Simbachawene: Imarisheni ulinzi wa sungusungu
- Amesema vikundi hivyo vitasaidia kupunguza uhalifu kwenye jamii.
Dar es Salaam. Waziri wa Mambo ya ndani, George Simbachewe ameagiza kuimarishwa kwa vikundi vya ulinzi shirikishi vikiwemo vya sungusungu ili kudhibiti vitendo vya kihalifu na wizi mdogo mdogo unatokea kwenye jamii.
Agizo hilo la Simbachawene linaweza kuwa ni utekelezaji wa agizo la Rais Samia Suluhu Hassan alilolitoa wakati akizungumza na Wazee jijini Dar es Salaam leo (Ijumaa Mei 7, 2021) kuwa Jeshi la Polisi na jamii idhibiti tabia za wizi, uporaji na ujambazi ambazo zimeanza kuibuka tena hasa katika majiji makubwa likiwemo la Dar es Salaam.
Akizungumza leo Mei 17, 2021 jijini Mwanza alipofanya ziara ya kutembelea vitengo mbalimbali vya Jeshi la Polisi likiwemo dawati la jinsia, uhamiaji na Gereza la Butimba, Waziri Simbachawebe ameeleza kuridhishwa na utendaji kazi wa polisi ambao umesaidia kupunguza uhalifu majini na nchi kavu.
Hata hivyo, amesema jeshi hilo linapaswa kuimarisha ulinzi wa raia na mali zao kwa kuhakikisha sungusungu wanafanya kazi zao vizuri kwenye mitaa mbalimbali ili kutokomeza uhalifu wa kila namna.
Soma zaidi:
“Tunatambua kuwepo kwa changamoto nyingi za uhalifu ndani ya Ziwa na kama hakuna boti la kusaidia katika kupambana inaweza kuongeza uhalifu hivyo ni vema boti litengenezwe na gharama zitumwe haraka,” amesema Waziri huyo wakati alipotembelea kikosi ya majini jijini hapa.
Mbali na kitengo hicho pia Waziri huyo ametembele kikosi cha Jeshi la Zimamoto na kuagiza kufanyika uchunguzi wa kina kwa matukio ya moto mashuleni na kueleza kuwa mengi hufanywa kwa hujuma za wanafunzi.
“Ninaagiza kufanyika kwa uchunguzi wa kina kwenye matukio ya moto mashuleni ambapo mengi yamebainika kufanywa na wanafunzi kwa utundu wao na wenye lengo la kuhujumu, matukio haya yachunguzwe na yapatiwe suluhu na si kuishia hewani, ” amesisitiza.
Latest