Shule, vyuo kuendelea kufungwa Tanzania, wagonjwa wa corona wakifikia 53
- Rais John Magufuli asitisha maadhimisho ya Sherehe za Muungano na Mei Mosi kujikinga na corona
- Sh500 milioni zilizopangwa kwa ajili ya Sherehe za muungano kuipiga jeki Zanzibar
- Shule na vyuo vitaendelea kufungwa hadi hapo itakapotangazwa
- Dar es Salaam yaendelea kuongoza kuwa na wagonjwa wengi wa COVID-19
Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imesema shule za awali, msingi, sekondari na vyuo vyote vya elimu ya kati na vya elimu ya juu vitaendelea kufungwa kama ilivyoagizwa awali hadi hapo itakapotoa tamko jingine ili kuzuia kusambaa kwa virusi vya ugonjwa wa corona (COVID-19) vilivyoathiri watu 53 hadi sasa.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameeleza leo kuwa sanjari na agizo hilo Rais John Magufuli amesitisha maadhimisho ya Sherehe za Muungano pamoja na Sikukuu ya Wafanyakazi (Mei Mosi) ili kuepuka msongamano na kuendelea kuzuia virusi vya corona visisambae zaidi. Sherehe hizo zilipangwa kufanyika Aprili 26 na Mei Mosi mtawalia.
Majaliwa ameeleza leo (Aprili 14, 2020) katika kikao cha Kamati ya kitaifa ya uratibu wa mapambano dhidi ya COVID-19) kuwa hadi leo Tanzania ina watu 53 waliobainika kuwa na virusi vya corona ikiwa ni ongezeko la wagonjwa wanne kutoka walioripotiwa na Wizara za afya za Zanzibar na Tanzania Bara jana.
Wagonjwa wote wanne wapya wapo jijini Dar es Salaam. Hata hivyo, taarifa ya Ofisi ya Waziri Mkuu haikuweka bayana jinsia zao na umri.
Wagonjwa hao wapya waliotangazwa leo wanaifanya Dar es Salaam kuendelea kuwa kitovu kwa kuwa na wagonjwa 36 kati ya 53 waliopo nchini sawa na theluthi mbili ya watu wote waliobainika kuambukizwa ugonjwa huo unaosambaa kwa kasi ulimwenguni. Hii ina maana kuwa kwa kila wagonjwa watatu waliopo Tanzania wawili wapo Dar es Salaam.
Soma zaidi:
- WHO kutathmini upya marufuku ya kutoka nje kudhibiti Corona
- Wagonjwa wa Corona wazidi kuongezeka Tanzania
- Unayotakiwa kufahamu kuhusu virusi vya Corona
Majaliwa amesema Serikali bado haijatangaza kufunguliwa kwa shule, vyuo na shughuli za michezo pamoja na misongamano isiyokuwa ya lazima, hivyo maeneo hayo yataendelea kusalia katika karantini na wanafunzi wote wandelee kubakia majumbani kwao.
Machi 17 na 18 mwaka huu Serikali ilitangaza kuzifunga shule za awali, msingi, sekondari na vyuo vyote vya elimu ya kati na vya elimu ya juu kwa muda wa siku 30.
Serikali ya Zanzibar yapigwa jeki
Kutokana kusitishwa kwa sherehe hizo, Majaliwa ameeleza kuwa Rais Magufuli ameagiza Sh500 milioni ambazo zilitengwa kwa ajili ya maadhimisho ya miaka 56 ya Sherehe za Muungano zipelekwe kwenye mfuko wa kupambana na COVID-19 wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Majaliwa amewaomba wadau mbalimbali waendelee kuiunga mkono Serikali katika mapambano dhidi ya virusi vya corona kwani janga hilo ni kubwa na wanaweza kutuma fedha kupitia akaunti Na: 9921159801 yenye jina la National Relief Fund Electronic.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiteta na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, kwenye kikao cha Kamati ya Kitaifa ya Uratibu wa Mapambano dhidi ya Ugonjwa wa Homa kali ya Mapafu (COVID – 19), kilichofanyika jijini Dodoma, Aprili 14, 2020. Picha|Ofisi ya Waziri Mkuu.
Waziri Mkuu amesema elimu ya tahadhari inapaswa kuendelea kutolewa kwa wananchi ili waweze kujikinga na maambukizi ya homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi vya corona.
“Kama si lazima kutoka, wananchi waendelee kutulia majumbani mwao,” amesema Majaliwa.
Kiongozi huyo wa nchi ameagiza kuwa wataalamu wanaosimamia utoaji wa huduma katika maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya wa watu wenye maambukizi ya COVID-19, wakiwemo madaktari wote wapewe vifaa vya kijikinga ili kuhakikisha hawapati maambukizi ya ugonjwa huo.
Amesema watu waliokutana na wagonjwa waendelee kufuatiliwa kwa umakini na wahusika wawashirikishe viongozi wote hadi wa ngazi za chini na kwamba athari za kiuchumi zinazojitokeza kufuatia ugonjwa huo ziendelee kuchambuliwa.
Latest
