Mapato sekta ya utalii yapaa Tanzania
- Yameongezeka kutoka Sh1.6 trilioni mwaka 2020 hadi Sh3.1 trilioni) mwaka 2021.
- Ongezeko la watalii wa kimataifa lachangia kuongezeka kwa mapato.
- Serikali kuwekeza katika utalii wa fukwe kuongeza mapato zaidi.
Dar es Salaam. Mapato yatokanayo na sekta ya utalii nchini Tanzania yameongezeka kwa asilimia 93.7 ndani ya kipindi cha mwaka mmoja uliopita, Wizara ya Maliasili na Utalii imeeleza.
Idadi ya mapato yatokanayo na utalii imeongezeka kutoka Dola za Marekani milioni 714.59 sawa na Sh1.6 trilioni mwaka 2020 hadi Dola za Marekani milioni 1,310.34 (Sh3.1 trilioni) mwaka 2021.
Ongezeko hilo la mapato limechangiwa kwa kiasi kikubwa na kuongezeka kwa idadi ya watalii waliotembelea vivutio mbalimbali zikiwemo mbuga za wanyama mwaka jana.
Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Juma Mkomi amesema mwaka mmoja baada ya mlipuko wa janga la Uviko-19, idadi ya watalii iliongezeka kutoka watalii 620,867 mwaka 2020 hadi kufikia watalii 922,692 mwaka jana sawa na ongezeko la asilimia 48.6
Sababu zilizochangia ongezeko la watalii kwa mujibu wa Mkomi ni jitihada zinazofanywa na Serikali pamoja na sekta binafsi katika kutangaza vivutio vya utalii ndani na nje ya nchi.
Watalii wanaokuja Tanzania hupendelea kutembelea mbuga wa za wanyama na fukwe. Picha| exploretanzaniatours.com
Utafiti mpya waibeba sekta ya utalii
Jana Septemba 30, 2022 jijini Arusha, Serikali ilifanya uzinduzi wa ripoti ya Utafiti wa Watalii Walioondoka nchini mwaka 2021.
Utafiti huo unaonyesha kuwa Tanzania inazidi kufanya vizuri katika sekta ya utalii huku mapato yatokanayo na utalii yakiongezeka.
Mkomi amesema, matokeo ya utafiti yanaonesha idadi kubwa ya watalii walikuja hapa nchini mwaka jana kwa ajili ya kutembelea hifadhi za wanyamapori na fukwe.
Utafiti huo umefanywa na Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kushirikiana na Benki Kuu Tanzania (BoT), Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Idara ya Uhamiaji, Kamisheni ya Utalii Zanzibar na Shirikisho la Wawekezaji katika Sekta ya Utalii Zanzibar (ZATI)
Takwinu za utafiti huo, zimepatikana kutokana na utafiti uliofanywa katika vituo vikubwa nane vya watalii, ikiwemo viwanja vya ndege vya kimataifa pamoja na maeneo ya njia za kuingilia na kutokea watalii.
Idadi kubwa ya watalii walioingia nchini mwaka jana walitokea nchi ya Ufaransa ikifuatiwa na Marekani, Kenya na Zambia.
Mkomi amesema matokeo ya utafiti huo yameonesha kuwa wastani wa matumizi ya mtalii kwa siku hapa nchini yaliongezeka kutoka Dola za Marekani 152 (Sh354,365) mwaka 2020 hadi kufikia Dola za Marekani 199 sawa na Sh463,921 mwaka 2021.
Soma zaidi:
Kwa nini mchango wa sekta ya misitu ni mdogo katika pato la Taifa?
Mipango kuongeza watalii
Kaimu Mkurugenzi wa Utalii Wizara ya Maliasili na Utalii, Richie Wandwi amesema kwa sasa wizara imejidhatiti kuwekeza nguvu katika utalii wa fukwe kwa vile ni aina ya utalii ambao unaonekana kupendwa na watalii wengi wanaoingia nchini.
Wizara itaendelea kuzifanyia kazi changamoto mbalimbali ambazo baadhi ya watalii wamekutana nazo ili kuhakikisha idadi ya watalii inazidi kuongezeka na vivutio vilivyopo hapa nchini vinatangazwa kwa kasi zaidi katika jumuia za kimataifa.
Shirika la Umoja wa Mataifa la Utalii Duniani (UNWTO), watalii wa kimataifa wanatarajiwa kuongezeka kati ya asilimia 55 hadi asilimia 70 ya viwango vya 2019 mwaka huu wa 2022.
Hata hivyo, ongezeko hilo linategemea hali ya ugonjwa wa Uviko-19, mabadiliko ya vita nchini Ukraine na hali ya kiuchumi, hasa mfumuko wa bei na bei za nishati.