Wateja wa benki ya FMBE wapigwa tena kalenda malipo yao

Daniel Samson 0446Hrs   Mei 13, 2019 Biashara
  • Serikali imesema haijulikani ni lini zoezi la ugawanyi wa fedha za ufilisi wa benki hiyo litaanza kutokana na kuwepo kwa kesi mahakamani.
  • Kesi hiyo imefunguliwa na nchi ya Cyprus ambayo inataka iwalipe wateja wa FBME na siyo Serikali ya Tanzania. 
  • Benki hiyo ilifungwa mwaka 2017 kutokana na changamoto za mtaji wa uendeshaji.

Dar es Salaam. Huenda waliokuwa wateja wa benki ya FMBE wakaendelea kusubiri kwa muda mrefu kupata fedha zao baada ya Serikali kusema haijulikani ni lini zoezi la ugawanyi wa fedha za ufilisi wa benki hiyo litaanza kutokana na kuwepo kwa kesi zinazokwamisha mchakato wa ukusanyaji madeni na mali za benki hiyo.

May 8, 2017 Benki ya FMBE ilinyang’anywa leseni na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ambayo ni mlezi benki nchini kutokana na kushindwa kujiendesha na changamoto za mtaji. 

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Ashatu Kijaji ametoa ufafanuzi huo leo (Mei 13, 2019) bungeni wakati akijibu swali la Mbunge Asha Abdula ambaye alitaka kujua Serikali imechukua hatua gani kuwalipa fidia wananchi walioweka amana zao katika benki ya FBME. 

“Tarehe ya kuanza ugawaji wa fedha zinazotokana na ufilisi haijulikani kwa sasa kutokana na uwepo wa kesi zinazokwamisha zoezi la ukusanyaji mali na madeni ya FMBE,” amesema Dk Kijaji.

Amebainisha kuwa Benki Kuu ya Cyprus ndiyo imefungua kesi hiyo kwa madai kuwa inawajibika kulipa madeni ya wateja wote wa benki ya FBME na siyo Serikali ya Tanzania. 

“Aidha, zoezi la kukusanya mali na fedha zilizokuwa zimewekezwa na benki ya FBME katika taasisi mbalimbali hususan nje ya nchi imekumbwa na changamoto za kisheria kati ya Tanzania na nchi ya Cyprus ambako benki ya FBME ilikuwa na tawi ambalo lilikuwa linaendesha sehemu kubwa ya biashara zake na kusababisha ucheleweshaji wa ukusanyaji na ugawaji wa fedha za ufilisi,” amefafanua Dk Kijaji. 

Hata hivyo, amesema Serikali kupitia Bodi ya bima ya amana, Benki Kuu ya Tanzania pamoja na ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali iko katika mazungumzo na Serikali ya Cyprus ili kulipatia suala hilo ufumbuzi.


Zinazohusiana: 


Baada ya Kijaji kujibu swali hilo, aliinuka Mbunge na Mtama, Nape Nnauye ambapo amesema kwanini Serikali isiwalipe wateja wa benki hiyo kisha iendelee na michakato mingine ya ufilisi ili kuwapa fursa kuendelea na shughuli za uzalishaji mali.

Wakati akijibu swali hilo la nyongeza, Dk Kijaji amesema ulipaji wa fedha za ufilisi lazima ufuate mchakato wa kisheria uliopo.

Amesema kwa mujibu wa Sheria ya Mabenki na taasisi za Fedha ya mwaka 2006 kifungu cha 39, kifungu kidogo cha II na III, amana au akiba ya wateja katika benki au taasisi ya fedha zina kinga ya bima ya amana kiasi kisichozidi Sh1.5 milioni tu na endapo mteja ana salio la amana kilichozidi Sh1.5 milioni atapata fidia ya asilimia 100.

Wateja walio na amana zaidi ya Sh1.5 milioni wanalipwa Sh1.5 milioni kama fidia ya bima ya amana na kiasi kilichobakia kinalipwa kwa mujibu wa sheria na taratibu za ufilisi.

Benki ya FBME tawi la Tanzania iliyofungwa tangu mwaka 2017. Picha|Mtandao.


Kufilisika kwa benki ya FBME

Uamuzi wa Benki Kuu kuifungia benki hiyo ulitokana na notisi iliyotolewa July 15 2014 na Taasisi ya Marekani inayopambana na uhalifu wa kifedha “the US Financial Crimes Enforcement Network”(FinCEN), iliyoituhumu FBME kuwa ni taasisi inayojihusisha na biashara ya utakatishaji wa fedha haramu (money laundering) na hatua ya Benki Kuu ya Cyprus kuliweka tawi la FBME lililopo nchini Cyprus chini ya uangalizi maalumu (special administration).

FBME walifungua kesi huko Marekani (US District Court for the District of Columbia) wakiiomba Mahakama kutengua uamuzi wa FinCEN ambapo hatimaye April 14 2017 Mahakama ilitoa uamuzi ambao unairuhusu FinCEN kuendelea na utekelezaji wa uamuzi wake wa mwisho (Final Rule) ambao unaifungia benki ya FBME kutumia mfumo wa kibenki wa Marekani.

Uamuzi huo wa Mahakama unaongeza athari kwa kiwango kikubwa katika uendeshaji wa FBME kwa kuwa haitaweza tena kufanya miamala ya kibenki ya kimataifa na kupata huduma za mifumo ya kibenki na hivyo itashindwa kutoa huduma muhimu kwa wateja wake kwa mujibu wa leseni waliyopewa.

“Benki Kuu ya Tanzania imesimamisha shughuli zote za FBME Bank Limited kufuta leseni yake ya kufanya shughuli za kibenki, kuiweka chini ya ufilisi na kuiteua Bodi ya Bima ya Amana (DIB) kama mfilisi kuanzia tarehe 8 Mwezi Mei, 2017,” inasomeka taarifa ya BoT kuifutia leseni FBME iliyotolewa Mei 8 mwaka 2017.

Related Post