Fahamu mambo ya kufanya kabla hujawasha gari asubuhi
- Ni pamoja na kukagua ‘oili’ na maji.
- Itakusaidia kuepuka matengenezo ya gharama kubwa au kupoteza kabisa chombo chako.
Dar es Salaam. Je! Ni kitu gani cha kwanza huwa unafanya kabla ya kuwasha gari yako asubuhi, unafanya ukaguzi wowote, au msukumo wa kuwahi sehemu husika ndiyo kipaumbele chako?
Je! Unafahamu kuwa asilimia kubwa ya watu wanaoharibikiwa magari yao na kutumia gharama kubwa kufanya matengenezo hutokana na kupuuzia dalili za tatizo husika au kutofanya uchunguzi wa gari yake mara kwa mara?
Itakumbukwa Januari 20, 2023, miongoni mwa habari zilizoteka vyombo vya habari nchini ni kuungua kwa gari aina yaNissan Dualis, maeneo ya Mbezi beach Tangi bovu, jijini Dar es Salaam, ambapo kwa mujibu wa shuhuda ambaye ni dereva anasema aliona tu moshi ukitokea sehemu ya injini.
Huenda nawe ni miongoni mwa wasiojua nini wanatakiwa kufanya kabla ya kuwasha gari, oondoa shaka. Kupitia makala haya utaweza kufahamu ni nini hasa unatakiwa kufanya kabla ya kuwasha gari yako jambo ambalo litakuepusha na matengenezo ya gharama kubwa au kupoteza kabisa chombo chako cha usafiri.
Soma zaidi
-
Kwaheri: Necta yafuta orodha ya 10 bora kidato cha nne Tanzania
-
Necta yatangaza matokeo kidato cha nne 2022, ufaulu waongezeka kiduchu
-
Kuona matokeo kidato cha nne bonyeza hapa
Angalia kiwango cha maji
John Massawe ambaye ni fundi wa magari Mabibo jijini Dar es Salaam ameiambia Nukta Habari (www.nukta.co.tz) kuwa kabla ya kuwasha gari asubuhi ni muhimu kuangalia kwanza kiwango cha maji kilichopo kwenye rejeta.
“Injini ya gari inapofanya kazi huzalisha joto ambalo linatakiwa kupoozwa ili injini ifanye kazi kwa ufanisi, na maji ndiyo hufanya kazi hiyo. Kukosekana kwa maji kwenye mfumo wa upozaji huweza kusababisha joto kuwa jingi kupita kiasi na hivyo gari hukosa nguvu au mafuta yanaweza kuchanganyika na oili, “ amesema Massawe.
Kagua ’oili’ na ‘haidroliki’ (vilainishi)
Oili (mafuta lainishi) ni miongoni mwa vimiminika muhimu sana kwenye gari, injini ya gari imeundwa na vyuma ambavyo huzunguka ili kuipa gari nguvu ya kutembea, vyuma hivi vinatakiwa kulainishwa ili kuepusha msuguano.
Mfumo wa gia pia umetengenezwa katika namna ambayo unahitaji kilainishi (haidroliki) ili ufanye kazi kwa ufasaha. Massawe anashauri kutumia vifaa vya kupimia oil kama (deep stick), ambayo huwa na namba maalumu zinazoonesha kiwango kinachotakiwa.
Aidha aina zote za oili yaani (ya injini na ya mfumo wa gia ) huwa na kilomita maalumu ambazo gari ikishatembea zinatakiwa kubadilishwa, ni muhimu kuzingatia na kubadili oili kwa wakati ili kuepuka athari hasi.
‘Deep stick’ kifaa cha kuangalizia kiasi cha oili kilichopo katika injini kwa wakati husika.Pichal Esau Ng’umbi, Nukta Africa
Washa gari na sikiliza muungurumo
Wakati mwingine tatizo linaweza kuwa ndani ya gari au sehemu ambayo huwezi kuona kwa macho mpaka ifunguliwe, hivyo kupitia kusikiliza muungurumo wa gari unaweza kubaini kama kuna mabadiliko yoyote.
Massawe anashauri kuiacha gari ikiunguruma wastani wa dakika kumi kwa gari ndogo na dakika 15 kwa gari kubwa hususani zinazotumia ‘turbo’ ili kuipa nafasi oili kupata joto na kuingia kwenye mzunguko wa injini.
“Gari za turbo hutakiwi kuiwasha na kuweka gia moja kwa moja uondoke utapelekea kuua mfumo wa turbo, unatakiwa uiache kidogo oili ipate joto kisha itaanza kupanda kwenye mfumo, hii ipo kwenye magari makubwa ya mizigo au gari ndogo zenye mfumo huo,” amesema Massawe.
Kagua tairi zote
Gari hutembea kwenye mwendo thabiti ikiwa na tairi zenye uwiano sawa wa hewa (upepo) ikiwa tairi moja ina mapungufu huathiri mwendo wa gari pamoja na uwezo wa dereva kuiongoza inavyotakiwa.
Inashauriwa kukagua upepo katika tairi za gari kabla ya kuanza kuendesha ili kubaini kama kuna mabadiliko yoyote.
Ni muhimu kuwasiliana mara moja na mtaalamu au fundi wa magari pale unapobaini changamoto katika gari yako badala ya kulazimisha kuitumia hivyo hivyo jambo ambalo litasababisha tatizo kuwa kubwa zaidi au kutengeneza tatizo jingine.
Latest



