Mambo yanayokwamisha mapambano ya ukatili wa kijinsia mtandaoni
- Ni pamoja na ukosefu wa elimu juu ya ukatili wa mtandaoni.
- Kukosekana ushirikiano kati ya vyombo vya dola na waandishi wa habari.
- Inashauriwa Watanzania waangazie maudhui yenye kujenga.
Dar es Salaam. Licha ya uwepo kwa juhudi mbalimbali kupambana na ukatili wa kijinsia mtandaoni, bado safari ni ndefu kumaliza vitendo hivyo ambavyo vimekuwa vikiwaathiri zaidi wanawake na watoto kwa sababu ya kukosekana kwa elimu sahihi ya matumizi ya mtandao.
Ukatili huo huusisha zaidi udhalilishaji kwa kutumia maudhui ya sauti, video na maandishi ambayo watu hufanyiwa hasa katika mitandao ya kijamii.
Mratibu wa Programu kutoka Shirika la kutetea haki za wanawake la Pollicy, Navina Mutabazi amesema ukatili wa kijinsia unaofanyika mtandaoni unahusisha ufuatiliaji, udukuzi, uonevu na maneno ya kumfadhaisha mtu kimaumbile.
“Kwa upande wangu, ukatili wa kimtandao niliopitia ni kuambiwa maneno mabaya kuhusu mwili wangu,” amesema Mutabazi wakati wa mjadala wa wadau mbalimbali wakiwemo waandishi wa habari kuhusu ukatili wa kijinsia mtandaoni uliofanyika jana Februari 4, 2022 jijini Dar es Salaam.
Katika mjadala huo, wadau hao wameibua hoja mbalimbali ikiwemo sababu mbalimbali ambazo zinashamirisha ukatili huo licha ya hatua zilizochukuliwa na Serikali kutunga sheria, kanuni za kuwalinda watu mtandaoni.
Baadhi ya wadau waliohudhuria mjadala wa ukatili wa kijinsia mtandaoni ulioandaliwa na Pollicy. Picha| Rodgers George.
Baadhi ya sababu hizo ni:
Kutokuwepo na uelewa juu ya ukatili wa kimtandao
Siyo kila mtu akinenewa neno baya mtandaoni wengine hudhani kuwa huo ni ukatili. Kwa baadhi maneno mabaya ni utani na ni jambo la kawaida.
Mwandishi wa habari wa kujitegemea, Caren Joel amesema yeye ni miongoni mwa wahanga wa ukatili wa mtandaoni ambapo kuna wakati alilazimika kuachana na mitandao ya kijamii kwa sababu ya maoni hasi na udhalilishaji aliyopata kutoka mtandaoni.
“Nilikaa nje ya mitandao kwa miezi nane,” amesema Joel.
Mdau huyo wa maudhui amesema, ili kupigana na ukatili wa mtandaoni, inatakiwa watu wapewe elimu kwa upana kuhusu suala hilo kuwa “hiki ni ukatili, hiki siyo.”
Soma zaidi:
- Jinsi ya kufanya mitandao ya kijamii isikuharibie mahusiano yako
- Yaliyojificha nyuma ya mahusiano, ndoa zinazoanzia mtandaoni
- Unyanyasaji wachangia kuwakimbiza wasichana kwenye mitandao ya kijamii
Ukosefu wa takwimu kwa Waandishi wa habari
Sababu nyingine ni ukosefu wa takwimu sahihi kuhusu matukio ya ukatili wa kijinsia yanayofanyika mtandaoni ikizingatiwa kuwa baadhi ya matukio hayaripotiwi na wahusika au watumiaji wa mitandao ya kijamii huyafumbia macho kwa kujua au kutokujua.
Hali hiyo pia hurudisha nyuma harakati za kutokomeza vitendo hivyo kwa sababu inakuwa ngumu kufahamu ukubwa wa tatizo na jinsi lilivyoathiri watu kama hakuna takwimu sahihi.
Mwandishi wa habari kutoka moja ya chombo cha habari nchini, Elizabeth Edward amesema inakuwa vigumu kuripoti matukio ya ukatili bila takwimu za matukio husika.
“Upatikanaji wa takwimu za kesi za ukatili wa kimtandao bado,” amesema Edward.
Mambo mengine yanayochangia kasi ndogo ya mapambano ya ukatili huo ni pamoja na kukosekana ushirikiano baina ya wanahabari, vyombo vya dola na wahanga wa ukatili huo pamoja na taaluma ya habari kufanywa na watu ambao siyo wanahabari.
Katika mjadala huo ulioandaliwa kwa ushirikiano wa Pollicy, kampuni ya Media Convergency na maabdara ya Data Lab, wadau wa maudhui wameshauri mapambano hayo kuanza kwa kujenga uelewa kwa watumiaji wa mtandao
Pia Watanzania kubadili fikra kwa kuchagua maudhui sahihi yanayowajenga kimaisha na kuepuka jumbe zinazochochea udhalilishaji wa watu huku wakitakiwa kukemea na kuwaripoti watu wanaofanya vitendo hivyo katika mamlaka husika.