Pazia kampeni za uchaguzi lafungwa leo

October 28, 2025 4:48 pm · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link
  • Vyama vyatumia mikutano kujinadi ili kupigiwa kura kesho Oktoba 29.
  • Katiba Mpya, uchumi wa wananchi vyatawala kampeni za vyama.

Dar es Salaam. Vyama vya siasa leo vimemaliza kampeni za Uchaguzi Mkuu wa Rais, wabunge na madiwani Tanzania Bara, huku wagombea wa nafasi mbalimbali wakitumia dakika za lala salama kuwashawishi Watanzania wawapigie kura. 

Kampeni za uchaguzi  zilianza Agosti 28 mwaka huu kwa Tanzania Bara baada ya uteuzi uliofanywa Agosti 27, 2025 na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC).

Baadhi ya vyama vikiwemo vya ADA TADEA, NCCR Mageuzi ACT-Wazalendo na NRA vilimaliza kampeni za wagombea urais jana.

Kampeni za uchaguzi kwa Zanzibar ngazi zote zilianza Agosti 28, mwaka huu na zilihitimishwa jana kupisha kura ya mapema iliyofanyika leo Oktoba 18, 2025. 

Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimehitimisha kampeni zake leo Oktoba 28, 2025 jijini Mwanza huku mgombea wake wa urais, Samia Suluhu Hassan akisisitiza kuwa endapo atapewa ridhaa na Watanzania ataendeleza na kuimarisha miundombinu na kukuza sekta ya uzalishaji. 

“Tutafanya ujenzi wa miundombinu ya usafiri na usafirishaji kwa watu na bidhaa ili kurahisisha shughulu za kiuchumi na kukuza wigo wa mashirikiano ya sekta binafsi ya ndani na nje ya nchi,” amesema Samia wakati akizungumza na wanachama wa CCM katika viwanja vya CCM Kirumba jijini humo. 

Samia aliyeambatana na mgombea mwenza Emmanuel Nchimbi katika kampeni hizo amesema kuwa wataendeleza mapambano dhidi ya rushwa na kutakuwa na maridhiano ya kitaifa ili kufanikisha upatikanaji wa Katiba Mpya.

Wakati CCM wakihitimisha kampeni Kanda ya Ziwa, chama cha ACT-Wazalendo kwa Tanzania Bara kimehitimisha kampeni zake katika Jimbo la Kigoma Mjini.

ZItto Kabwe ambaye ni mgombea ubunge katika jimbo hilo kupitia ACT-wazalendo amesema chama chake kikipata ridhaa ya kuchaguliwa kitaboresha hali ya maisha ya wananchi wa Kigoma Mjini. 

“Tutaimarisha mji wetu kwa kuwa na mpango kabambe wa kufukia makorongo na kujenga barabara za ndani na mifereji ya maji ya mvua ili mji wetu uwe miongoni mwa miji bora,” amesema Zitto.

Kwa upande wa Zanzibar, ACT-Wazalendo walihitimisha  kampeni zake jana ambapo Othman Masoud Othman anayegombea urais amesema watasimamia haki za raia kwa kuwarejeshea Wazanzibari  utambulisho wao kwa kuwapa vitambulisho.  

“Tutasimamia haki za raia kwa kuwarejeshea Wazanzibari wana wa nchi hii kwanza utambulisho wa nchi yao kwa kuwa ni wazanzibari kwa kuwapa vitambulisho vya utaifa,” amesema Othman.

Maelfu ya Wananchi Mkoa wa Mwanza na kanda ya Ziwa kwa ujumla wamejitokeza kwa wingi katika Uwanja wa CCM Kirumba katika Mkutano wa kufunga kampeni za Mgombea Urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan. Picha | CCM.

Chama Cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA) kilihitimisha kampeni zake Octoba 27 Jijini Dar es salaam kwa mgombea wake wa urais Salum Mwalim kuahidi kuunda Serikali ya upatanisho na kuimarisha umoja na mshikamano kwa Watanzania. 

Chama cha Democratic Party (DP) na mgombea wake Abdul Mluya nacho kilifunga kampeni zake mkoani Iringa jana na kuahidi kujenga barabara, zahanati pamoja na kutetea maslahi ya wakulima na wafugaji.

Nacho Chama cha Tanzania Democratic Alliance (TADEA) kupitia mgombea wake wa urais George Bussungu kilihitimisha kampeni zake jijini Mwanza jana na kuahidi kulijenga upya jiji hilo kwa kujenga barabara ya juu ili kutoharibu makazi ya watu.

Sera za vyama vyote vinavyoshiriki uchaguzi mwaka huu, zimejikita katika kuwapatia Watanzania Katiba mpya, mageuzi ya utawala na kuimarisha uchumi kwa wananchi wa kawaida.

CCM yatawala kampeni za uchaguzi

Licha ya vyama 17 kusimamisha wagombea urais wa Tanzania, mgombea wa CCM, Rais Samia ameonekana zaidi kutikisa kampenikwa upande wa Tanzania Bara. 

Vyama  vingine vya upinzani vilivyotazamiwa kuleta upinzani mkubwa wa ushindani  kwa nafasi ya urais ni Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) pamoja na ACT- Wazalendo.

Vyama hivyo havikupata fursa hiyo kwa sababu Chadema kilijitoa kushiriki Uchaguzi Mkuu kwa kutosaini kanuni ya maadili ya uchaguzi huku ACT-Wazalendo, mgombea wake Luhaga Mpina akiwekewa pingamizi na Mwanasheria Mkuu wa Serikali na hivyo kukosa sifa ya kushiriki uchaguzi katika ngazi ya urais. .

Vyama vingine vilivyosimamisha wagombea ni NCCR- Mageuzi,  UPDP, TADEA, NRA, MAKINI,  NLD, AAF, DP, ADA-TADEA, ADC, SAU, UMD na UDP.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Follow Us on TikTok

Subscribe to Our YouTube Channel

Subscribe

Loading videos...

Loading videos...

Loading videos...

Enable Notifications OK No thanks