Simu kwa wapenda michezo ya mtandaoni hii hapa
Ukiwa unapendelea kucheza michezo ya mtandaoni, basi simu hii ya “ROG Phone 5s Pro” ni chaguo sahihi. Picha| Droid News.
- Ni simu aina ya “ROG Phone 5s Pro” ya kampuni ya Asus.
- Uwezo wake wa kumbukumbu ni GB18 na uhifadhi ni GB512
- Inauzwa kati ya Sh3.9 milioni hadi Sh4.1 milioni.
Dar es Salaam. Ni wazi kuwa mbali na kuwa chombo cha kuwasiliana, kila simu ina nguvu na madhaifu yake. Mfano kuna simu ambayo nguvu yake kubwa ni kamera huku nyingine ikiwa ni uhifadhi mkubwa.
Hivyo hivyo zipo simu ambazo nguvu yake ni muonekano mzuri lakini ukija kwenye utendaji kazi, utabaki ukisema “bora uhai”.
Kwa “ROG Phone 5s Pro” simu janja kutoka kampuni ya kutengeneza bidhaa za kielektroniki ya Asus, nguvu yake ni kuwafurahisha wanaopenda kutumia simu kwa ajili ya kucheza michezo ya video (video games).
Mbali na nguvu hiyo, huenda imezipiga vikumbo simu nyingi zilizoingia sokoni mwaka huu, (2021) kwa kamera, uwezo wa uhifadhi na mengineyo.
Imekuja na yapi?
Kinachoipa nguvu kwa wacheza magemu simu hii ni uwezo mzuri wa betri ambapo simu hii ina uwezo wa kudumu kwa saa sita mtu anapokuwa anacheza magemu mbalimbali na bado ikabakisha asilimia 20 za ziada.
Mdau wa magemu na teknolojia kutoka tovuti ya India Today amesema betri lenye uwezo wa mAh 6000 linaweza kutumia kucheza magemu mbalimbali ikiwemo “PUBG Mobile” ambayo yote yanahitaji utendaji kazi tofauti tofauti wa simu.
Kwa mtumiaji wa kawaida ambaye hachezi magemu, betri hilo lina uwezo wa kukaa na chaji kwa hadi saa 28 kulingana na matumizi.
Simu hii pia inaruhusu kuchaji kwa haraka (quick charge) na inatumia chaja ya “type C kwa type C” kuchajia.
Boksi lake linakuja na kipini cha kutolea laini, chaja ya simu, kipozeo cha simu (AeroActive Cooler 5) pamoja na jaLada la simu.
Kama unapendelea earphones, itabidi ukazinunue kivyake.
Soma zaidi:
- Yaliyomo: Simu mpya ya Motorola kutambulishwa sokoni wiki hii
- Samsung A52: Simu ya Watanzania wa uchumi wa kati
- Ushindani wa Simu: Sony yaingiza simu mpya sokoni
Mengine ya “kujimwambafai”
Asus ROG Phone 5s Pro inaambatana na vihisishi (sensor) ikiwemo seezi (fingerprint) zilizowekwa ndani ya skrini pamoja na utambuzi uso (facial recognition) ambavyo ni muhimu kwa ulinzi wa simu.
Simu hii ina uwezo wa kutumia laini mbili za simu zinazotumia mtandao wa 5G/4G/3G au 2G kulingana na eneo la mtumiaji.
Simu hii ina spika tisa ambazo zimetengenezwa kuhimili sauti za juu na za chini bila kuipatia sauti ukakasi. Kwa wacheza magemu, wanafahamu umuhimu wa sauti kali.
Ingawa simu hizo zinauzwa kwa bei ya juu lakini zina uwezo mkubwa wa kiutendaji hasa kudumu na chaji kwa muda mrefu. Picha| Droid News.
Wengine wajipange
Licha ya kuwa simu hii imewekezwa kwa wacheza magemu, huenda ikawafaa pia watengeneza maudhui ya video na picha kwani kamera zake siyo za mchezo.
5s Pro ya Asus ina kamera inayoweza kurekodi video za 8K (Uwezo wa juu zaidi wa kurekodi video bora kwenye simu janja), uwezo wa kurekodi video za kasi ndogo (slow motion) na uwezo wa kupiga picha wakati wa kurekodi video (hili linafanyika hata kwa simu zingine).
Kamera kuu ya simu hii ina uwezo wa “MegaPixel” (MP) 64 na kamera ya mbele ina uwezo wa MP 24.
Simu hii ina kamera nne. Moja mbele na tatu nyuma ambapo mbali na kamera ya MP64, inaambatana na kamera ya picha pana (MP13) na kamera ya picha za karibu almaarufu kama “macro” (MP5).
Ikilinganishwa na Samsung Galaxy S21 Ultra 5G, Asus anasubiri sana kwani Samsung ina MP 108 lakini amefanikiwa kumpiga kikumbo Apple iPhone 13 Pro ambayo kamera kuu ina MP12.
Hivyo hivyo kwa kamera ya mbele. Samsung anaongoza kwa kuwa na MP 40, Rog ikiwa na Mp24 na mwisho, iPhone ikiwa na MP 12. Mlinganyo huu umezingatia baadhi ya matoleo ya “Pro”.
Bei yake ni ya moto
Hata tusizunguke sana, Rog 5s inauzwa kwenye jukwaa la AliExpress kwa Sh3.9 milioni hadi Sh4.1 milioni ikiwa ni nje ya gharama za usafiri kuja Tanzania.
Bei hiyo ni juu ya simu zote ambazo Nukta Habari imezilinganisha nayo na ni zaidi ya simu zote ambazo Nukta Habari imezifanyia uchambuzi kwa mwaka huu.
Uwezo wake wa kumbukumbu (RAM) ni GB18 huku uhifadhi (storage) ikiwa ni hadi GB512.
Latest
