Maagizo 7 ya Rais Samia kwa Jeshi la Polisi

June 9, 2025 5:58 pm · Kelvin Makwinya
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni pamoja na kuzingatia maadili, kuongeza mapambano dhidi ya dawa za kulevya pamoja na kulinda amani wakati wa uchaguzi. 

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ametoa maagizo saba kwa Jeshi la Polisi yanayolenga kuboresha utendaji kazi wa jeshi hilo ikiwemo kuzingatia maadili, kuongeza mapambano dhidi ya dawa za kulevya pamoja na kulinda amani wakati wa uchaguzi. 

Rais Samia aliyekuwa akihutubia katika sherehe za kuhitimisha mafunzo ya Maofisa na Wakaguzi wa Polisi leo Juni 9, 2025 katika viwanja vya vya Chuo cha Taaluma ya Polisi Jijini Dar es Salaam amewaambia wahitimu kuwa wanapaswa kutekeleza majukumu yao kwa weledi na kusimamia viapo vyao.

Rais Samia amewaambia wahitimu kuwa wanapaswa kutekeleza majukumu yao kwa weledi na kusimamia viapo vyao. Picha | Ikulu Mawasiliano.

Aidha, Rais Samia amelitaka jeshi hilo kuongeza nguvu katika usimamizi wa usalama wa raia barabarani ili kupunguza vifo na majeruhi wanaosababishwa na ajali.

Kwa mujibu wa Rais Samia jumla ya matukio 1,322 ya ajali barabarani yameripotiwa katika kipindi cha miezi minne kati ya Januari mpaka Aprili 2025 huku vifo vikiongezeka kwa asilimia tisa na kufikia 1,275 kulinganisha na mwaka 2024.

Rais Samia pia amelitaka Jeshi la Polisi kuimarisha mafunzo, kuhakikisha kuwa mifumo ya Tehama ya Jeshi la Polisi inasomana ili kuongeza weledi wa utendaji wa kazi, kuongeza mapambano dhidi ya rushwa na zaidi kuimarisha amani na usalamakipindi cha uchaguzi.

Kwa upande wake Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania, IGP Camillus Wambura licha ya kumshukuru Rais Samia kwa kuimarisha miundombinu na upatikanaji wa vifaa na vitendea kazi ndani ya Jeshi la Polisi ameahidi jeshi lake litasimamia uwepo wa amani kabla, wakati na baada ya uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu

Kwa mujibu wa risala iliyosomwa na Naibu Kamishina wa Polisi, Lazaro Mambosasa, jumla ya  maafisa 787 kati yao wanaume 632 na wanawake 145 waliripoti kwenye mafunzo ya maafisa na wakaguzi wasaidizi.

Kati ya maafisa walioripoti, Inspekta Rosemary Mapango alifariki kwa maradhi wakati mafunzo hayo yakiendelea na hivyo kufanya idadi ya maafisa kubakia 786.

Hata hivyo, waliohitimu kwa kupimwa kitaaluma katika masomo ya darasani, mafunzo kwa vitendo na mwenendo wa tabia na maadili ni maafisa wasaidizi 174 ambapo kati ya hao wanaume ni 133 na wanawake ni 41. 

Aidha, maafisa saba waliondoshwa mafunzoni kwa kushindwa kufikia viwango vya chuo kwa kujihusisha na vitendo vya utovu wa nidhamu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks