Chungu; Malezi ya mzazi mmoja Tanzania

February 27, 2025 3:50 pm · Kelvin Makwinya
Share
Tweet
Copy Link
  • Baadhi ya wazazi wakiri kuelemewa na majukumu.
  • Wanasaikolojia wasema ongezeko la familia za mzazi mmoja linatokana na sababu mbalimbali, ikiwemo mifumo ya makuzi na malezi ambayo watu hupitia. 

Dar es Salaam. Katika kijiji cha Kisopwa Barabarani, mkoa wa Pwani, Daudi Frank (30), anajikuta katika jukumu la kulea mtoto wake wa miezi sita peke yake baada ya mama wa mtoto huyo kuamua kuondoka.

Bila kuwa na chaguo Frank anaamua kuanza safari hiyo ya malezi kama baba na mama kwa mtoto huyo ambaye safari yake ya ukuaji bado changa ikitaji ungalizi zaidi.

“Mwanzo ilikuwa vigumu sana, nilikuwa sijui nifanye nini mtoto anapolia usiku, wakati mwingine nilihisi kama nimeshindwa, lakini sikutaka kumkatisha tamaa mwanangu. Niliamua kuwa baba na mama kwa wakati mmoja” amesema Frank.

Si Frank pekee aliyekutana na hali hiyo ya kulea peke yake, Neema Leonard (43) mama wa watoto watatu na yeye ni muhanga wa malezi ya upande mmoja ikisababishwa na kutalakiana na baba wa watoto hao.

Ni vigumu kwa mzazi mmoja pekee kuweza kubeba majukumu ya kijinsia kwa mtoto wa jinsia tofauti. Picha | Imehaririwa na Grok AI.

Hali anayokutana Frank na Neema imekuwa ikiongezeka siku za karibuni ikichangiwa na sababu mbalimbali ikiwemo talaka, vifo au kutengana kwa wazazi na kusababisha mzigo wa malezi kubakia kwa mzazi mmoja.

Utafiti uliofanywa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kwa kushirikiana na ICF Macro mwaka 2010, uliochapishwa mwaka 2011, unaonyesha kuwa asilimia 24 ya watoto nchini Tanzania wanalelewa na mzazi mmoja.

Asilimia 19 kati yao wanalelewa na mama pekee, huku asilimia tano wakilelewa na baba pekee.

Aidha, Takwimu za Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) zinaonyesha kuwa mwaka 2019 talaka zilikuwa 442, mwaka 2020 zilifikia 511 na mwaka 2021 ziliongezeka hadi kufikia 550 jambo linaloendelea kuchangia kuongezeka kwa watoto wanaolelewa na mzazi mmoja.

Kuongezeka kwa Idadi ya Talaka ni kiashiria cha ongezeko la familia zenye mzazi mmoja.

Wanasaokolojia waeleza sababu

Mwanasaikolojia wa kujitegemea Deo Sukambi ameiambia Nukta Habari kuwa ongezeko la familia za mzazi mmoja linatokana na sababu mbalimbali, ikiwemo mifumo ya makuzi na malezi ambayo watu hupitia. 

Sukambi anasema kuwa watu waliokua katika mazingira yenye migogoro ya kifamilia au unyanyasaji kati ya wazazi wao mara nyingi huathirika kisaikolojia, jambo linalowafanya wengi kuamua kuishi peke yao.

“Mtu anayekulia kwenye familia yenye migogoro hukua na wasiwasi mwingi au mtazamo hasi kuhusu familia, hali inayoweza kumfanya aamue kutokuwa na familia ya kawaida,” ameeleza Sukambi.

Mwanasaikolojia huyo amebainisha kuwa mifumo ya familia isiyo na usawa ambayo mzazi mmoja ana mamlaka makubwa kuliko mwingine huathiri watoto kisaikolojia na kuwafanya wawe na mtazamo hasi kuhusu ndoa na familia. 

“Familia yenye baba au mama aliye na nguvu kupita kiasi inaweza kusababisha watoto kuhofia kuwa na familia kwa kuhisi kutawaliwa na wenza wao,” amesema Sukambi.

Sukambi pia amesisitiza kuwa watoto waliolelewa na mzazi mmoja wana uwezekano mkubwa wa kuanzisha familia za mzazi mmoja, kwani hukosa mifano ya jinsi ya kushirikiana na mzazi wa pili.

Mbali na hayo, utandawazi na kuenea kwa desturi za magharibi pia vimetajwa kuwa vichocheo vya kuongezeka kwa familia za mzazi mmoja. 

Familia bora hujengwa na mama, baba na watoto, Picha | Amka Tanzania.

Malezi ya mzazi mmoja ni mzigo

Baada ya kutalakiana  na mzazi mwenzie Neema alilazimika kubeba majukumu ya kulea watoto mwenyewe huku akikabiliwa na ukata unaomfanya ashindwe kumudu baadhi ya gharama ikiwemo ada za shule.

“Sikuwahi kusahau siku ambayo mwanangu alishindwa kwenda shule kuanza darasa la kwanza wakati nilikuwa nimesha muandikisha, lakini sikuwa na pesa ya sare. Iliniumiza sana…

“…Najitahidi kuhakikisha wanakula, wanavaa, na hata kupata elimu, lakini maisha ni magumu sana ni ngumu sana kulea watoto peke yako,” amesema Neema kwa huzuni. 

Mtoto anapokosa sauti ya baba au mama katika maisha yake, kuna mambo muhimu anayoweza kukosa kujifunza. Picha | Medium.

Sukambi anasema kuwa mbali na aina hiyo na malezi kuwa kusababisha mzigo kiuchumi pia huweza kusababisha changamoto maendeleo yao ya kihisia na kijamii.

“Mtoto anapokosa sauti ya baba au mama katika maisha yake, kuna mambo muhimu anayoweza kukosa kujifunza, kama vile jinsi ya kushirikiana, kuonyesha upendo, au hata kujifunza jinsi ya kushughulikia migogoro kwa njia ya kiutu uzima,” amesema Sukambi.

Pia, watoto kutoka familia za mzazi mmoja mara nyingi hukabiliwa na hisia za upweke na wakati mwingine lawama za nafsi, hasa wanapokuwa hawana majibu ya kutosha kuhusu kwa nini wazazi wao hawako pamoja. Hali hii inaweza kuchangia matatizo ya kihisia kama vile unyogovu au wasiwasi wa kijamii.

Pamoja na athari hizo watoto hao ambao hulelewa na mzazi mmoja hukumbana na changamoto za kijinsia zinazoweza kusababisha momonyoko wa maadili au kushindwa kukabiliana na majukumu baadae.

“Kwa mfano, mtoto wa kiume anayelelewa na mama pekee anaweza kukosa mfano wa kuigwa wa kiume, jambo ambalo linaweza kumzuia kuelewa baadhi ya majukumu ya kijinsia au kujiandaa kikamilifu kuwa baba bora

…Hali hii inaweza kusababisha watoto kuathirika kitabia, kwa kuwa wanakosa mfano wa moja kwa moja wa jinsi ya kushirikiana na jinsia nyingine,” ameongeza Sukambi.

Hata hivyo, Sukambi anasisitiza kuwa watoto kutoka familia za mzazi mmoja wanaweza kufanikiwa ikiwa mzazi atahakikisha wanapata upendo, mwongozo, na msaada wa kijamii kutoka kwa familia au marafiki wa karibu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks