Shughulikieni changamoto vifaa vya kudhibiti ajali barabarani-Wadau
- Kutatuliwa kwa changamoto hizo kutasaidia kuongeza ufanisi wa mfumo huo na kupunguza ajali za barabarani.
- Mfumo huo wa kifaa cha kielektroniki cha VTS (Vehicle Tracking System) kinafuatilia mwenendo wa mabasi ya masafa marefu.
- Madereva washauri magari yote yakiwemo malori yafungiwe kifaa hicho.
Dar es Salaam. Siku moja baada ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isaack Kamwelwe kuzindua mfumo wa kifaa cha kielektroniki cha VTS (Vehicle Tracking System) kinachofuatilia mwenendo wa mabasi ya masafa marefu, wadau wa usafiri wamependekeza kutatuliwa kwa changamoto za mgongano wa maslahi na ufanisi wakati wa utekelezaji wa mfumo huo.
Kwa mujibu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafari wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) kifaa hicho kilianza kutumika kwa majaribio tangu mwaka 2016 ambapo mpaka sasa kimefungwa katika mabasi 2, 840 na kuunganishwa katika mfumo wa kufuatilia mwenendo wa vyombo vya usafiri nchini.
Wakati akizindua VTS jana (Januari 9, 2019), Mhandisi Kamwelwe alisema kifaa hicho kitasaidia kupunguza vifo, vilema na hasara inayotokana na ajali za barabarabi kwasababu mabasi yote yatakuwa yanafuatiliwa kwa karibu.
Hata hivyo, wadau wa usafiri wamesema ili kuongeza ufanisi wa mfumo huo, kuna kila sababu ya kutatua changamoto ya mgongano wa maslahi kati ya polisi wa usalama barabarani, Sumatra na chama cha wamiliki wa mabasi (TABOA) ambao wote wanawajibika na usimamizi wa mabasi ya mikoani.
Mkurugenzi wa Idara ya Tehama katika kampuni ya Fleet Track inayotoa huduma ya VTS, Joshua Mshanga ameiambia www.nukta.co.tz kuwa kabla mfumo huo haujatambulika rasmi ulileta msuguano miongoni mwa wadau wenye jukumu la kulinda usalama wa abiria na magari.
“Ni vizuri imekua rasmi maana kulikuwa na mgongano kati ya Taboa, Sumatra na polisi, VTS italeta manufaa kwa madereva na wenye magari,” amesema Mshanga.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isaack Kamwelwe akifuatilia uzinduzi wa mfumo wa kifaa cha kielektroniki cha VTS (Vehicle Tracking System) kinachofuatilia mwenendo wa mabasi ya masafa marefu. Anayemuelekeza ni Mkurugenzi Mkuu wa Sumatra, Hilliard Ngewe. Picha| Mwananchi.
Sambamba na hilo ni utoaji wa elimu ya matumizi ya vifaa hivyo kwa madereva, abiria na wadau wengine wanaosimamia usalama barabarani hasa katika kudhibiti mwendo kasi.
“Elimu itolewe zaidi na Sumatra kuhusu matumizi ya VTS,” amesema Mshanga huku akiwalalamikia baadhi ya madereva, “waache kuharibu vifaa maana wanahatarisha maisha ya abiria, wachukulie kama sehemu ya usalama wao.”
Mabasi yote ya mikoani sasa yatalazimika kufunga vifaa hivyo vya VTS ambavyo taarifa zake hutumwa Sumatra kwa ajili ya kudhibiti mwendo wa madereva waluwalu katika safari zao.
Pia wadau wa usalama barabarani wamependekeza ratiba zinazotolewa na Sumatra za mabasi ya mikoani zipitiwe upya ili ziendane na mfumo mpya wa kufuatilia mwendo wa mabasi ambayo hayaruhusiwi kutembea zaidi ya kilomita 80 kwa saa (80km/hr).
“Ratiba mpya itolewe kwasababu unaweza kukuta gari linafika muda uleule wa zamani ilihali spidi imedhibitiwa,” amesema Imani Mangowi, balozi wa usalama barabarani kutoka mkoa wa Kilimanjaro.
Mangowi ameiambia www.nukta.co.tz kuwa ufungaji wa VTS kwenye mabasi umekuja wakati muafaka na anawashauri madereva kufuata sheria za usalama barabarani na watumie vifaa hivyo kwa uhalali.
Changamoto nyingine inayohitaji suluhisho ni kuweka uwiano wa spidi hasa kwa malori ya mizigo ambayo hayahusiki na ufungaji wa vifaa hivyo, jambo linalowapa wakati mgumu madereva wa mabasi kutumia barabara.
“Wahakikishe wanafunga kwenye vyombo vyote, unaweza kuwa barabari ukitaka kumpita mwenzio (overtake) hasa malori wanaongeza spidi makusudi wakijua kabisa kilomita 80 kwa saa ndio mwisho wako(dereve wa basi) hivyo hii inaweza kupelekea ajari,” amesema Ally Bakongo, mmoja wa madereva wa mabasi ya mkoani.
Zinazohusiana:
- VTS: Vifaa vya kudhibiti ajali vinavyoogopwa na madereva waluwalu
- Serikali yaangazia daladala, mabasi ya mikoani kuongeza mapato kielektroniki
Faida za vifaa vya VTS unasaidia kuunguza gharama za mafuta kwa sababu spidi inadhibitiwa na kulifanya gari litembee kwa muda uliopangwa. Pia inaokoa gharama za matengenezo ya mara kwa mara hasa ubadilishaji wa matairi.
Hata hivyo, Afisa Mwandamizi wa Mawasiliano wa Sumatra, Salum Pazzy amesema kuwa mfumo huo wa VTS umeanza kutumika katika kanda zote wanazosimamia na wanaendelea kutatua changamoto zinazojitokeza ili kuyafikia mabasi yote nchini.
Kwa mujibu wa Kamwelwe, Tanzania ina mabasi 49,000 ambapo kati ya hayo 7,000 ni mabasi yanayofanya safari zake mikoani na yanayobaki ambayo ni sawa na asilimia 85.7 ni daladala zinazofanya safari zake ndani ya miji.