Serikali yaingilia kati vitambulisho vya NIDA, usajili laini za simu
- Yaonesha kutoridhika na kasi na ya usajili, Waziri Mkuu atoa maagizo kwa NIDA.
- NIDA yatakiwa kuwapa wananchi angalau namba za utambulisho wa usajili wao kabla ya muda wa usajili wa laini za simu haujamalizika.
Dar es Salaam. Serikali imeiagiza Mamlaka ya Usajili wa Vitambulisho vya Taifa (NIDA) kuhakikisha inawapatia wananchi hasa waliopo vijijini angalau namba za utambulisho wa usajili wao kabla ya muda wa usajili wa laini za simu kwa alama za vidole haujamalizika.
Waziri Mkuu, Kassimu Majaliwa amesema utoaji wa namba za utambulisho wa raia wananchi ambao hawajapata vitambulisho vya uraia utawawezesha kuingia kwenye orodha ya wale wanaosubiri kusajiliwa hata kama muda wa usajili utakuwa umeisha.
Mwisho wa usajili wa laini za simu kwa alama za vidole na vitambulisho vya Taifa ni Desemba mwaka huu. Hadi sasa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imesema kuwa haitaongeza muda wa kusajili laini za simu kwa alama za vidole baada ya Desemba kupita.
Majaliwa amelitoa agizo hilo jana (Septemba 21, 2019) wakati akizungumza na wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa hospitali ya wilaya ya Geita iliyopo kwenye Kijiji cha Nzela mkoani Geita.
Taarifa ya Ofisi ya Waziri Mkuu inaeleza kuwa Serikali imewapatia NIDA vifaa vya kisasa vya kielektroniki ili wafanye kazi zao kwa haraka na ufanisi, lakini hali hairidhishi kwa sababu wananchi wengi bado hawajapata vitambulisho na kasi ya usajili wa laini za simu inalalamikiwa katika meneo mengi.
“NIDA mnalalamikiwa, nimeenda Morogoro Vijijini NIDA mnalalamikiwa hivi utendaji wenu uko je? Kwanini mnachelewa?” amehoji Majaliwa huku Afisa Msajili wa NIDA wa Wilaya ya Geita, Paschal Saro ambaye alijitetea kwamba wamesajili laini za simu 340 na tayari namba za usajili 330 zimeshatolewa.
Soma zaidi:
- Simu za mkononi sasa kupima ugonjwa wa kifua kikuu
- Apple yaingiza sokoni simu mpya zinazotumia mfumo wa ‘eSIM’
- Mhandisi Nditiye atoa ufafanuzi usajili wa laini za simu kwa kutumia alama za vidole
Saro alimwambia Waziri Mkuu kuwa suala la utata wa uraia kwa baadhi ya wanananchi wanaoomba vitambulisho vya NIDA ni moja ya sababu zinazochelewesha usajili wa vitambulisho vya uraia.
Aidha, Waziri Mkuu aliwasihi wananchi wote kuwa walinzi wa nchi yao kwa kutoa taarifa za watu ambao wanaomba vitambulisho vya uraia wa Tanzania wakati si raia na aliwataka watoe taarifa mara moja kwenye vyombo vya dola pale wanapogundua kuwa kuna raia wa nje wanafanya mchakato wa kupata vitambulisho hivyo.
Latest