Rais Samia ateua Mkurugenzi mpya NIDA miezi mitano baada ya nafasi hiyo kuwa wazi

December 18, 2024 6:41 pm · Fatuma Hussein
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni James Wilbert Kaji ambaye alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Moshi, mkoani Kilimanjaro.
  • Uteuzi huo unafanyika baada ya nafasi hiyo kuwa wazi kwa miezi mitano.

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amemteua James Wilbert Kaji kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) miezi mitano baada ya nafasi hiyo kuwa wazi.

Taarifa ya Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Dk Moses Kusiluka iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu leo Disemba 18, 2024 imethibitisha uteuzi wa kiongozi huyo ambaye alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Moshi, mkoani Kilimanjaro.

Awali mamlaka hiyo iliongozwa na Ismail Rumatila aliyeitumikia nafasi hiyo kabla ya kuteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Afya Agosti 14 mwaka huu.

Huenda uteuzi wa kiongozi huo ukaimarisha utendaji kazi wa mamlaka hiyo inayolalamikiwa na wananchi hususani katika suala la utoaji wa vitambulisho tangu kuanzishwa kwake.

Kusuasua zoezi hilo kumemfanya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Innocent Bashungwa, kuagiza  vitambulisho milioni 1.2 ambavyo tayari vimetengenezwa vitolewe na kusambazwa kwa wananchi ndani ya miezi miwili.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Disemba 17, 2024, katika ziara ya kikazi, Bashungwa aliitaka NIDA kuwajibika na kuhakikisha vitambulisho hivyo vinawafikia walengwa haraka.


“Ni jukumu lenu kuhakikisha kadi hizi mnazifuatilia na zinawafikia walengwa ndani ya miezi miwili. Nitakapokuja tena, nataka taarifa kwamba vitambulisho vilivyotengenezwa vimewafikia walengwa,” alisema Bashungwa.

Aidha, Waziri Bashungwa aliiagiza NIDA kuhakikisha Watanzania ambao vitambulisho vyao vilifutika maandishi wanapatiwa vitambulisho vipya bila gharama yoyote wala usumbufu.

Mfano wa kitambulisho cha NIDA ambacho kila raia wa Tanzania anapaswa kuwa nacho. Picha/ nida.go.tz.

Pia alisisitiza kuboresha huduma kwa wananchi kwa kuondoa urasimu na kuwachukulia hatua watumishi wazembe wanaoshindwa kuwahudumia wananchi ipasavyo.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Uzalishaji wa Vitambulisho NIDA, Edson Guyai, alisema changamoto kubwa ni vitambulisho vya wanafunzi na watu waliohama makazi.

Hata hivyo, alibainisha kuwa NIDA inashirikiana na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kufuatilia walengwa na kuwatumia ujumbe kuhusu maeneo wanayoweza kuchukua vitambulisho vyao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks