Mbinu tatu za kukwepa maumivu ya mikopo umiza Tanzania

February 15, 2024 3:37 pm · Nuzulack Dausen
Share
Tweet
Copy Link
  • Usichukue mkopo bila malengo yeyote, fanyia shughuli za uzalishaji upate marejesho.
  • Hakikisha taasisi unayochukua mkopo imesajiliwa na mamlaka husika
  • Soma kwa makini vigezo na masharti kabla ya kukubali kupokea mpunga.

Zanzibar. Miaka ya hivi karibuni baadhi ya Watanzania wamejikuta wakiingia kwenye lindi la madeni baada ya kukopa kwenye taasisi za kifedha zenye masharti magumu na riba kubwa inayopukutisha vibubu vyao.

Sehemu kubwa ya wanaolizwa ni wale wanaopata mikopo kwenye taasisi za huduma ndogo za fedha ukitofautisha na taasisi kubwa za kifedha kama benki za biashara zenye mifumo imara ya huduma.

Hata hivyo, jambo ambalo wengi hawafahamu ni kuwa baadhi ya maumivu hayo yangeepukika iwapo wangekuwa makini kabla ya kuingia makubaliano na mtoa huduma hizo za mikopo.

Kwa mujibu wa Deogratius Mnyamani, Ofisa Mwandamizi Mkuu wa Idara ya usimamizi huduma ndogo za fedha wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), kuna mambo makuu matatu ya kuyafuata kabla ya kumwaga wino au kubonyeza “kubali” kwenye simu yako ili upate mkopo likiwemo uhalali wa taasisi unayotaka kukopa.


1. Usichukue mkopo bila malengo

Mtaalamu huyo anaonya kuwa wapo baadhi ya watu hujikuta wakienda kwenye taasisi za kifedha kuchukua mkopo bila ya kuwa na malengo yeyote muhimu kiasi cha kufanya wakopaji wazitumbue fedha bila uhakika wa kupata fedha za kurejesha.

Jambo la msingi kufahamu hapa ni kwamba mkopo si zawadi bali ni fedha unazotakiwa kurejesha baada ya kufanyia shughuli za uzalishaji.

Mnyamani anasema siyo sahihi kuchukua mkopo kwa ajili ya kushonea sare au kumtunza rafiki yako kwenye “birthday” (siku yake ya kuzaliwa) kwa kuwa shughuli hizo hazirejeshi maokoto zaidi ya kupukutisha kibubu.

“Tunashauri ukishakuwa na madeni usiingie kuchukua mikopo itakayokuongezea mzigo wa madeni. Siku zote chukua mkopo na uingize kwenye shughuli za uzalishaji zitakazokusaidia kupata fedha za kurejesha deni lako…

…hiyo birthday itasaidia kurejesha mkopo?” amesema mtalaamu huyo huku akibaninisha kuwa baadhi ya watu walioenda BoT kulalamika hawakuwa na malengo ya kukopa.

Zahanati ya Afya ya Jamii iliyopo Kipunguni jijini Dar es Salaam iliyoanzishwa na vijana nane kwa mkopo wa Halmashauri ya Wilaya ya Ilala. Kufahamu vema malengo ya mkopo hususan yanayohusisha shughuli za uzalishaji husaidia mkopaji kuwa na uhakika wa marejesho. Picha| Esau Ng’umbi/Nukta.  

2. Usichukue mkopo kwenye taasisi ambayo haijasajiliwa

Katika harakati za kusaka fedha kujikwamua na shida iliyokushika ni rahisi tu kuingia makubaliano ya mkopo na taasisi iliyo tayari kukukopesha.

Kwa wakati huo inawezekana kutosajiliwa kwake isiwe nongwa lakini ukweli ni kwamba taasisi isiyosajiliwa ni hatari zaidi hasa pale mtakaposhindwana katika kurejesha mkopo na yenyewe kuanza kukushughulikia ikiwemo kunyang’anya mali au kukutoza riba na tozo za juu ambazo hujawahi kuzifikiri.

“Kamwe usichukue mkopo kwenye taasisi isiyokuwa na leseni. Kabla ya kuingia makubaliano ya kuchukua mkopo jiulize, hii taasisi imesajiliwa au la?,” Mnyamani ametoa ushauri huo wakati wa semina kwa wahariri na wanahabari wa biashara na uchumi visiwani Zanzibar leo, Februari 15, 2024. 

Uzuri wa kuchukua mkopo kwenye taasisi iliyosajiliwa ni rahisi kupata haki yako kwenye mamlaka za kiudhibiti na mahakamani pale unapominywa haki yako. Baadhi ya watu Tanzania wamelizwa baada ya kuweka fedha au kukopa kwenye taasisi ambazo hazijasajiliwa kutoa huduma hiyo jambo lililowanyima kupata haki zao.

Mfano, kuna vijana nane wahitimu wa elimu ya juu jijini Dar es Salaam ambao waliamua kuchukua mkopo wa halmashauri wakiwa na malengo ya kuanzisha kituo cha afya ili kupunguza changamoto ya wagonjwa kutembea umbali mrefu. Kwa sasa zahanati walioanzisha kwa mkopo huo imekua na ni tegemeo kwa jamii inayowazunguka huku wakiwa na uhakika wa kurejesha mkopo wao. 

Ofisa Mwandamizi Mkuu wa Idara ya usimamizi huduma ndogo za fedha wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Deogratius Mnyamani anaeleza kuwa miongoni mwa mambo yanayowaliza wengi ni kukubali mikataba ya mikopo bila kusoma na kuelewa masharti na vigezo vya huduma. Picha: John Bukuku/Full Shangwe Blog. 

3. Soma vigezo na masharti kabla ya kukubali mkopo

Baadhi ya mikataba ya mikopo huwa na karatasi nyingi sana zenye mwandiko wenye herufi ndogo ndogo zilizochapwa. Uvivu wa kusoma masharti na vigezo vinaweza kukuletea majuto kiasi cha kuathiri mustakabali wa maisha yako na ya familia yako.

Mtaalamu huyo wa BoT anasema ni vizuri ukaomba ueleweshwe vizuri riba ya mkopo unaouingia italipwa kwa kipindi gani, je, ni kwa siku, mwezi au mwaka? Je, kuna gharama nyingine za kuuhudumia mkopo husika kama bima na gharama nyinginezo? Kama zipo ni kiasi gani? Iwapo nitachelewa kurejesha marejesho kwa muda husika nitapigwa faini kiasi gani?

Mnyamani anaeleza kuwa licha ya BOT kutaka riba itegemee nguvu ya soko lakini wameweka ukomo wa riba kwa taasisi za fedha zilizopo daraja la pili la watoa huduma ndogo za fedha ambazo zinahusisha taasisi za kifedha zisizopokea amana ili kuwalinda wateja na watoa huduma.


Soma zaidi:

 Mikopo ya halmashauri inavyoweza kupunguza umaskini, ukosefu wa ajira Tanzania

Nukta the Podcast: Ifahamu zahanati iliyoanzishwa kwa mkopo wa halmashauri


Anaeleza kuwa BOT imetoa bei elekezi ya kupata mkopo kwenye taasisi zilizopo daraja la pili ambayo ni riba ya asilimia 3.5 kwa mwezi ya kiwango ulichokopa inayopigiwa hesabu kwa njia ya ‘reducing balance’ (inayobadilika au kupungua kwa kadri deni linavyolipwa).

“Ukipiga hesabu hapa kwa mwaka ni kama asilimia 42…hi si ndogo kwa mkopaji na wala si kubwa kwa mkopeshaji. Unaweza kukopesha kwa riba chini ya hapo kwa kuwa zipo taasisi zinazokopesha hadi asilimia 2 kwa mwezi,” anaeleza.

Hakikisha unatembelea taasisi mbalimbali za kifedha ili kutafuta ile yenye masharti rafiki na riba ambayo haitakuumiza sana hapo baadaye.

Pamoja na kufuata mbinu hizo za kupunguza maumivu yatokanayo na mikopo umiza, wataalamu wa masuala ya huduma za benki wanaonya kuwa ni vema mkopaji akarejesha deni lake kwa wakati ili kusaidia watu wengine wapate fursa za kukopa.

Uaminifu katika urejeshaji deni lako unasaidia kukuongezea sifa za kukopesheka na taasisi yeyote ya kifedha zikiwemo benki za biashara.

Masoko & Zaidi
Loading…
No recent matches
No upcoming matches
/
No matches found for this filter
18 Jun, 2026 · TZS
No forex gainers today
No forex losers today
Forex rates unavailable
19 Jun, 2026 · TZS
No gainers today
No losers today
19 Jun, 2026
No active movers today

Inaendeshwa na Nukta AI

Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
Siku ya Familia, Mtoto wa Afrika kuadhimishwa Juni 30, 2026

Siku ya Familia, Mtoto wa Afrika kuadhimishwa Juni 30, 2026

Nukta TV

Wadau wa 'kubet" watoa ya moyoni, pendekezo kupanda kwa tozo 5%

Wadau wa 'kubet" watoa ya moyoni, pendekezo kupanda kwa tozo 5%

Nukta TV

Wasemayo wananchi, vocha za kukwangua kupigwa maruku mijini

Wasemayo wananchi, vocha za kukwangua kupigwa maruku mijini

Nukta TV