Ripoti mpya yapendekeza njia ya kuwanusuru wanahabari na ukatili Tanzania

June 16, 2023 3:54 pm · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni pamoja na kubadili sera zitakazolinda usalama wa waandishi wakiwa kazini.

Dar es Salaam. Licha ya kuwa mstari wa mbele kuhabarisha umma, wanahabari wamekuwa wakikumbwa na matatizo lukuki ukiwemo ukatili wa kijinsia jambo linalowarudisha nyuma kutekeleza majukumu yao ipasavyo.

Wanahabari ni nguzo muhimu katika jamii kutokana na kazi yao ya kuibua changamoto, kuongeza uwazi na uwajibikaji na kuchochea maendeleo nchini.

Hata hivyo, wanahabari wengi wanafanya kazi katika mazingira magumu na sasa ripoti mpya ya utafiti uliofanywa na Kituo cha Africa Freedom of Information Centre (AFIC) inashauri marekebisho ya kisera ili kulinda  usalama wa wanahabari na hasa wanawake.

Ripoti hiyo iliyoangazia zaidi masuala ya usalama wa kijinsia kwa waandishi wa habari nchini ni matokeo ya utafiti uliofanywa katika nchi za Tanzania, Kenya na Uganda mwaka 2016 mpaka mwaka 2021.

“Katika mazingira ambayo Serikali hazina sheria, sera, na mifumo mahususi ya kitaasisi inayoshughulikia usalama wa wanahabari wa kike hauwezi kushughulikia ipasavyo vitisho na vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake,” Mratibu Ufuatiliaji na Tathmini wa AFIC,  Charity Komujjurizi,  alisema wakati wa uzinduzi wa matokeo ya utafiti huo Juni 16, 2023  jijini Dar es Salaam. 

Katika utafiti uliofanywa na AFIC, imegundulika changamoto zinazo wakumba waandishi wa habari wanawake zimesababisha kuwe na asilimia 40 tu wanawake wanaofanya kazi hiyo huku sehemu kubwa kati yao wakikosa nafasi za juu za uongozi. 

“Ripoti hiyo pia inafichua kuwa kati ya mameneja 50 katika vyombo vya habari, mwanamke mmoja tu ndiye aliye katika ngazi ya Mkurugenzi Mtendaji,” ameongeza  Komujjurizi.

Unyanyasaji wa kijinsia bado ni janga

Kwa mujibu wa utafiti huo uliofanywa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA) mwaka 2019, takriban nusu ama asilimia 48 ya wanawake katika vyombo vya habari nchini walifanyiwa unyanyasaji wa kijinsia.


Soma zaidi


Mbali na unyanyasaji wa kijinsia waandishi wa habari nchini wameendelela kukumbwa na vitisho, kukamatwa, kuwekwa kizuizini kinyume cha sheria, pamoja na utekaji nyara mambo yanayoongeza hofu na kuathiri utendaji wa kazi zao.

‘Wanahabari wapewe vifaa vya usalama’

AFIC wamependekeza waandishi wa habari kupewa vifaa vya kulinda usalama wao wakati wote wanapokuwa wanatekeleza majukumu yao ndani na nje ya ofisi.

“Usalama kwa wanahabari lazima ujumuishe kutoa vifaa vya usalama kwa wanahabari wote, kimwili na kiteknolojia…wanahabari wanapaswa kuhimizwa kufanya kazi katika timu inapofaa ili kuhakikisha usalama wao,” alisema Charity.

Kuwajengea uwezo waandishi wa habari

AFIC imependekeza kuwa programu za mafunzo na kujenga uwezo kwa wanahabari ziandaliwe na kutekelezwa ipasavyo ili kuhakikisha usalama wa wanahabari hususani kimwili, kiakili na kisakolojia kwa walioathirika na vitendo vya ukatili kazini.

“Mafunzo yanapaswa kujumuisha ufuatiliaji, uwekaji kumbukumbu, kuripoti usalama wa wanahabari, utoaji wa huduma za kisheria, za kisaikolojia na kijamii,” inasomeka sehemu ya ripoti ya utafiti huo wa AFIC.

Wadau mbalimbali wa maendeleo ya sekta ya habari, wamekuwa wakitoa mafunzo kwa wanahabari na wahariri katika kuboresha kazi zao na kujilinda na masuala yanayotishia usalama wao. 

Miongoni mwa wadau hao ni kampuni ya Nukta Africa ambayo imekuwa ikitoa aina ya mafunzo hayo kwa zaidi ya miaka mitano.

Wadau wa habari wanasema kuwa maboresho ya sera ndani ya vyombo vya habari husika yatasaidia zaidi kuwanusuru wanahabari na matatizo yanawakabili kwa sasa. 

Mwenyekiti wa Taasisi  ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Africa  (MISA) nchini Tanzania, Salome Kitomari, alisema sera hizo lazima ziwe jumuishi ili zihakikishe kwamba wanahabari wanawake na wanaume wanafanya kazi katika mazingira mazuri.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW