Serikali ya Zanzibar yazuia mapumziko Novemba 27 kwa watumishi wa umma
- Yasema watumishi wa umma waendelee na kazi kama kawaida.
Dar es Salaam: Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema hakutakuwa na mapumziko siku ya jumatano Novemba 27 mwaka huu kama inavyofanyika kwa wakazi wa Tanzania bara ambao pia wanatarajia kuitumia siku hiyo kwa ajili ya kupiga kura.
Taarifa ya Msemaji Mkuu wa Serikali hiyo Charles Hilary iliyotolewa leo Novemba 25,2024 inafafanua kuwa watumishi wa umma wa Zanzibar wanatakiwa kuendelea na majukukumu yao kama kawaida.
“Kwa vile Zanzibar hakuna uchaguzi huo wa Serikali za Mitaa, Serikali Ya Mapinduzi Ya Zanzibar inawaarifu wananchi wote Jumatano Novemba 27 2024 ni siku ya kazi kama kawaida Zanzibar, ahsateni” amesema Hilary.
Taarifa ya Hilary inakuja ikiwa ni masaa machache Tangu Rais Samia aitangaze rasmi siku ya Jumatano ya Novemba 27 mwaka huu kuwa ni mapumziko kwa wafanyakazi wa umma wa Tanzania bara ili kutoa nafasi ya kushiriki katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
Kwa mujibu wa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa uchaguzi huo utafanyika kuanzia saa tatu asubuhi hadi saa 10 jioni na kutoa nafasi kwa wananchi waliojiandikisha kuwachagua viongozi wawatakao.
Zoezi hili linaloratibiwa na wizara hiyo ni miongoni mwa matukio muhimu nchini yatakayoliwezesha Taifa kuwa na viongozi watakaosimamia maendeleo katika mitaa, vijiji na vitongoji kwa miaka mitano ijayo.