamba hilo linalomilikiwa na Serikali lina ukubwa wa hekta 135,903. Pia linatumika kwa shughuli mbalimbali ikiwemo ufugaji wa nyuki. Picha| Wizara ya Maliasili na Utalii.


  • Ukataji wa miti hovyo wachangia.
  • Misitu ilichangia asilimia 2.8 katika pato la Taifa (DGP) mwaka jana ikilinganishwa na asilimia 2.6.
  • Serikali yaingilia kati kulinda misitu isiharibiwe.

Dar es Salaam. Licha ya mchango wa sekta ya misitu kuongezeka ndani ya kipindi cha mwaka mmoja uliopita, jitihada zinahitaji kulinda rasilimali hiyo ili kuimarisha mchango wake katika maendeleo ya Tanzania.

Kwa mujibu wa Kitabu Cha Hali ya Uchumi wa Taifa kwa mwaka 2021, sekta ya misitu ilichangia asilimia 2.8 katika pato la Taifa (DGP) mwaka jana.

Mchango huo umeongezeka kutoka asilimia 2.6 ya mwaka 2020. 

Tangu mwaka 2016, mchango wa sekta hiyo kwa GDP haujawahi kuvuka asilimia tatu huku mchango wake ukipanda na kushuka.

Mathalan, mwaka 2016, misitu ilichangia asilimia 2.9 ambapo mwaka uliofuata ikachangia asilimia 2.8 kabla mchango wake haujashuka hadi asilimia 2.7 mwaka 2018 na 2019.

Hata hivyo, mwaka uliofuata wa 2020, mchango wa sekta hiyo ulishuka zaidi hadi asilimia 2.6 kabla hujapanda hadi asilimia 2.8 mwaka jana.  

Tanzania inakadiriwa kuwa na hekta milioni 48 za misitu, kiwango ambacho kimechukua ardhi ya nchi kwa asilimia 51 huku sekta hiyo ikiajiri watu takriban milioni 4, kwa mujibu wa Wizara ya Maliasili na Utalii. 

Sababu za mchango mdogo

Utafiti wa Mkakati wa Kupunguza Ukataji Miti Hovyo na Uharibifu wa Misitu (Mkuhumi) wa mwaka 2013 unaonyesha kuwa ukataji wa miti hovyo ni miongoni mwa vitu vinavyofanya misitu nchini ipunguze kasi katika kuchangia pato la Taifa.

Ripoti ya utafiti huo inaeleza kuwa endapo misitu haitalindwa, kiwango cha hasara katika uchumi nchi kati ya mwaka 2013 hadi 2033 kitakuwa Sh273 bilioni.

Waziri wa Maliasili na Utalii Balozi Dk Pindi Chana katika hotuba ya bajeti ya wizara yake kwa mwaka 2022/23 alisema kuwa kiwango cha kutoweka kwa misitu kwa mwaka kimeongezeka kutoka hekta 372,800 kwa makadirio ya mwaka 2015 hadi hekta 469,420 kwa mwaka 2018.

Waziri Dk Chana alieleza kuwa ukataji miti unachangiwa zaidi na kuongezeka kwa idadi ya watu, utafutaji maeneo kwa ajili ya makazi na shughuli mbalimbali na usafishaji wa mashamba kwa ajili ya kilimo. 

Waziri huyo alisema ili kuokoa misutu, Serikali itaimarisha ulinzi katika hifadhi mbalimbali nchini, kutatua migogoro ya ardhi na kusimamia ukusanyaji wa mapato ya misitu. 

Pia kushirikiana na sekta binafsi kutoa elimu na kuhamasisha jamii kushiriki harakati za kulinda na kutunza misitu nchini.

Enable Notifications OK No thanks