Polisi kumsaka Mo Dewji nje ya Tanzania

October 19, 2018 6:41 pm · Nuzulack Dausen
Share
Tweet
Copy Link
  • IGP Simon Sirro amesema wanawasiliana na polisi wa kimataifa (Interpol) baada ya uchunguzi wa awali kuonyesha kuwa gari linalodaiwa kuhusika kumteka limetokea nchi jirani.
  • Pia, amesema watatumika wachunguzi wa ndani kwenda katika baadhi ya nchi jirani kuhakikisha anapatikana.

Dar es Salaam. Jeshi la polisi limetanua wigo wa kumtafuta mfanyabiashara aliyetekwa Mohammed Dewji hadi nchi jirani baada ya kutangaza kuwa wanawasiliana kwa karibu na polisi wa kimataifa (Interpol) katika jithada za kumpata bilionea huyo.

Mkuu wa Jeshi la Polisi, Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Simon Sirro amewaambia wanahabari leo Ijumaa (19 Oktoba 2018) kuwa wameamua kushirikiana na Interpol baada ya uchunguzi wa awali kubainisha kuwa gari ambalo huenda lilihusika kumteka Dewji lililotokea nchi jirani.

Amesema baada ya timu ya uchunguzi kwenda mpakani mwa Tanzania na nchi hiyo ambayo hakuitaja, ilibainika kuwa gari aina ya Toyota Surf lilionekana maeneo hayo Septemba mosi mwaka huu.

“Tumepata ‘details’ za kutosha ambazo hatuwezi kuzisema na ufuatiliaji wetu unafanyika. Lakini kubwa zaidi ni kwamba tunawasiliana na wenzetu wa Interpol na ufuatiliaji unafanyika. Nani mwenye lile gari imefahamika na nchi anayotoka, nani aliyekuwa dereva  lile gari tumefahamu kwahiyo watu wetu wa Interpol wanafanya hiyo kazi,” amesema Sirro na kuongeza;

“Pia, tatahakikisha  watu wetu wanazunguka baadhi ya nchi jirani kuhakikisha kuwa tunampata (Dewji).”

Hata alipoulizwa na wanahabari juu ya jina la nchi ambayo gari hilo linadaiwa kutokea, bosi huyo wa polisi amesema kuwa ni mapema sana kuitaja kwa kuwa jambo hilo linaweza kuliingiza taifa katika mvutano.


Zinazohusiana: RC Makonda aeleza mazingira ya kutekwa Bilionea Mo Dewji

Dau la Bilioni 1 kutolewa kwa atakayefanikisha kupatikana kwa Bilionea Mo Dewji


Leo ni siku ya nane tangu Dewji apotee baada ya kutekwa na watu wawili wageni wenye silaha mapema Oktoba 11, 2018 katika hoteli ya Colesseum Masaki Jijini hapa. Hadi sasa bado haijafahamika lengo la kutekwa Dewji huku polisi wakieleza kuwa itafahamika baada ya mfanyabiashara huyo au watekaji kukamatwa.

Katika mkutano huo na vyombo vya habari, Sirro amesema kuwa uchunguzi kupitia picha za CCTV umebaini mara baada ya kumteka Dewji katika hoteli hiyo gari hilo lilitokomea na kuingia Barabara ya Ali Hassan Mwinyi na kisha kuingia katika mzunguko wa kwenda Kawe.

“Bado watu wetu wanafuatilia kama walienda Silver Sand ama Kawe”, IGP Simon Sirro.

Kutokana na uwepo wa taarifa hizo, ameeleza kuwa polisi watafanya msako wa nyumba kwa nyumba katika eneo la mwisho kuonekana kwa gari hilo ili kuhakikisha anapatikana.

Wanahabari wakiwa katika mkutano na IGP Sirro mapema Oktoba 19 mwaka huu ambapo Mkuu huyo wa polisi alibainisha kuanza kushirikiana na Interpol kumsaka Mo Dewji. Picha| Nuzulack Dausen.

Ili kujilinda  na matukio kama lililomtokea Dewji, Sirro amewashauri watu wenye uwezo wa kumiliki silaha hasa wale matajiri wafanye hivyo kujihami kwa kuwa sheria inaruhusu na kwamba uhalifu wa aina hiyo unaweza kufanyika hata na watu wa nje ya nchi wenye nia ovu.

Hata hivyo, Sirro alitupilia mbali ombi la baadhi ya watu wanaoisihi Serikali kuomba nguvu ya vyombo vya nje vya uchunguzi kufuatilia suala la kutekwa kwa bilionea huyo akieleza kuwa vyombo vya ulinzi vya ndani vina uwezo na weledi wa kutosha kukamilisha kazi hiyo.

Mapema wiki hii Waziri Kivuli wa Mambo ya Ndani, Godbless Lema alisema kuwa ni vyema Serikali ikaomba msaada kutoka mashirika ya kijasusi ya nje ili ijitoe na lawama ya kuhusika katika matukio ya utekaji.

Serikali kwa nyakati kadhaa imepinga suala hilo ikieleza kuwa vyombo vya ndani vinatosha kufanya uchunguzi huo.

Enable Notifications OK No thanks