Yaliyomo: Simu mpya ya Motorola kutambulishwa sokoni wiki hii

April 27, 2021 7:51 am · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni simu mpya aina ya Moto G20.
  • Itashindana na simu zingine zilizoingia sokoni mwaka 2021.
  • Simu hiyo ina kamera ya kawaida, betri ambalo ni zaidi ya simu za mamilioni.

Dar es Salaam. Kama wewe ni mtumiaji wa simu za kampuni ya Motorola, kaa mkao wa kula maana wiki hii wanakusudia kuingiza sokoni simu mpya aina ya Moto G20 ili kuendeleza ushindani katika soko la simu duniani. 

Moto G20 itaingia sokoni kupambana na simu mbalimbali kutoka makampuni makubwa duniani ambazo tayari zimetambulisha simu zao mwaka huu. 

Miongoni mwa simu hizo ni Samsung S 21 Ultra, Sony na OnePlus huku Samsung ikiitambulisha  Galaxy A52 ambayo gharama yake ni Sh850,000. 

Moto G20 ni simu inayotarajiwa kuingia sokoni wiki hii licha ya bado haijatajwa tarehe husika ya kuzinduliwa. 

Sifa kubwa ya simu ya Moto G20 ni betri yenye nguvu ya mAh5,000 ambayo uwezo wake ni kustahimili matumizi ya kawaida yanayoweza kudumu kwa siku mbili au zaidi. 

Betri hilo ni zaidi ya betri la Galaxy A52, iPhone12 na Samsung Galaxy S21 ambazo uwezo wake ni mAh4,000 hadi 4,500.

Moto G20 inaambatana na betri linaloweza kukaa na chaji kwa siku mbili au zaidi. Picha| GSM Arena.

Sifa nyingine ya simu hii ni ukubwa wa skrini yake na hivyo kufaa kwa matumizi mbalimbali ikiwemo kucheza michezo ya kielektroniki, kuangalizia filamu, kuandikia na hata kusomea kwa wanafunzi.

Moto G20 inaambatana na skrini yenye ukubwa wa inch 6.5 ambao ni sawa na Samsung Galaxy A52 na Realme C20 inayotengenezwa na kampuni ya Oppo ya nchini China.

Kamera za Moto G20 siyo haba japo kushindana na simu za mwaka 2021 inaweza kuwa kibarua kizito. Simu hiyo ina kamera tatu na kamera kuu ina Mega Pixel (MP) 48, kamera ya upana (ultra wide) ina MP8 na ya kupiga picha za karibu (macro) ikiwa na MP2. 

Picha za mbele yaani “selfie” za simu hiyo zitapigwa na kamera yenye uwezo wa MP13 ambayo ni chini sana ikilinganishwa na simu zingine.


Soma zaidi: 


Moto G20 inakuja na uhifadhi wa Gigabytes (GB) 4 kwa RAM (uhifadhi wa muda mfupi) na GB 64 hadi 128 kwa ROM (uhifadhi wa muda mrefu) ambao pia unaweza kuongezeka kwa kuweka kadi ya kumbukumbu (memory card)

Je unahisi gharama ya Sh417,420 ambayo ni bei yake ya kiwandani nje ya kodi inakufaa kwa matumizi yako? Kama ndiyo, unaweza kuipata kupitia duka rasmi la Motorola pale itakapotoka rasmi wiki hii.

Usikae mbali na Nukta Habari ambayo inakujuza mambo yote uhimu yanayohusu teknolojia.

Enable Notifications OK No thanks