Shida juu ya shida: Uhaba wa maji unavyokwamisha vita ya Uviko-19 Singida

October 25, 2021 11:32 am · Charles
Share
Tweet
Copy Link
  • Wanakijiji cha Misake wafauta maji ya dimbwi kilomita nne.
  • kukosekana maji kwawazuia kunawa mikono mara kwa mara.
  • Serikali yaahidi kutatua changamoto hiyo huku akiwataka kupata chanjo ya Uviko-19.

Singida. Katika moja ya madimbwi ya maji pembezoni mwa barabara ya Kijiji cha Misake, Wilaya ya Ikungi mkoani Singida lipo kundi kubwa la wanawake na wasichana linawania maji.

Pamoja ya kuwa ni alfajiri, idadi ya wanaokuja kufuata maji katika dimbwi hili inaongezeka kila dakika huku wengine wakija na tela zanazovyutwa na ngombe na kusubiri katika foleni.

Haya ndiyo maisha ya kila siku kwa wakazi wa eneo hili jambo linalosababisha kukosa maji ya uhakika hivyo kuathiri jitihada ya kujikinga na ugonjwa wa virusi vya Corona (Uviko-19).

Kwa mujibu wa wataalamu wa afya njia kubwa ya kupunguza maambukizi ya virusi vya Corona ni pamoja na kusafisha mikono mara kwa mara kwa maji safi.

Uhaba wa maji safi na salama unawafanya watu wanaoikosa huduma hiyo muhimu kwa maisha ya binadamu kuwa hatarini kupata magonjwa ya tumbo pamoja na Uviko-19. 

Ripoti ya Shirika la umoja wa mataifa linaloratibu upatikanajii wa maji (UN Water Development Report) watu bilioni 4.2 ama asilimia 55  ya watu duniani hawana vifaa vya kawaida vya kunawia mikono majumbani kutokana na uhaba wa maji safi na salama. Hali inawakumba zaidi watu waishio katika maeneo ya vijijini.

Nchini Tanzania,  kwa mujibu wa Ripoti ya Wizara ya Maji ya mwaka 2019/2020  jumla ya miradi ya maji 1,659 yenye vituo vya kuchotea maji 131,370 imejengwa. Kati ya vituo vilivyojengwa, vituo 86,780 vinafanya kazi na vina uwezo wa kuhudumia wananchi wapatao milioni 25.4 sawa na asilimia 64.8 au takriban theluthi mbili ya watu waishio vijijini.

Katika maeneo ya mijini upatikanaji wa huduma ya maji katika miji mikuu ya mikoa ni asilimia 80 na kwa miji mikuu ya wilaya, miji midogo na miradi ya kitaifa upatikanaji wa huduma hiyo ni asilimia 64.

Hepiphania Romadi akichotaja maji katika dimbwi lililopo kilomita nne kutoka nyumbani kwake. Picha| Charles Kombe.

Wakazi wa kijiji hiki wanasema uhaba wa maji umesababisha kuingia gharama kubwa kupata huduma hiyo, kiasi cha kufanya unawaji mikono mara kwa mara kuwa kama anasa licha ya kuwa inashauriwa na wataalamu wa afya. 

Mzaliwa katika kijiji hicho, Hepiphania Romadi, licha ya kuwa na mtoto mchanga anasema amekuwa akilazimika kuamka saa 10 alfajiri kwenda kufuata maji.

 “Huwa tunaamka asubuhi sana… pengine unakuta una mtoto kama mnavyoona hapa mtoto wangu bado ana miezi miwili na wiki tatu lakini inatubidi kuamka hivyo hivyo kufuata maji,” anasema Hepiphania akiwa amebeba mtoto pembeni ya bwawa dogo la maji. 

Hepiphania anasema maji anayoyapata wakati mwingine huwa ni ndoo ya lita 20 ambayo huwa na matumizi makubwa jambo linalowafanya kwenye kaya yao kuahirisha kunawa mikono kutunza kidogo walichofanikiwa kupata kwa siku hiyo. 

Licha ya kufuata maji katika umbali wa zaidi ya kilomita nne lakini bado imekuwa ni hatari kutokana na uwepo wa wanyama hatari pamoja na changamoto nyingine wakati wa kutafuta maji hayo.

“Ukitoka usiku unakutana na fisi mara watu usiowajua yaani inakua shida kweli na huwezi ruhusu watu wachezee maji eti kisa cha huu ugonjwa wa corona,” anasema Kija Makida, mkazi wa Kijiji cha Kikhomango aliyefuata maji katika eneo hilo.

Kijiji cha Makida kipo umbali wa kilometa nne kutoka katika bwawa hilo.

Uongozi wa kijiji cha Miseki unakiri uwepo cha changamoto ya maji na kuwa licha ya jitihada za kutoa elimu bado suala la unawaji mikono limeendelea kuwa changamoto. 

“Suala la kunawa ndilo linalowasumbua watu kwenye kijiji chetu. Tumewaambia vijana waendelee kushirikiana kuchimba visima vifupi lakini pamoja na kuwa maji yanapatikana kwa shida, wananchi waendelee kujitahidi kunawa mikono ili kujikinga na ugonjwa huu wa Corona,” anasema Salimu Sungi, Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Misake. 

Hata hivyo, licha ya uhaba wa maji katika maeneo hayo bado wapo wanakijiji wanaojitahidi kutumia kiasi hicho kidogo cha maji walichokipata kuhakikisha wananawa mikono akiwemo Mwanaidi Suleimani.

“Wengine hawawezi kabisa kutumia maji kwa sababu yako mbali lakini mimi nimejitahidi hivyo hivyo ninachokipata na nawa mikono kwa sabuni. Maana hakuna namna tunaelezwa huu ugonjwa ni hatari,” anasema Mwanaidi.

Pamoja na hali hiyo, wahudumu wa afya wameendelea kutoa elimu ya afya ya kujikinga na Uviko-19 licha ya mwitikio kuwa mdogo. 

Paul Samuel, Mhudumu wa afya katika Zahanati ya Minyughe mkoani hapa anasema huwa wanawapatia elimu ya Uviko-19 wateja wao kila asubuhi wanapofika kupata matibabu juu ya umuhimu wa kujikinga maradhi hayo pamoja na kupata chanjo mapema. 


Upatikanaji wa maji ni suluhu pekee

Ili kuweza kukabiliana ipasavyo na Uviko-19, Samuel anasema Serikali yapaswa kutatua tatizo la uhaba wa maji katika eneo hilo kwa upekee wake ili kuondoa changamoto mbalimbali zinazotokana na ukosefu wa maji ikiwemo kutokufuata taratibu za kujikinga na Uviko-19.

Uongozi wa Wilaya ya Ikungi unaeleza kuwa wametengeneza mfumo endelevu wa kutatua changamoto ya maji ambao ni Wakala wa Maji na Usafi Vijijini (Ruwasa) na kwamba kuna miradi iliyobuniwa kutokomeza adha hiyo. 

Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Jerry Murro ameiambia Nukta Habari (www.nukta.co.tz) kuwa Serikali imejiridhisha kuwa miradi ya maji iliyoibuliwa ni endelevu ili kuhakikisha wakazi hao wanapata huduma ya maji safi na salama. 

Murro anasema wameendelea kutoa elimu juu ya Uviko-19 kwa kushirikiana na wadau wakubwa wa wilaya ikiwemo madiwani, wenyeviti wa vijiji pamoja na viongozi wa dini.

“Wilaya hii ni kubwa sana, kwa mfano kutoka hapa hadi Iyumbu ni kilomita zaidi ya 360…sio kitu unachoweza kifanya muda mfupi. Kikubwa tumewafikia na wanajua Corona ni nini, namna ya kujikinga na chanjo imekuja na wanatakiwa kuchanja,” anasema Murro. 

Ukosefu wa maji katika kjiji cha Misake umesababisha wakazi wake kushindwa kujikinga na Uviko-19 kwa kunawa mikono kwa maji tiririka kwa sababu rasilimali hiyo haipatikani kwa urahisi. Picha| Charles Kombe.

Wadau wa afya wanasema kuwa licha ya kuwa ugonjwa siyo jambo zuri lakini ujio wa  Uviko-19 umerejesha mwamko wa watu kunawa mikono hivyo Serikali iendelee kuboresha upatikanaji wa huduma za maji safi na salama kufanikisha jambo hilo. 

“Ugonjwa wa Corona umeongeza mwamko wa kunawa mikono jambo ambalo ni zuri kwa kweli ingawa bado siyo wote wanaoweza kufanya hivyo kutokana na mazoea lakini tumeendelea kuwaasa wananchi juu ya umuhimu wa kunawa mikono maana si kwamba wanajikinga na corona tu, hata magonjwa mengine yanayosababishwa na bakteria,” Dk Abdul Mkeyenge, mtaalamu wa afya. 

Dk Mkeyenge anaeleza kuwa ni vyema wadau wa afya, taasisi binafsi pamoja na mashirika mbalimbali kushirikiana na Serikali ili kuendelea kutoa elimu kuhusu kunawa mikono na umuhimu wake katika kuepusha magonjwa mbalimbali.


Watumia wazee wa kimila, kijadi kufikisha elimu

Katika kuongeza hamasa, Murro anasema zaidi ya robo tatu au asilimia 75.4 ya wakazi wa wilaya yake wanafahamu kuhusu ugonjwa wa virusi vya Corona licha ya kuwa wapo baadhi ambao wanahitaji kuelimishwa kwa lugha yao ambapo Serikali imeendelea kuwapa elimu kupitia wazee wa kimila na jadi pamoja na wadau wengine.

Kuhusu mwitikio wa chanjo katika wilaya hiyo, Murro anasema baada ya elimu kutolewa wamehakikisha wananchi wanatoka majumbani na kwenda kuchanja ili kujikinga na ugonjwa wa Corona licha ya kuwa bado mwamko hauridhishi kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo woga na uzushi kutoka mitandao ya kijamii.

Mkuu wa wilaya pia ameendelea kuwataka wananchi wa maeneo yote kujitokeza kuchanja chanjo ya Corona pamoja na kuendelea kufuata taratibu zote za kujikinga na ugonjwa huo.

Makala hii imefadhiliwa na Shirika la maendeleo ya habari la International Media Support (IMS) na Umoja wa Ulaya (EU).

Masoko & Zaidi
Loading…
No recent matches
No upcoming matches
/
No matches found for this filter
13 Jun, 2026 · TZS
No forex gainers today
No forex losers today
Forex rates unavailable
13 Jun, 2026 · TZS
No gainers today
No losers today
13 Jun, 2026
No active movers today

Inaendeshwa na Nukta AI

Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
🔴LIVE: HII HAPA BAJETI KUU YA SERIKALI 2026/2027

🔴LIVE: HII HAPA BAJETI KUU YA SERIKALI 2026/2027

Nukta TV

Mashine za kukaushia rangi za kucha kutozwa ushuru kwa asilimia 10

Mashine za kukaushia rangi za kucha kutozwa ushuru kwa asilimia 10

Nukta TV

Wazee wa 'kubet' hii inawahusu, 5% kutozwa kwenye dau la kamari

Wazee wa 'kubet' hii inawahusu, 5% kutozwa kwenye dau la kamari

Nukta TV