Rais Samia: Jeshi la Polisi msitumie sheria kama kitega uchumi

May 18, 2021 9:17 am · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link
  • Alitaka litumie sheria kudhibiti uhalifu na siyo kukusanya mapato.
  • Awataka askari polisi kutoa elimu zaidi kuliko kutoa adhabu na faini.

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amelitaka Jeshi la Polisi Tanzania kutumia sheria na adhabu kudhibiti uhalifu kuliko kuzitumia kama kitega uchumi cha kujipatia mapato yotokanayo na faini na tozo za makosa yakiwemo ya usalama barabarani. 

Rais Samia aliyekuwa akizungumza leo Mei 18, 2021 wakati akifungua kiwanda cha ushonaji cha Jeshi la Polisi kilichopo Kurasini jijini Dar es Salaam amesema kazi muhimu na ya kwanza ya askari polisi ni kulinda usalama wa raia na mali zao na siyo kukusanya mapato.

“Jeshi la Polisi, sheria zetu tunazozitunga ni sheria za udhibiti. Sasa tusijielekeze sana kutumia sheria na ile component (sehemu) ya makosa na adhabu kwamba ni kitega uchumi kwa ajili ya jeshi letu, zaidi zitumike kudhibiti kuliko ukusanyaji wa faini na tozo zingine,” amesema Rais Samia. 

Amelitaka jeshi hilo liongeze juhudi katika kutoa elimu kwa raia kuhusu umuhimu wa ulinzi na kuendeleza amani na utulivu ili kupunguza makosa ya uhalifu.

“Na hapa nihimize suala zima la elimu kwa raia. Muongeze jitihada wananchi wawasikie zaidi na wawaelewe ili kupunguza haya. Ni vyema tujielekeza katika elimu kuliko kutumia sheria kama vitega uchumi,” amesisitiza Rais. 


Soma zaidi: 


Kiongozi huyo mkuu wa nchi ametoa tahadhari hiyo baada ya Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) Simon Sirro kusema uhalifu na fedha zinazokusanywa kutokana na makosa mbalimbali zimepungua kutokana na kudhibitiwa kwa makosa hayo nchini.

“Ukilinganisha Januari  hadi Aprili 2020 na Januari  hadi Aprili, 2021 uhalifu umepungua kwa asilimia 13.5, ajali za barabarani zimepungua kwa asilimia 29.1,” amesema IGP Sirro wakati wa kufungua kiwanda hicho. 

Amesema kupungua huko kwa makosa hayo kumesababisha kupungua pia kwa kiwango cha makusanyo ya faini za makosa ya barabarani hadi Sh50.1 bilioni katika kipindi cha Julai 2020 hadi Aprili 2021 kutoka Sh56 bilioni mwaka jana Julai 2019 na Julai 2020.

IGP Sirro amesisitiza kuwa jeshi hilo halifanyi kazi ya kukusanya mapato, bali fedha hizo zinatokana na kukiukwa kwa sheria mbalimbali, kinyume na malalamiko ya watu kuwa jeshi hilo limejielekeza zaidi kukusanya fedha kuliko kutoa elimu kwa raia. 

Mradi wa ujenzi wa kiwanda cha kisasa cha ushonaji cha Kurasini kwa mujibu wa Jeshi la Polisi,  ulizinduliwa Mei 30, 2020 na umegharimu Sh666.4 milioni.

Kiwanda hicho kina uwezo wa kuchukua watendaji 250 na vyerehani 200 ambapo Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Khamis Chilo amesema kitasaidia kuongeza uzalishaji wa sare za maafisa, wakaguzi na askari, tatizo ambalo lilikuwa halijapata ufumbuzi kwa muda mrefu.

Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
Rais Samia azindua minara 758, aacha maagizo mazito juu ya mkongo wa taifa

Rais Samia azindua minara 758, aacha maagizo mazito juu ya mkongo wa taifa

Nukta TV

JAJI MKUU: Njia za asili ni mojawapo ya njia halali za utatuzi wa migogoro

JAJI MKUU: Njia za asili ni mojawapo ya njia halali za utatuzi wa migogoro

Nukta TV

Hesabu ya bosi, bei ya mafuta pasua kichwa madereva wa daladala

Hesabu ya bosi, bei ya mafuta pasua kichwa madereva wa daladala

Nukta TV