Sababu za Australia kupiga marufuku mitandao ya kijamii kwa watoto chini ya miaka 16
- Imelenga kuwalinda watoto dhidi ya madhara hasi ya mtandao kama uonevu, maudhui hatari na unyanyasaji
- Zuio kuanza rasmi mwakani baada ya sheria kupitishwa.
Dar es Salaam. Serikali ya Australia imependekeza kupiga marufuku matumizi ya mitandao ya kijamii kwa watoto walio chini ya umri wa miaka16 hatua inayokusudiwa kuwalinda dhidi ya athari mbaya za kidijitali na kuwaepusha na madhara ya muda mrefu yanayoweza kuzuiwa mapema.
Mitandao itakayohusishwa na sheria ya marufuku hii ni Instagram na Facebook inayomilikiwa na kampuni ya Meta, TikTok ya Bytedance mtandao wa SnapChat pamoja na X unaomilikiwa na tajiri namba moja duniani Elon Musk.
Sheria hiyo ya katazo italazimisha majukwaa ya mitandao ya kijamii kuthibitisha umri wa watumiaji na kuwazuia wale walio chini ya miaka 16.
Ili kuepukana na udanganyifu wa umri sheria hiyo imependekeza matumizi ya mifumo ya kibiometriki au kwa kutumia taarifa zilizosajiliwa na mamlaka za Serikali kuthibitisha umri wa mhusika.
Aidha, majukwaa ya mitandao ya kijamii yatakayoshindwa kuhakiki kwa ufasaha umri sahihi wa watoto wanaotumia huduma zao nchini humo yatapigwa faini ya takriban Sh85 bilioni.
Kwa mujibu wa Michelle Rowland, Waziri wa Mawasiliano Australia takribani theluthi mbili ya watoto wa wanaoishi nchini humo wenye umri wa miaka 14 hadi 17 wamewahi kuona maudhui yenye madhara makubwa mtandaoni, ikiwemo matumizi ya dawa za kulevya, kujiua, au kujidhuru.
Ulinzi wa watoto ni sababu
Licha ya mitandao ya kijamii kuwa sehemu muhimu ya maisha ambapo hutumika kama kupashana habari, kuwasiliana, kuuza na kununua bidhaa hutumika pia kama chanzo cha changamoto za kiusalama na kisaikolojia kupitia vitendo vya uonevu mtandaoni, ambapo watoto wanaweza kutukanwa, kudhalilishwa, au hata kutishiwa.
Hatua hiyo inaweza kuwasababishia watoto matatizo ya afya ya akili kama vile wasiwasi, unyonge, pamoja na msongo wa mawazo.
Maudhui mengine yasiyo salama mtandaoni kwa watoto ni pamoja na maudhui yanayohamasisha matumizi ya dawa za kulevya, vurugu, au mitazamo isiyofaa kuhusu mwili (body image), hali inayoweza kuathiri mtazamo wa watoto kuhusu maisha yao na dunia kwa ujumla.
Kuchochea maendeleo chanya
Matumizi ya kupita kiasi ya mitandao ya kijamii yanahusishwa na athari mbaya kwenye ukuaji wa watoto, hasa katika hatua muhimu za awali za ukuaji wao ikiwemo kushiriki michezo inayoweza kuwasaidia kuimarisha afya, pamoja na ukaribu na wazazi au walezi wao.
Utafiti wa athari za matumizi ya vifaa vya mawasiliano ya kielektroniki kwa watoto uliochapishwa na ‘National Center for Biotechnology I nformation’ unaonesha matumizi ya muda mrefu ya vifaa vya mawasiliano kama kompyuta na simu yanaweza kuathiri ukuaji wa maeneo ya ubongo yanayohusika na maamuzi, kumbukumbu, na utambuzi wa kihisia, kupunguza muda wa matumizi ya vifaa hivyo kwa watoto kunawapa nafasi ya kushiriki katika shughuli za kujifunza na kucheza zinazokuza uwezo wa akili.
Utafiti huo umebeinisha kuwa watoto wanaotumia muda mwingi kwenye mitandao ya kijamii, hasa usiku, hupata changamoto za kulala, hali inayosababisha uchovu, kupungua kwa umakini darasani na afya mbovu ya mwili kwa ujumla.
Aidha, matumizi ya mitandao ya kijamii yasiyofaa yanaweza kuathiri ufaulu wa masomo kwasababu muda ambao ungepaswa kutumiwa kujifunza unatumika kwenye maudhui yasiyo na tija, hali hii inaweza kuathiri mafanikio ya kielimu kwa wanafunzi.
Kushughulikia changamoto za faragha mtandaoni
Watoto wengi hawana uelewa wa kina kuhusu jinsi data zao zinavyokusanywa na kutumika na kampuni za teknolojia.
Majukwaa mengi ya mitandao ya kijamii hukusanya taarifa binafsi za watumiaji kama vile eneo, tabia za matumizi, na mapendeleo. Data hizi mara nyingi hutumiwa kwa faida ya kibiashara, ikiwa ni pamoja na matangazo yaliyoelekezwa (targeted ads).
Kupunguza au kuzuia watoto kutumia mitandao ya kijamii kutasaidia kulinda faragha yao na kupunguza hatari ya unyonyaji wa kibiashara. Hii pia inalenga kuwahamasisha wazazi kuhusu umuhimu wa kulinda taarifa za watoto wao.
Kurahisisha malezi kwa wazazi
Zuio hili pia linalenga kuwawezesha wazazi na walezi kusimamia vyema maisha ya kidijitali ya watoto wao kwani wanapokuwa na matumizi madogo wa mitandao ya kijamii, wazazi wanapata nafasi nzuri zaidi ya kuelekeza watoto wao kushiriki shughuli zenye manufaa zaidi kama michezo, kusoma, na mazungumzo ya kifamilia.
Pia litasaidia wazazi kuimarisha mazungumzo ya ana kwa ana na watoto wao, hali ambayo ni muhimu katika kujenga maadili na tabia bora.Hata Hivyo sio mitandao yote itaguswa na zuio hilo, watoto wataendelea kuwa na uwezo wa kufikia huduma za ujumbe, michezo ya mtandaoni na huduma zinazohusiana na afya na elimu, kama vile jukwaa la msaada wa afya ya akili kwa vijana, ‘Headspace’, pamoja na ‘Google Classroom’ na ‘YouTube’ za kampuni ya Alphabet.