Zingatia haya kabla hujanunua oili ya gari

January 31, 2023 11:54 am · admin
Share
Tweet
Copy Link
  • Kila gari inatumia aina tofauti ya oili, usikariri, usijichanganye!
  • Utofauti mkuu upo kwenye ‘viscosity’ (wepesi au uzito). 
  • Inatakiwa kubadilishwa mara baada ya kilomita zake kuisha.

Dar es Salaam. Taswira ya kimiminika kizito kiasi chenye rangi nyeusi, utelezi kiasi  pamoja na harufu ya mafuta ndiyo huwa vichwani mwa wengi wasikiapo kuhusu oili. Ni zaidi ya hivyo!!

Wamiliki wa magari au vyombo vya moto vinavyohitaji kimiminika hicho ili kufanya kazi huenda wana taswira nyingine,  labda ya gharama ya oili kila wanaponunua au umuhimu wake kwenye chombo hicho.

Watu wengi wamekuwa wakiitumia oili katika shughuli mbalimbali ikiwemo kuzuia mchwa, kufukuza wadudu hatari kama tandu na nyoka pamoja na matumizi yake yaliyozoeleka ya kilainishi kwenye injini za vyombo vya moto.


Oili ni nini?

Kwa mujibu wa John Massawe, fundi wa magari aliyepo Mabibo jijini Dar es Salaam, oili ni kilainishi kilichopo katika hali ya kimiminika ambacho hutumika kwenye baadhi ya injini za vyombo vya moto ili kupunguza msuguano.

Kawaida oili safi huwa na rangi ya kahawia au dhahabu na rangi huonekana kukolea au kufifia kutegemeana na aina ya oili au kampuni inayozalisha bidhaa hiyo.

Oili zimegawanyika katika makundi kadhaa, na kila aina ina gari zake mahususi ambayo huwezi kuitumia katika aina nyingine. Sababu ya utofauti huo ni kutokana na kila injini ya gari huwa imetengenezwa katika namna tofauti hivyo haziwezi kutumia oili aina moja.

Oili nyingine hutengenezwa kutegemeana na hali ya hewa ya eneo ambapo gari inatumika. Mathalan maeneo yenye baridi kali hutumia oili nyepesi ambayo huwahi kupata joto na kuingia kwenye mzunguko wa gari.

Kila oili inatumika kwa gari husika. Ukienda kununua oili hakikisha inaendana na gari lako. Picha | Daudi Mbapani/Nukta.

Utofauti uko hapa

Utofauti mkubwa wa oili upo katika ‘viscosity’(uzito au wepesi) wa oili inayomiminika kwenye injini kwa wakati husika.

Kuna namba mbili ambazo zinafafanua utofauti huo, nambari ya kwanza hutanguliwa na herufi ‘W’ ambayo humaanisha kiwango cha oili kinachomiminika wakati injini ikiwa imepoa na namba ya pili humaanisha kiwango cha oili kinachomiminika kwenye oili inapokuwa kwenye joto la kawaida.

Kwa hiyo namba ndogo inamaanisha oili hiyo ni nyepesi na inapita kiurahisi zaidi katika injini. Mathalan, oili ya 5W-30 itapita kiurahisi zaidi katika injini kuliko 10W-40 ambayo ni nzito.

Oili nyepesi zinafaa zaidi katika maeneo yenye baridi, huku oili nzito ikifaa maeneo yenye joto au magari makubwa ya mizigo.


Soma zaidi


Unatakiwa kubadilisha oili muda gani?

Oili hubadilishwa pale muda wake unapokuwa umekwisha. Inatakiwa kutumika katika idadi ya kilomita fulani ambazo huainishwa katika kadi ya huduma, na kila oili huwa na kilomita zake.

Mfano, oili ya 5W-50 inaweza kutumika kwenye wastani wa kilomita 5,000 hadi 9,000.

“Unaponunua oili kuna kadi unapewa, fundi lazima aorodheshe kilomita ambazo ile gari imetembea kwa wakati huo. Kwa hiyo utakuwa unafatilia kujua kama kilomita hizo zimefika, hata hivyo baadhi ya gari huwa zinatoa tahadhari kama oili imekwisha,” anasema Massawe ambaye ana uzoefu wa kutengeneza magari kwa miaka nane.

Inashauriwa pia kukagua oili kila siku kabla hujawasha gari kwa kutumia fimbo maalumu (deep stick) ili kubaini kama kuna mapungufu yoyote.

Oili ni moja kati ya kiungo muhimu kwenye gari. Picha | Daudi Mbapani/Nukta

Madhara ya kutobadilisha oili kwa wakati

Kazi kubwa ya oili katika injini ni kupunguza msuguano wa vyuma vinavyofua nguvu inayotumika katika chombo husika. Iinapokosekana husababisha msuguano kuwa mkubwa ambapo injini inaweza kuungua au kufa au tope la oili kuziba baadhi ya mifumo muhimu.

Fundi Massawe anashauri ni muhimu kufahamu aina ya oili inayopaswa kutumika kwenye chombo chako kabla ya kuinunua, kupata kadi ya marekebisho unaponunua oili, na kuibadilisha kwa wakati pale unapobaini muda wake umekwisha.


Tangazo:

Enable Notifications OK No thanks