Serikali inavyoangazia daladala, mabasi ya mikoani kuongeza mapato kielektroniki

December 24, 2018 7:41 pm · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link

Tanzania ikianza kutumia mfumo wa utoaji wa tiketi za kielektroniki itaungana na nchi ya Rwanda ambayo inatumia mfumo huo kwenye mabasi ya umma ambapo mashine za tiketi zimewekwa kwenye mabasi. Picha| newtimes.co.rw


  • Waziri wa Uchukuzi, Mhandisi Isack Kamwelwe amesema mfumo uliopo sasa ni wa “kienyeji” unaikosesha Serikali mapato yatokanayo na huduma za usafiri. 
  • Wizara yake inaendelea kufanya mazungumzo na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ili kupata namna nzuri itakayosaidia kupatikana kwa mapato hayo.
  • Baadhi wananchi wamesema ni mfumo mzuri lakini unaweza kusababisha mtikisiko wa ajira kwa baadhi ya watu.

Dar es Salaam. Serikali inaendelea kutafuta namna mbalimbali zitakazosaidia kukusanya mapato kwa wingi na safari hii Serikali imesema kuanzia Januari 2019 mabasi yote yanatakiwa kutumia mfumo wa utoaji wa tiketi za kielektroniki kwa abiria ili kurahisisha upatikanaji wa kodi. 

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe amesema maabasi hayo yanajumuisha daladala zinazofanya safari katikati ya miji na yale yanafanya safari zake kutoka mkoa mmoja hadi mwingine. 

Katika hotuba yake ya Desemba 20, 2018 wakati wa uzinduzi wa ujenzi wa daraja la kisasa la Salender litakalopita juu ya Bahari  ya Hindi na kupunguza adha ya foleni jijini Dar es salaam, Kamwelwe alisema mfumo uliopo sasa wa ukataji tiketi za mabasi ni wa “kienyeji”, jambo linaloikosesha Serikali mapato yatokanayo na vyombo vya usafiri. 

Mpango huo mpya wa Kamwelwe ni wa tatu kutangazwa na Serikali ndani ya mwezi mmoja baada ya Rais John Magufuli kugawa vitambulisho kwa wakuu wa mikoa hivi karibuni kwa ajili ya wafanyabiashara wadogowadogo ili wachangie mapato na tangazo la Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) la kuwataka wafanyabiashara mtandaoni kujisajili na kulipa kodi. 

“Tumekubaliana, tumeshaongea na Katibu Mkuu wa Hazina kwamba ikifika Januari, Mhe Rais mabasi yote tiketi zote ziwe ni elektroniki na kwa kufanya hivyo Mheshimiwa Rais tutakusanya kodi kwa urahisi bila ubabe,” amesema Kamwelwe.

Amesema ili kukamilisha agizo hilo wizara yake inaendelea kufanya mazungumzo na TRA ili kupata namna nzuri itakayosaidia kupatikana kwa mapato hayo ambayo yamekuwa yakipotea kwa muda mrefu. 

“Wizara yangu inaendelea kuongea na kamishna wa ‘domestic revenue’ (mapato ya ndani) tunapataje mapato hapa, ukataji wa tiketi bado uko kienyeji,” amesema.  


Zinazohusiana: 


Kwa mujibu wa Kamwelwe Tanzania ina mabasi 49,000 ambapo kati ya hayo 7,000 ni mabasi yanayofanya safari zake mikoani na yanayobaki ambayo ni sawa na asilimia 85.7 ni daladala zinazofanya safari zake ndani ya miji. 

Katika daladala zote zilizopo nchini, 9,000 zinapatikana mkoa wa Dar es Salaam, ambapo zikiwekewa mikakati mizuri zinaweza kuwa sehemu ya kukuza mapato ya Serikali. Kwa takwimu alizotoa Kamwelwe hivi karibuni, kwa kila daladala tano zilizopo Tanzania, moja ipo mkoa wa Dar es Salaam.

Mwaka 2017 sekta ya uchukuzi ilikuwa ni moja zilizofanya vyema baada ya kuchangia asilimia 16.5 ya Pato la Taifa (GDP) ikiwa nyuma kidogo ya sekta ya utalii ambayo ilichangia asilimia 17.2. 

Matumizi ya tiketi za kielektroniki kwa mabasi huenda ni utekelezaji wa maagizo ya Rais Magufuli aliyoyatoa Desemba 10, 2018 ambapo aliwataka watendaji wa Serikali kutumia vizuri fursa ya vyanzo vya mapato vilivyopo nchini katika kukusanya kodi ikiwemo sekta ya uvuvi katika bahari kuu, madini na uchimbaji wa gesi asilia.

Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) inaendelea na majaribio ya mfumo wa tiketi za kielektroniki kwa mabasi ya daladala kabla ya kuhamishia kwa mabasi yanayoenda mkoani. 

Afisa Mwandamizi wa Mawasiliano wa Sumatra, Salum Pazzy ameiambia nukta.co.tz kuwa wanaendelea kuweka sawa baadhi ya mambo kwa kushirikiana na TRA ili mfumo huo uanze kufanya kazi kwa wakati kama alivyoeleza Kamwelwe.

Kupitia mfumo huo, mamlaka hizo mbili zitaweza kupanga nauli na kodi zinazoendana na mapato ya wamiliki wa mabasi ikizingatiwa kuwa mfumo huo utawawezesha kuwa na takwimu za mapato yanayoingia.

Pia utasaidia kuondoa mkanganyiko wa majukumu ya kazi kati ya wamiliki wa mabasi na madereva na kila mmoja ataweza kusimama katika nafasi yake, kuliko hivi sasa ambapo madereva hasa wa daladala wanaonekana kuchukua nafasi ya wamiliki. 

Hali hiyo inatokana na dhana kuwa wao ndiyo wanajua mwenendo wa biashara na mapato, jambo linalowakosesha wamiliki mapato na kushindwa kulipa kodi inavyotakiwa.

Baadhi ya madereva na makondakta jijini Dar es Salaam wamesema ni mfumo mzuri lakini umakini unahitajika ikizingatiwa kuwa daladala ni nyingi na zinatofautiana nauli kutoka eneo moja hadi nyingine. 

“Hatujui itakuwaje tunasubiri watakavyopanga wao kama tiketi zitakuwa zinakatwa kwenye vituo au kwenye gari kama ilivyo sasa,” amesema John Nzela, dereva wa daladala ya Makumbusho-Tegeta.

Kuanza kutumika kwa mfumo huo kunaweza kuwasaidia abiria wa mikoani kuokoa muda na kuepuka usumbufu wa kwenda katika vituo vya mabasi na kuwatumia mawakala kukata tiketi. 

Mkazi wa Kibaoni mkoa wa Singida, Raheli Essau ameiambia Nukta kuwa ni mfumo mzuri lakini huenda usilete matokeo yaliyokusudiwa kutokana na mazingira ya usafiri ya Tanzania ikizingatiwa kuwa watu wengi bado wamekumbatia mifumo ya zamani ya biashara. 

Amebainisha kuwa mfumo huo pia utaleta mtikisiko kidogo hasa kwa watu wanaohusika na utengenezaji, ukataji wa tiketi za mabasi wakiwemo wamiliki wa maduka ya uchapishaji, mawakala na wapiga debe ambao wamekuwa wakitegemea shughuli hiyo kuendesha maisha yao. 

“Inaweza kuwa na athari kwa namna moja au nyngine baadhi ya watu watapoteza ajira maana kuna stationary zimeajiri watu kutengeneza hizo tiketi,” amesema Raheli. 

Enable Notifications OK No thanks