Serikali kufanya mabadiliko ya sera, sheria kukuza usawa wa kijinsia
- Rais Samia asema mabadiliko hayo yatachochea ustawi wanawake na wanaume.
- Ahimiza uwepo wa kizazi chenye usawa.
Arusha. Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amesema Serikali itaendelea kufanya mabadiliko ya sera na sheria ili kuleta mabadiliko mbalimbali kwenye jamii katika kuimarisha haki na usawa kijinsia
Rais Samia aliyekuwa alizungumza katika kilele cha maadhimisho ya siku ya wanawake duniani yaliyofanyika kitaifa jijini Arusha leo Machi 8, 2025 amesema kuwa mabadiliko hayo yawezesha wanawake na wanaume kuwa na haki sawa katika masuala mbalimbali ikiwemo umiliki wa ardhi.
“Natamani kuona mabadiliko ya sera na sheria mbalimbali ambayo tunayafanya yawe yameleta mabadiliko zaidi kwa jamii mfano suala la umiliki wa ardhi lipewe uzito wake,” amesema Rais Samia.
Mwaka huu maadhimisho ya siku ya wanawake duniani yanafanyika ikiwa ni miaka 30 tangu kutolewa kwa tamko la Beijing liloweka misingi ya utekelezaji wa haki kwa wanawake na miaka 10 ya uwepo wa malengo ya maendeleo endelevu (SGD’s) yaliyoanzishwa na Umoja wa Mataifa (UN).
Rais Samia ametumia jukwaa hilo kueleza mafanikio 13 ambayo ni sehemu ya malengo endelevu 16 yaliyofanikiwa kutekelezwa nchini Tanzania ikiwemo kupunguza umaskini.
“Lengo la kwanza ni kupunguza umaskini, kwa upande wetu Tanzania mpaka tunafanya tathmini ya mpango wa tatu wa maendeleo tayari tulishapunguza umaskini kwa asilimia 26 kutoka kiwango kilichokuwa wakati tunaanza utekelezaji…sasa hivi hatushuki kwenye asilimia 30,” amesema Rais Samia.

Baadhi ya matukio yaliyofanyika katika kilele cha maadhimisho ya siku ya wanawake duniani ambayo kitaifa yamefanyika katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid Jijini Arusha.Picha|Ikulu.
Mbali na jitihada za kufikia lengo hilo, Rais Samia amesema Tanzania imefanikiwa kuondoa njaa kwa asilimia 100 na kujitegemea kwa chakula kwa asilimia 128 huku katika sekta ya afya Serikali ikifanikiwa kujenga miundombinu, kuongeza vifaa tiba na kupunguza idadi ya vifo vya mama na mtoto kutoka 1,500 kwa vizazi hai 100,000 hadi vifo 104 kwa vizazi hai 100,000.
Katika suala la elimu Rais Samia amesema idadi ya wanafunzi nchini inazidi kuongezeka huku kukiwa na uwiano sawa kati ya wasichana na wavualana suala alilolitaja kuongeza ushindani katika soko la ajira.
“Zile kazi zilizokuwa siyo za wanawake sasa zinaenda kuwa za wanawake…Katika ngazi ya vyuo vikuu mwaka 2024 kulikuwa na wanafunzi 334,854 wanawake wakiwa asilimia 44.95 tunakwenda kwenye 50/50 na huku ndipo kulikuwa kugumu kwa watoto wa kike kutoboa,” amesema Rais Samia.
Sekta ya maji nayo imezidi kupiga hatua ambapo mpaka kufikia Disemba, 2024 huduma ya maji imewafikia wakazi wa vijijini kwa asilimia 80 na mijini asilimia 90 huku miradi zaidi ya 1,000 ikiwa katika hatua za utekelezaji.
Kuhusu nishati Rais Samia amesema tayari vijijini 12,300 huku miradi mbalimbali ya umeme ikiendelea kutekelezwa ikiwemo Mradi wa Kuzalisha Umeme kwa Kutumia Maji (JNHPP) unaotarajiwa kuongeza uzalishaji wa umeme.
Pia Serikali imeendelea kuchochea ubunifu kwa vijana kwa kujenga miundombinu inayowawezesha vijana kubuni miradi mbalimbali, kupunguza kutokuwa sawa baina ya wanawake na wanaume, kuongeza usalama na utulivu pamoja na kufanya kazi kwa pamoja.
Latest



