Yafahamu majimbo 46 yanayosubiri kura ya ndio au hapana
- Ni majimbo ambayo wagombea wake wamekosa wapinzani.
- Majimbo hayo yanapatikana katika mikoa 17 ya Tanzania Bara.
- Mgombea atakayepigiwa kura nyingi za hapana, uchaguzi utarudiwa katika jimbo husika.
Dar es Salaam. Wakati Watanzania wakijiandaa kupiga kura kesho, Oktoba 29, 2025, kuwachagua Wabunge watakaowawakilisha kwa miaka mitano ijayo, tayari kuna baadhi ya wagombea wanaoingia katika kinyang’anyiro hicho wakiwa na uhakika wa ushindi.
Wagombea hao wamekosa wapinzani katika majimbo yao, hivyo watapigiwa kura ya ndiyo au hapana pekee.
Kwa mujibu wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), mwaka huu, Tanzania ina jumla ya majimbo 272 ya uchaguzi. Kati ya hayo, majimbo 222 yapo Tanzania Bara na 50 yako Zanzibar.
Uchambuzi wa Nukta Habari wa majimbo ya uchaguzi, umebaini kuwa majimbo 46 kati ya 272 wagombea wake hawana wapinzani na wote wanatoka katika Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Hii ni kwa sababu katika majimbo hayo, hakuna mgombea mwingine kutoka vyama vingine vya siasa vilivyoonyesha nia ya kugombea. Vingine viliwekewa pingamizi na hivyo wagombea wao kukosa sifa kuwania ubunge katika majimbo husika.

Wagombea hao 46 watapigiwa kura ya “ndiyo” au “hapana”, tofauti na utaratibu wa uchaguzi wa mwaka 2020 ambapo wagombea wa aina hiyo walikuwa wakipita moja kwa moja bila kupingwa yaani hawapigiwi kura.
Kwa mujibu wa INEC, iwapo mgombea atakuwa hana mpinzani, jina lake hubaki peke yake kwenye karatasi ya kura, na wananchi hupiga kura ya “ndiyo” au “Hapana” kuthibitisha au kukataa kumchagua.
Endapo zaidi ya nusu ya wapiga kura watapiga kura ya “hapana”, uchaguzi katika jimbo husika utarudiwa.
Hii ni hatua ya kikatiba inayolenga kuhakikisha ridhaa ya wananchi inalindwa hata pale ushindani wa vyama vingi unapokosekana.
Undani wa majimbo yanayosubiri kura ya ndio au hapana
Uchambuzi zaidi unaonyesha majimbo 46 yanayosubiri kura ya ndio au hapana, yapo katika mikoa 17 ya Tanzania Bara huku Zanzibar ikivunja rekodi ya kutokuwa jimbo hata moja ambalo litahusika na kura hiyo.
Mkoa wa Geita ndio unaongoza kuwa na majimbo mengi ambayo wagombea wake, kura ya ndio au hapana inawahusu.
Mkoa huo uliopo Kanda ya Ziwa una majimbo matano sawa na asilimia 10.8 ya majimbo yote yatakayopigiwa kura ya ndio au hapana. Majimbo hayo ni pamoja na Bukombe ambalo liko chini ya Dotto Biteko, Jimbo la Bukombe, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati.
Wagombea wengine wasio na washindani katika mkoa huo ni pamoja Chacha Mwita Wambura wa Geita Mjini, Rajab Seif wa Busanda, na Joseph Kasheku wa Geita, wakidhihirisha uimara wa CCM katika mkoa huo.
Mikoa mingine yenye majimbo mengi ni mkoa wa Rukwa, Kagera, Morogoro na Manyara ambapo kila mmoja umetoa majimbo manne.
Wagombea waliopitishwa bila upinzani katika Mkoa wa Rukwa ni Khalfan Hilaly wa Sumbawanga Mjini, Joackim Canoni (Kalambo), Moses Ludovico (Nkasi Kusini) na Clement Sangu wa Kwela, wote wakiwa wanachama wa CCM.

Enespher Kabati wa Kilolo ambaye ni moja kati ya wabunge wanawake waliodumu kwa muda mrefu anauwakilisha Mkoa wa Iringa. Wengine katika mkoa huo ni Exaud Silaoneka wa Mufindi Kaskazini, na Mwakiposa Kihenzile wa Mufindi Kusini.
Mkoa wa Kagera nao, una majimbo manne likiwemo jimbo la Biharamulo Magharibi ambapo John Chiwelesa anasubiri kupigiwa kura ya ndiyo au hapana.
Mikoa mingine ni Iringa, Singida, na Tanga ina majimbo matatu kila mmoja.
Mkoa wa Iringa unahusisha wagombea watatu akiwemo Enespher Kabati wa Kilolo, Exaud Silaoneka wa Mufindi Kaskazini, na Mwakiposa Kihenzile wa Mufindi Kusini.
Hali kama hiyo ipo pia Singida, ambako wagombea ni Yohana Stephen wa Jimbo la Itigi, Jesca Kishoa wa Iramba Mashariki, na Emmanuel Kingu jimbo la Ikungi Magharibi.
Kwa mkoa wa Tanga, wagombea wasio na wapinzani ni Mnzava Paul wa Korogwe Vijijini, Profesa Shemdoe Silas wa Lushoto, na Abdallah Shangazi wa Mlalo.
Mikoa yenye majimbo mawili ni pamoja na Lindi, ambako wapo Fadhili Ally, jimbo la Nachingwea na Buriani Nandala wa Ndanda.
Kwa mkoa wa Njombe wagombea wanaosubiri kura ya ndiyo au hapana ni Chongolo Godfrey wa jimbo la Makambako na Joseph Zacharius wa Ludewa huku, John Nchimbi wa jimbo la Nyasa na Jenista Mhagama katika jimbo la Peramiho wakiwakilisha mkoa wa Ruvuma.
Mkoa wa Shinyanga pia una majimbo mawili ambapo Njalu Silanga anasubiri kura ya ndiyo au hapana katika jimbo la Itilima na Kundo Mathew jimbo la Bariadi Mjini.
Hussein Bashe ambaye kwa sasa ni Waziri wa Kilimo naye kura ya ndio au hapana inamuhusu katika jimbo la Nzega Mjini pamoja na Abubakar Omari wa Manonga mkoani Tabora.

Kwa upande wa mikoa yenye jimbo moja moja, Arusha ambapo Ikayo Ndoinyo anawania nafasi jimbo la Ngorongoro, Katavi ambapo Moshi Selemani anasubiri kura ya ndiyo au hapana katika jimbo la Tanganyika.
Mikoa mingine ni Mbeya na Songwe ukitoa majimbo ya Kyela na Lupa ambapo Ulimboka Baraka na Njelu Kasaka wanagombea.
INEC yatoa msimamo
Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi ya mwaka 2024 inaeleza kuwa iwapo baada ya muda wa urejeshaji wa fomu za uteuzi kumalizika, jina la mgombea mmoja pekee ndilo litakalokuwa limepitishwa na Msimamizi wa Uchaguzi katika jimbo husika, basi mgombea huyo atachukuliwa kuwa amependekezwa bila pingamizi.
Hata hivyo, sheria hiyo inafafanua kuwa ili mgombea huyo aweze kutangazwa kuwa Mbunge, ni lazima apigiwe kura na wapiga kura wa jimbo husika, ambapo kila mpiga kura atapiga kura ya “Ndiyo” au “Hapana” kumpitisha au kumkataa mgombea huyo.
Kwa mujibu wa sheria hiyo, iwapo mgombea watapata kura nyingi za ndio, basi watawawakilisha wananchi wao bungeni kwa kipindi cha miaka mitano mpaka 2030.
Kura ya “Ndiyo” au “Hapana” ni utaratibu wa kikatiba na unaolenga kulinda haki ya wananchi ya kutoa maamuzi kwa hiari hata pale ambapo ushindani wa vyama vingi haupo.
Wananchi wanapewa nafasi ya kuamua iwapo wanamtaka au hawamtaki mgombea husika.
Kati ya wagombea 46 ni wangapi watapigiwa kura za hapana? Macho na masikio kwa wapiga kura wa majimbo husika baada ya matokeo ya ubunge kutangazwa na wasimamizi wa uchaguzi.
Latest