Wanawake zaidi ya 100,000 watakavyofaidika na ujuzi wa kidijitali Tanzania
- Watapatiwa ujuzi huo na Shirika la kutetea haki za wanawake la Pollicy.
- Watawezeshwa kutumia mitandao vizuri na kukabiliana na ukatili.
Dar es Salaam. Wanawake 200,000 wa Tanzania na Uganda wanatarajia kupata mafunzo ya matumizi sahihi ya mtandao, jambo litakalowasaidia kuwaongezea fursa ajira na kukabiliana na ukatili wa kijinsia unaotokea mtandaoni.
Mafunzo hayo yatakayotolewa na Shirika la kutetea haki za wanawake la Pollicy yanakusudia kuziba pengo la elimu ya kidijitali kati ya wanaume na wanawake katika nchi hizo mbili za Afrika Mashariki.
Kwa mujibu wa utafiti wa shirika hilo uliofanyika mwaka 2020 ulibaini kuwa kuna unyanyasaji wa kimtandao katika nchi za Afrika ambao unawagusa zaidi wanawake.
Kwa mujibu wa utafiti huo, ukatili wa mtandaoni kwa wanawake unaongoza nchini Uganda kwa asilimia 32.8 ikifuatiwa na Ethiopia (asilimia 31), Kenya (asilimia 28), na Senegal kwa asilimia 25.
Nchi zingine zenye ukatili wa kimtandao dhidi ya wanawake ni Afrika Kusini ambayo ukatili wa kijinsia upo kwa asilimia 23.3.
Kushamiri kwa ukatili huo ni matokeo ya kukosekana kwa elimu ya kutosha kuhusu matumizi ya mitandao na hivyo kuwaingiza wasichana na watoto katika unyanyasaji na uonevu ambao huathiri maisha yao ya sasa na ya baadaye.
Mwanzilishi wa Shirika hilo, Neema Lyer amesema lengo la Pollicy wakati wa uzinduzi wa programu hiyo amesema lengo ni kujenga kizazi cha wanawake wenye ujuzi wa kiteknolojia ili wawe na uwezo wa kukabiliana na changamoto za mtandaoni.
“Uzinduzi wa programu ya mabalozi wa kidijitali utasaidia matumizi mazuri ya intaneti miongoni mwa wasichana. Malengo yetu ni kuwa na teknolojia inayoigusa jamii na tutakuwa tukiwafundisha na kujenga kizazi cha wanawake wabobevu katika teknolojia,” amesema Lyer.
Mdau huyo wa masuala ya jinsia amesema wanapenda kuona idadi ya wanawake wenye uelewa wa masuala ya kidijitali ili kupata fursa mbalimbali za maisha huku wakikabiliana na ukatili wa kijinsia unaofanyika mtandaoni.
Mratibu wa mradi kutoka Pollicy, Navina Mutabazi amesema mafanikio ya programu hii yatakuwa taa ya kijani katika kuchochea programu hiyo kuwafikia wanawake wengine barani Afrika.
Latest