Sababu, madhara wanandoa kuchepuka

July 2, 2025 5:32 pm · Fatuma Hussein
Share
Tweet
Copy Link
  • Malezi na kukosa faraja vyatajwa kuchochea wanandoa kuchepuka.
  • Wanaume kukosa ujasiri wa kujiamini chanzo afya ya akili.

Dar es Salaam. Kuchepuka katika ndoa si tu jambo la faragha kati ya wanandoa wawili, bali ni changamoto ya kijamii inayobeba athari kubwa kwa familia na taifa kwa ujumla.

Wimbi la usaliti katika ndoa limeendelea kukua kwa kasi, likivunja nguzo za mawasiliano, kulea watoto katika mazingira yasiyo na utulivu na kusababisha ongezeko la talaka na msongo wa mawazo.

Kwa mujibu wa takwimu za Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA), idadi ya ndoa zilizosajiliwa iliongezeka kutoka 41,456 mwaka 2021 hadi 51,011 mwaka 2022 sawa na ongezeko la asilimia 18.7.

Hata hivyo, mwaka 2023 idadi hiyo ilipungua hadi kufikia 40,648, ikiwa ni upungufu wa asilimia 23. 

Wakati huo huo, talaka zilizosajiliwa ziliongezeka hadi 711 kutoka 447 za mwaka 2022 hadi 711 sawa na ongezeko la asilimia 59.1.

Kuongezeka kwa talaka kunaibua maswali mazito kuhusu nini hasa kinachoendelea ndani ya mahusiano ya ndoa. 

Je, ni tamaa, ukosefu wa malezi bora, au athari za kisaikolojia? Na nini hatima ya watoto na familia nzima pale uaminifu unapopotea? Usikae mbali makala hii inaenda kujibu maswali yako yote.

Sababu wanandoa kuchepuka

Mtaalamu wa mahusiano na ndoa kutoka mkoani Tanga Leyla Abubakari anasema malezi na tabia binafsi ni miongoni mwa sababu kuu zinazowachochea wanandoa kuchepuka.

Watu waliokulia katika familia zisizo na uaminifu au zilizokuwa na migogoro mingi ya kindoa huwa na athari za kisaikolojia zinazoweza kuathiri mahusiano yao ya baadaye.

“Mtu akizoea kuwa na mahusiano mengi kabla ya ndoa, huwa ni vigumu kwake kutulia na mtu mmoja,” anasema Abubakari. 

Kukosekana kwa mfano mzuri wa ndoa katika familia pia huathiri mtazamo wa mtu kuhusu uaminifu.

“Mtu amekuwa akiona baba yake anatoka nje ya ndoa au mama yake akifanya kwa baba yake kwa hiyo na yeye anaona kuwa hivyo ndoa ndivyo inavyotakiwa kuwa,’’ anaeleza mtaalamu huyo wa mahusiano. 

Afya ya akili

Changamoto za kisaikolojia kama vile msongo wa mawazo, wasiwasi, na hali ya kutokujithamini huweza kuchangia mtu kufanya maamuzi yasiyo ya busara, ikiwemo kuchepuka.

Hata hivyo, mwanasaikolojia huyo anasema kuwa wanaume wengi hukosa kujiamini na hutumia mahusiano mengi ya kimapenzi kama njia ya kuonyesha uanaume wao.

“Wanaume wengi siku hizi wanakosa ule ujasiri wa kujiamini, kwa hiyo hawana njia nyingine ya kuonyesha ujasiri wa kujijengea uwezo wao katika jamii zaidi ya kuwa na idadi kubwa ya wanawake, wanaamini utakapokuwa na idadi kubwa ya wanawake wewe ni rijali,” anasisitiza Abubakari.

Changamoto za kisaikolojia kama vile msongo wa mawazo, wasiwasi, na hali ya kutokujithamini huweza kuchangia mtu kufanya maamuzi yasiyo ya busara, ikiwemo kuchepuka. Picha/ Canva.

Ushawishi wa marafiki

Marafiki wanaweza kuwa na ushawishi mkubwa katika maamuzi ya mtu, iwe ni kwa njia ya moja kwa moja au isiyo ya moja kwa moja.

Kundi la marafiki linalodharau ndoa na uaminifu huweza kumfanya mtu aone kuchepuka kama jambo la kawaida. 

“Marafiki wengine huwadhihaki wanaume wanaoshikamana na wake zao wakisema ‘amekaliwa na mke wake,’ jambo ambalo linaweza kuathiri maamuzi ya mtu,” anaeleza.

Sio kila rafiki anatarajiwa kuwa na tabia mbaya lakini watu hutaka kuendana na mazingira ya jamii wanayoishi hivyo kuna uwezekano mkubwa wa wao pia kuiga mwenendo huo.

Mara nyingine, hisia hizi za kutoridhishwa huhusiana zaidi na mawasiliano duni kuliko uwezo wa mwanaume. Picha/ Canva.

“Wengine ni watu tu wazuri lakini marafiki wanawambia huwezi kuwa na mtu mmoja wewe sio mchungaji, wewe sio padri. Wakiona mwanaume anayemtii mke wake utasikia huyu mke wake kamkalia, hawezi kuwa sawa,” ameongeza Abubakari.

Kiongozi wa dini ya Kiislamu na mshauri wa masuala ya ndoa  Maalim Abbasi kutoka mkoani Dar es Salaam, anaeleza kuwa mwanamke kutokutoshelezwa na mwanaume kihisia ni miongoni mwa sababu zinazochochea wanawake wengi kuchepuka.

Kutokufikia kiwango cha kuridhishwa kimwili na mwenza wake kunaweza kumfanya mwanamke ahisi kutengwa au kutothaminiwa. 

Mara nyingine, hisia hizi za kutoridhishwa huhusiana zaidi na mawasiliano duni kuliko uwezo wa mwanaume.

Tamaa ya kipato

Changamoto za kifedha zinaweza kuchangia migogoro katika ndoa. Kwa mfano, wanandoa wanapokumbwa na ugumu wa kifedha kama vile mishahara midogo, gharama kubwa za maisha, au majukumu mazito ya kifamilia ikiwemo kulea watoto au kusaidia ndugu, mara nyingi hushindwa kupata muda wa kuzungumza kwa amani au kupanga mustakabali wao kwa pamoja. 

Pesa haitatui kila shida ila inaweza kusaidia kuleta amani kwenye familia.Picha/ Canva.

Hali hii huweza kuwafanya baadhi ya watu, wakiwemo wanawake wanaofanya kazi, kuhisi kuwa hawathaminiwi au hawapati msaada wa kutosha kutoka kwa wenza wao. 

Wengine huamua kutafuta msaada wa kifedha kutoka kwa watu wa nje ya ndoa, jambo ambalo huweza kuvuruga misingi ya uaminifu.

Kukosa faraja

Abbas ameeleza kuwa kwa mujibu wa vitabu vya dini mwanaume ana haki kwa mwanamke na mwanamke ana haki kwa mwanaume na kukosekana kwa haki hizi kunachangia kwa kiasi kikubwa tabia ya kuchepuka katika ndoa nyingi.

Aidha, maendeleo ya utandawazi na matumizi ya mitandao ya kijamii yamekuwa kichocheo kikubwa cha kuchepuka kwa wanandoa wengi ambao wanakosa faraja na mawasiliano ya karibu katika ndoa zao hivyo wanatafuta hisia hizo kwenye majukwaa ya mitandaoni. 

Hali hii huanza kwa mazungumzo ya kawaida lakini huweza kugeuka kuwa mahusiano ya kimapenzi ambayo huishia kuvunja ndoa.

Mapenzi pekee hayatoshi kuifanya ndoa iwe na furaha daima kuna muda uwepo wa kipato unaweza kupunguza migogoro katika ndoa. Picha/ Canva.

Anasisitiza kuwa mwanaume anapokosa utulivu na mapokezi mazuri kutoka kwa mke wake hasa baada ya kurudi nyumbani akiwa amechoka anaweza kujikuta akihisi kutothaminiwa na kushindwa kupata furaha anayotarajia katika ndoa ,

“Mwanaume kinachomfanya aende nje ni kuukosa utulivu ndani ya nyumbani, unaona mwanaume amekuja amechoka hakaribishwi vizuri, haandaliwi vizuri, hivyo anakosa furaha ya ndoa.

Kwa mujibu wa Abbasi kati ya watu 10 wanaopelekea mashtaka kwake watu nane kati yao mashtaka yao ni wenza wao kuchepuka. 

Kupungua kwa hamasa ya mapenzi

Baada ya kuwa katika ndoa kwa muda, baadhi ya wanandoa huanza kuhisi kuwa hamasa ya mapenzi imepungua. 

Kukosa mguso wa kimapenzi au hisia za karibu kunaweza kusababisha mmoja wa wanandoa kutafuta uhusiano wa nje ili kujaza pengo hilo.

Kukosa mguso wa kimapenzi au hisia za karibu kunaweza kusababisha mmoja wa wanandoa kutafuta uhusiano wa nje. Picha/Canva.

Ingawa Abbasi amebainisha kuwa wanawake wengi hawana uelewa mzuri kuhusu mapenzi, hivyo suala la kufikishana kileleni limekuwa ni changamoto kwa wanandoa. Sababu hii inaweza kuchangia baadhi ya wanaume kutoka nje ya ndoa kutafuta mbadala.

Wanandoa wanalipi la kusema?

Mariam John mkazi wa Dar es Salaam anasema kuwa kwa sasa si wanaume tu wanaochepuka bali hata wanawake wamekuwa sehemu ya tatizo. 

Anasema sababu zinazowafanya wanandoa kuchepuka ni pamoja na ugumu wa maisha na kusalitiwa na waume zao.

Wanandoa wakivishana pete siku ya harusi yao. Picha/ Canva.

Naye, Abdallah Ngereza wa Mkoa wa Tanga anaeleza kuwa wanawake wanachepuka kwenye ndoa zao kwa sababu baadhi ya wanaume hawajui namna ya kuishi na mwanamke.

“Mwanamke akikosa hitajio lake la kimaumbile, moyo wake unapata majeraha yaani inaweza kufika akawa hajali. Hitajio la kihisia lazima ulitafute, mwanamke akipata mwingine anayemjali lazima achepuke,’’ anaeleza Ngereza.

Athari za kuchepuka 

Kuchepuka hupoteza mapenzi na kuondoa uaminifu katika ndoa, jambo linaloweza kusababisha migogoro, talaka au hata maamuzi mabaya kama kujiua. 

Vilevile, wenza huathirika kisaikolojia, ambapo aliyeumizwa hupata maumivu ya kihisia na aliyechepuka huishi na hatia. Pia watoto huathirika kutokana na migogoro ya wazazi, hali inayoweza kuharibu malezi na tabia zao.

Kuchepuka kunayumbisha hali ya kiuchumi ya familia kwa kuwa mhusika hulazimika kugharamia maisha ya mchepuko na familia kwa wakati mmoja. 

Kwa kuimarisha mawasiliano na kutafuta msaada wa kitaalamu, wanandoa wanaweza kuepuka madhara haya na kudumisha ndoa zenye amani.

Follow Us on TikTok

Subscribe to Our YouTube Channel

Subscribe

Loading videos...

Loading videos...

Loading videos...

Enable Notifications OK No thanks