Wamachinga, wajasirimali waeleza Magufuli alivyowainua Mwanza

Mariam John 0114Hrs   Machi 19, 2021 Biashara
  • Wamesema aliwapa uhuru wa kuendesha biashara zao bila kusumbuliwa.
  • Aliwasaidia kupata vitambulisho vya ujasiriamali.
  • Wamesema watamkumbuka kwa utetezi wake kwa wanyonge. 

Mwanza. Baadhi ya wamachinga na wajasirimali Jijini Mwanza wameeleza hofu yao kuwa hawajui nini kitatokea kuhusu uhuru wa kufanya biashara baada ya kifo cha mtetezi wao Hayati Rais John Magufuli aliyeaga dunia Machi 17, 2021 mkoani Dar es Salaam. 

Magufuli (61) aliyefariki katika hospitali ya Mzena mkoani hapa kwa maradhi ya moyo anatarajiwa kuzikwa wilayani Chato katika mkoa wa Geita. 

Mwenyekiti wa Shirikisho la Umoja wa Machinga Tanzania (Shiuma), Ernest Matondo amesema kifo cha Dk Magufuli kimewaondolea wamachinga  ushujaa. 

Matondo ametaja uhuru na fursa ya kufanya shughuli zao bila bughudha kutoka mamlaka za halmashauri na vitambulisho vya wamachinga kuwa miongoni mwa mambo ambayo kundi hilo litamkumbuka. 

“Kabla ya Rais Magufuli hajaingia madarakani wamachinga hawakuwa na uhakika wa kesho yao; kulikuwa na operesheni za mara kwa mara za kuwaondoa mitaani iliyoambatana na kunyang’anywa au kuharibiwa mali zao. Yote hayo yalikoma chini ya uongozi wa Rais Magufuli,” amesema Matondo.

Ameeleza  kuwa wamachinga walikuwa wanatozwa ushuru wa kati ya Sh200 hadi Sh500 kwa siku na baada ya Magufuli kuingia madarakani sasa wanalipa Sh20,000 pekee kwa mwaka kwa ajili ya vitambulisho vya wamachinga na kufanya biashara popote.

Kauli ya kumbukumbu njema ya Rais Magufuli kwa wamachinga pia imetolewa na Joshua Kajala, mfanyabiashara mdogo katika mtaa wa Makoroboi jijini Mwanza anayesema kiongozi huyo alijenga msingi uliowalazimisha viongozi na watendaji wa Serikali kuwasikiliza na kutatua kero za wanyonge.

“Yeye binafsi alitoa nafasi kwa wananchi kueleza kero zao wakati wa ziara zake na mara nyingi alionyesha kukerwa alipobaini baadhi ya kero zingeweza kutatuliwa na viongozi wa chini,” amesema Kajala.


Soma zaidi:


Mfanyabiashara jijini hapa, Asha Amir bado ana kumbukumbu ya kiongozi huyo mkuu wa nchi ya kuwakemea papo kwa papo wasaidizi wake ambao hawakuwajibika kuboresha huduma za kijamii huku akiwataka waende kwa wananchi kutatua kero zao. 

Anasema hiyo iliwapata heshima hasa wafanyabiashara wadogo kupata suluhu ya changamoto katika maeneo yao. 

Mara kadhaa katika mikutano ya hadhara na ya kisiasa, Hayati Dk Magufuli amekuwa akisema yeye ni mtetezi wa wanyonge hasa wananchi masikini na amejitoa kwa ajili yao. 

Kauli kama hizo zimekuwa zikiwapa imani na nguvu, wamachinga kuendesha shughuli zao wakijua yupo kiongozi anayelinda maslai yao hata kama watakutana na changamoto. 

Katibu wa wafanyabiashara vijana katika soko la Makoroboi jijini hapa, Joseph Charles amewaomba viongozi wa Serikali kuendeleza yote mema yaliyoasisiwa na kusimamiwa na Rais Magufuli kama njia ya kumuenzi.

Related Post