Samsung A52: Simu ya Watanzania wa uchumi wa kati
- Inapatikana kwa bei ya Sh850,000.
- Kamera, betri na uhifadhi unasadifu bei ya simu hiyo.
- Inatajwa kuwa na mapungufu kadhaa ikiwemo kutumia mfuniko wa plastiki.
Dar es Salaam. Mahitaji ya simu hutofautiana kati ya mtu na mtu. Wengine hununua simu kwa kigezo cha kamera, betri, uzuri wa simu na hata kiasi cha pesa walichonacho.
Kwa mwaka 2021, simu nyingi zilizoingia sokoni zimekuja na bei ambazo hazishikiki na Mtanzania mwenye uchumi wa hali ya kawaida zikiwemo Samsung Galaxy S21 Ultra ambayo inauzwa kwa Sh3.5 milioni), OnePlus 9 pro (Sh2.5 milioni) na Sony Xperia 1 ii kwa Sh2.8 milioni.
Kulingana na matoleo hayo, Samsung haikusita kuingiza sokoni simu ya Samsung A52, ambayo watu wa uchumi wa kati wanaweza kumudu kununua.
Kinaga ubaga na Samsung Galaxy A52
Simu hiyo ambayo imeingia sokoni hivi laribuni inaambatana na sifa ambazo sinatosheleza matumizi ya kawaida ya simu janja. Licha ya kuwa baadhi ya vitu vinafikirisha, bado simu hiyo inafaa ikilinganishwa na bei yake.
Simu hiyo inaambatana na betri la mAh4500 ambalo lina uwezo wa kutumika kwa hadi siku mbili kulingana na matumizi. Uwezo huo ni sawa na baadhi ya simu zinazogharimu mamilioni ikiwemo Samsung Galaxy S20 ambayo betri yake ina uwezo wa mAh4000 huku bei yake ikiwa ni Sh1.36 milioni katika baadhi ya maduka ya Tanzania.
Simu hiyo inakaa na chaji muda mrefu kuliko simu ya Sony Xperia 1ii.
Pia utahitaji nusu saa tu kuichaji simu hiyo ifikie asilimia 50 ya ujazo wa betri lake ambayo inaweza kukufaa kwa siku nzima.
Hata hivyo simu hii bado ni haba kwa mabetri ya simu zingine ikiwemo Samsung S21 ambayo betri yake ina uwezo wa mAh5000.
Muonekano wa simu aina ya Samsung A52 ambayo imeingia sokoni hivi karibuni. Picha| Mtandao.
Kamera siyo haba
Kwa watumiaji wengi wa simu janja, simu ni picha na kama simu ina bei kubwa lakini kamera yake ni uchwara, simu hiyo haina nafasi katika mifuko yao wala pochi zao.
Samsung A52 inaambatana na kamera tatu ambapo kamera kuu ina uwezo wa kupiga picha zenye ubora wa Mega Pixel (MP) 64 ambayo ni juu ya Sony Xperia 1ii ambayo kamera yake ina uwezo wa MP 12.
Pia iko vyema kikamera kwa upande wa kupiga picha za mtindo wa selfie ambapo ina uwezo wa kupiga picha kwa MP 32 na kuzihifadhi kwa uwezo wa Gigabytes (GB) 128 hadi GB 256 ambao kwa watengeneza maudhui ni embe dodo chini ya mnazi.
Vingine vya kufurahia
Kwa wengi ulinzi wa simu ni kila kitu kwani haihitaji taarifa zako zilizopo katika simu zifikiwe na mtu yeyote anayeishika simu yako.
Galaxy A52 imeambatana na mfumo wa ulinzi kwa njia ya kuskani sura yaani “facial recognition”, alama za vidole na neno siri au msimbo. Uzuri wake ni kuwa sehemu ya kuskani alama ya vidole haipo nyuma hivyo kuungana na simu zingine zinazoingia sokoni mwaka huu kwa kuweka sehemu ya kuskani alama ya vidole kwenye skrini ya mbele.
A52 bado ina sehemu ya kawaida ya kuchomeka earphones, sehemu ya kuwekea kadi ya kumbukumbu huku ikiruhusu matumizi ya laini mbili.
Pia tofauti na simu zingine za uchumi wa kati, simu hii ina uwezo wa kukaa ndani ya maji kwa nusu saa hivyo kufaa kwa kwa mama, bibi, dada na hata kijana wa nyumbani ambaye kudumbukiza simu kwenye beseni la maji ni kitu cha kawaida.
Zinazohusiana:
- Yaliyojificha ndani ya programu mpya endeshi ya iPhone
- Tecno Spark 5: Simu maalum kwa wapenzi wa picha
- Sifa za simu mpya za Samsung zilizoingia sokoni Agosti 7
Huenda usifurahie haya
Katika zama za mwaka 2020 hadi 2021, matumizi ya plastiki kwenye simu janja yalikuwa yamepungua lakini Samsung imeamua kuendelea nayo katika simu hii.
Huenda mtu aliyezowea simu za kioo mbele na nyuma akakatishwa tamaa na simu hii.
Pia inaelezwa kuwa sehemu ya kuskani alama za video ya simu hiyo inasumbua na kumhitaji mtumiaji kubonyeza sehemu hiyo mara nyingi ndiyo ifanye kazi.
Pamoja na sifa zote nzuri zinazoambatana na simu hii huku bei yake ikiwa ni Sh850,000 katika baadhi ya maduka nchini ambayo Watanzania wa uchumi wa kati wanaweza kumudu kununua.
Endelea kusoma Nukta Habari (www.nukta.co.tz) kwa habari za teknolojia inayokuhusu.