WhatsApp kuruhusu matumizi namba zaidi ya moja

Davis Matambo 0907Hrs   Agosti 17, 2023 Teknolojia
  • Mtumiaji ataweza kuwa na akaunti zaidi ya moja kwenye kifaa kile kile.
  • Mabadiliko yanapatikana kwa watumiaji wa WhatsApp beta pekee.

Dar es Salaam. Hivi karibuni watumiaji wa mtandao wa Whatsapp watarajie kuwa na uwezo wa kutumia  zaidi ya namba moja ya simu kwenye programu moja ya ikiwa majaribio yanayofanyika hivi sasa yatatoa matokeo chanya.

Awali ilikuwa ni aidha  mtumiaji atumie kifaa kingine kusajili akaunti kwa namba nyingine au atumie toleo jingine la WhatsApp kama WhatsApp Business.

Mabadiliko hayo yanalenga kuwaondolea adha watumiaji wa mtandao huo ya kulazimika kuwa zaidi ya programu au  kifaa kimoja cha mawasiliano ili awe na akaunti mbili za WhatsApp.

Taarifa iliyochapishwa na mtandao WhatsApp beta Agosti 10, 2023 inabainisha kuwa kwa sasa mabadiliko hayo yanapatikana kwa baadhi ya watumiaji wa tovuti hiyo ya majaribio toleo la Android 2.23.17.8.

Mtandao wa WhatsApp hutumia WhatsApp beta kama sehemu ya majaribio ya maboresho inayokusudia kuyafanya, ili kujiridhisha na utendaji kazi wake kabla haijaidhinishwa kutumika kwenye programu kuu.

Hata hivyo watumiaji wa WhatsApp beta wanaweza kuwasiliana na wale wa WhatsApp ya kawaida ingawa wao huwa na uwezo wa kujaribu vitu vipya pale vinapotambulishwa kwa mara ya kwanza.

Mwonekano wa skrini ukionesha jinsi ya kuongeza akaunti nyingine ya ziada. Picha na WABetaInfo

Namna ya kuongeza akaunti mpya

Sasa kama wewe ni mtumiaji wa WhatsApp beta na unataka kuongeza akaunti mpya unachotakiwa kufanya ni kwenda sehemu ya mpangilio (settings) kisha bofya alama ya mshale unaoelekea chini.

Hapo utaona sehemu inayokuruhusu kuongeza akaunti ambapo kwanza utajaza namba, kisha taarifa nyingine kama jina na picha.

Baada ya kuongeza akaunti mpya, itabaki kwenye kifaa mpaka mtumiaji atakapochagua kutoka, kupitia hatua hiyohiyo pia, unaweza kubadilisha akaunti au kuziunganisha.


Soma zaidi


‘Sticker’ za akili bandia

Katika hatua nyingine WhatsApp inatarajia kuongeza  kipengele cha sticker (vibandiko) vya akili bandia ‘AI stickers’ ambapo watumiaji wanaweza kuziunda kwa kuandika maelezo ya muonekano wanaotaka na kuitumia kwenye mazungumzo yao.

Stickers hutumika kunogesha mawasiliano kati ya wahusika na wakati mwingine hutumika kama mbadala wa emoji.

Licha ya kwamba kipengele hiki kipo kwenye majaribio ya awali, kinatarajiwa kuongezwa kwenye mitandao mingine inayomilikiwa na kampuni ya Meta yaani Instagram na Facebook Messenger.

Hivi ndivyo skrini inayowezesha mtumiaji kuunda sticker kwa kubonyeza kitufe cha ‘Create’ inavyoonekana. Picha na WABetaInfo

Hatua zaidi za kuboresha faragha

Ili kukabili wasiwasi unaokua kuhusu faragha ya data za watumiaji, WhatsApp imezingatia kuimarisha udhibiti wa watumiaji wake, watumiaji watapewa uwezo wa kuwasiliana  bila kuacha alama yoyote ya kidijitali, kama vile uthibitisho wa kusomwa au ishara za kuandika ujumbe.

Kipengele hiki kinawawezesha watumiaji wa programu hiyo kuchagua wakati na jinsi wanavyoweza kuficha au kufichua uwepo wao mtandaoni, hivyo kuongeza udhibiti wao wa alama za kidijitali.

Related Post