IGP Wambura: Polisi 27 waliofukuzwa mafunzo kwa utovu wa nidhamu wafuatiliwe

March 7, 2025 4:26 pm · Kelvin Makwinya
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni kati ya wanafunzi 27 waliosimamishwa mafunzo ya uongozi mdogo yaliyohitimishwa katika Shule ya Polisi Tanzania-Moshi.

Dar es salaam. Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP)Camillus Wambura amemuagiza Kamishna wa Utawala wa jeshi hilo kufuatilia mienendo ya askari 27 waliofukuzwa mafunzo ya uongozi mdogo kwa makosa ya utovu wa nidhamu na kushindwa kuhimili mafunzo.

IGP Wambura aliyekuwa akizungumza mara baada ya kuhitimisha mafunzo hayo yaliyotolewa kwa askari polisi ngazi ya Sajini na Koplo amesema askari hao wanapaswa kufuatiliwa katika maeneo wanayofanya kazi na wanayoishi.

Kamishna utawala, wale wanafunzi waliokuja kusoma hapa, na wakashindwa kufika tarehe ya leo kwa sababu ya utovu wa nidhamu muwafuatilie kule wanakofanya kazi, kwa sababu kama unakuwa mtovu wa nidhamu kwenye chuo ambapo kuna eneo dogo na udhibiti mkubwa kule walipo na uhuru nina wasiwasi mkubwa,” amesema IGP Wambura.

Wambura amesisitiza kuwa ili askari polisi aweze kutimiza majukumu yake ipasavyo anapaswa kuwa na nidhamu huku akizingatia haki, weledi pamoja na uadilifu.

Kauli ya IGP Wambura inakuja wakati ambao kumekuwepo na malalamiko ya wananchi juu ya matukio ya ukiukwaji wa nidhamu kwa maafisa wa polisi ikiwemo kutoa lugha za matusi pamoja na kuomba rushwa.

Januari 15 mwaka huu Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro aliwaambia wanahabari kuwa jeshi hilo limewakamata na linawachukulia hatua askari wa usalama barabarani walionekana wakipokea rushwa katika video zilizosambaa kwenye kurasa mbalimbali za mitandao ya kijamii.

Komandanti wa Shule ya Polisi Tanzania, Ramadhani Mungi aliyekuwa akitoa taarifa ya mafunzo ameeleza kuwa kati wa wanafunzi 2,143 walioripoti Disemba 6, 2025 wanafunzi 27 walisimamishwa masomo kutokana na utovu wa nidhamu pamoja na uwezo mdogo katika kumudu mafunzo.

Mungi ameeleza kuwa mafunzo hayo yaliyo funguliwa rasmi Disemba 10, 2024 yalijumuisha wanawake 632 na wanaume 2143. Kati yao wanafunzi wa mafunzo ya Sajenti walikuwa 1837 waliofanya mafunzo yao kwenye kambi ya Kaba Pori na wale wa mafunzo ya Kopro 938 katika kambi ya Kilele Pori.

“Kati ya wanafunzi 27 waliosimamishwa, wanafunzi 17 ni kutoka mafunzo ya ngazi ya Sajenti na wanafunzi 6 ni kutoka mafunzo ya ngazi ya Kopro,” ameeleza Mungi

Aidha Mungi amesema kuwa wahitimu 2,752 waliofaulu na wamepata mafunzo tofauti kutoka katika masomo 13 waliyosoma ikiwemo masomo ya uongozi na sheria ambayo yanalenga kuwaongea maarifa, kukuza ujuzi wa stadi za kazi zao na kupandisha viwango vya tabia njema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks