Nsekela ateuliwa na CRDB kurithi mikoba ya Dk Kimei

Rodgers George 0528Hrs   Septemba 20, 2018 Habari
  • Bosi huyo mpya wa CRDB ana uzoefu wa miaka 20 akiwa amebobea katika masuala ya kimataifa ya kibenki na fedha.
  • Atakuwa na kibarua kigumu cha kuendeleza kazi nzuri iliyofanywa na Dk Kimei kwa takribani miaka 20

Dar es Salaam. Hatimaye Benki ya CRDB imemteua Abdulmajid Nsekela kuwa Mkurugenzi Mtendaji mpya wa benki hiyo akichukia nafasi ya Dk Charles Kimei ambaye atastaafu Mei, 2019 baada ya kuitumikia benki hiyo kwa miaka 20. 

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa umma, kabla ya kushika nafasi hiyo Nsekela alikuwa Kaimu Mkuu wa Huduma za Rejareja za kibenki katika benki ya NMB na alishika nafasi hiyo tangu mwaka 2015. 

Mchakato wa kumpata mrithi wa Dk Kimei, ulianza tangu Disemba 28, 2017 kufuatia kukaribia kwa muda wake wa kustaafu kwa mujibu wa sheria ambapo Bodi ya Wakurugenzi ya Benki ya CRDB iliunda kamati maalum iliyosimamia zoezi hilo na kufanikiwa kumpata Nsekela.

Nsekela ni msomi mwenye shahada ya uzamili ya Usimamizi wa Biashara (MBA-IBF) akiwa amebobea katika masuala ya kimataifa ya kibenki na fedha. 

Pia ana Stashahada ya Usimamizi wa Biashara aliyosomea katika Chuo Kikuu Cha Birmingham nchini Uingereza pamoja na Stashahada ya juu ya masuala ya kibenki kutoka Taasisi ya Usimamizi wa Fedha (IFM). Ana uzoefu wa zaidi ya miaka 20 katika huduma za rejareja za kibenki na huduma mbalimbali za kibenki. 


Zinazohusiana: 


Safari yake ilianzia CRDB mnamo mwaka 1997 kama Afisa wa benki baadaye mwaka 1998 alichaguliwa kuwa sehemu ya timu ya mpito ambayo ilibadili utendaji wa CRDB.

Mwaka 2000 Nsekela alipandishwa cheo na kuwa Meneja Uhusiano ambapo aliunda timu madhubuti ambayo ilianzisha na kuendeleza idara ya sasa ya kibishara ya makampuni (Corporate Banking Department) katika benki hiyo.

Kufuatia mafanikio yake makubwa ndani ya CRDB, mwaka 2003 alipandishwa tena cheo na kuwa Meneja Mkuu wa Uhusiano (Senior Relationship Manager)

Mwaka 2008 Nsekela alijiunga na Benki ya NMB PLC kama Meneja Mkuu (Personal Banking) kabla ya kupandishwa cheo na kuwa Mkuu wa Idara hiyo mwaka 2013. Desemba mwaka 2015 aliteuliwa kuwa Mkuu Biashara (Business Head Retail).

Baada ya hapo alijiunga tena na Benki ya CRDB ambapo alifanya kazi kubwa katika kuleta mabadiliko katika miundombinu ya mauzo na kukuwa kwa mtandao wa matawi ya benki hiyo. 

Kwa namna nyingi Nsekela aliwajibika kwa kufanya mabadiliko kwenye sekta ya kibenki Tanzania. Amesimamia miradi mbalimbali ya kibenki na kusaidia maendeleo lukuki katika benki mbili za Tanzania yaani CRDB na NMB kwa nyakati tofauti.

Mkurugenzi Mtendaji mpya wa CRDB, Abdulmajid Nsekela (kushoto) katika moja ya mikutano na Wanahabari wakati akiwa NMB. Pembeni yake ni Ofisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Bibi Ineke Bussemaker.

Kwa upande wake, Dk Kimea ambaye amehudumu katika nafasi hiyo tangu 1998 ikiwa ni miaka 20 ametoa mchango mkubwa katika mafanikio ya CRDB tangu kuanzishwa kwake mwaka .

Kwa mujibu wa CRDB, katika kipindi chake cha uongozi kama Mkurugenzi Mtendaji, Benki ya CRDB imefanikwa kupiga hatua kubwa ikiwemo kukua kwa faida kutoka Sh2 bilioni mwaka 1998 hadi kufikia Sh108 bilioni mwaka 2016.

Pia rasilimali za benki zikikua kutoka Sh54 bilioni hadi kufikia Sh5.3 trilioni mwaka 2016. Pia mtandao wa matawi umekua kutoka matawi 19 mwaka 1998 hadi matawi 262 mwaka 2017.  Pia amefanikiwa katika ufunguaji wa kampuni tanzu nchini Burundi (CRDB Bank Burundi Ltd) pamoja na kampuni tanzu za CRDB Bank Microfinance Ltd na CRDB Bank Insurance Ltd ambazo zote zinafanyakazi chini ya mwamvuli wa kampuni mama ya CRDB Bank PLC.

Bila shaka Nsekela atakuwa na kibarua kigumu kuimarisha utendaji wa benki hiyo ili iendelee kutoa ushindani katika sekta ya fedha nchini.


Related Post