Wahitimu vyuo vikuu wakumbushwa kuchangamkia fedha za halmashauri

Daniel Samson 0240Hrs   Disemba 15, 2018 Biashara
  • Ni fedha za asilimia tano zinazotengwa katika maeneo ya kila mwaka ili kuwawezesha vijana na wanawake kiuchumi.
  • Ni utaratibu wa Halmashauri zote nchini hutenga asilimia tano ya mapato yake ya ndani kila mwaka ili kuwawezesha vijana na wanawake.

Dar es Salaam. Wahitimu wa vyuo mbalimbali nchini wamepewa changamoto ya kutumia fursa ya uwepo wa fedha zinazotengwa na Halmashauri katika Wilaya zote nchini kila mwaka kuanzisha miradi ya kiuchumi ili kujikwamua kimaisha.

Halmashauri zote nchini hutenga asilimia tano ya mapato yake ya ndani kila mwaka ili kuwawezesha vijana na wanawake kutumia fedha hizo kwa ajili ya shughuli mbalimbali za kiuchumi ili kujikwamua kimaisha na kuchangia katika ukuaji wa pato la Taifa.  

Akihutubia wakati wa mahafali ya 32 ya Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini (IRDP) jijini Mwanza, Naibu Katibu Mkuu wizara ya Fedha na Mipango Dk Khatibu Kazungu, amewataka wahitimu wa vyuo ambao hawana ajira katika sekta rasmi waanzishe  na kujiunga katika vikundi vya uzalishaji mali ikiwa ni moja ya kigezo cha kuweza kupata fedha hizo.

“Serikali ya awamu ya tano imejidhatiti kuwaletea wananchi maendeleo endelevu kwa kuhakikisha kila mtu kwa nafasi yake anafanya kazi kwa uzalendo, uadilifu, bidii na maarifa lakini pia kudumisha amani na mshikamano ili kuwa na maendeleo endelevu kwa manufaa ya kizazi hiki na  kijacho.”amesema Dk Kazungu.

Taarifa iliyotolewa na kitengo cha mawasiliano katika wizara hiyo, imeeleza kuwa wahitimu hao pia wametakiwa kuchangamkia fursa ya mtengamano wa Afrika Mashariki kwa kupata ajira si tu ndani ya nchi na hata nje ya nchi kwa kuwa wahitimu hao wamebahatika kuwa na elimu yenye ubora inayoweza kuingia katika ushindani wa soko la ajira.


Zinazohusiana: Mambo ya kuzingatia unapoanzisha brand yako ya biashara

                           Acha kuwaza kuwa mfanyabiashara, anza kufanya biashara


Kaimu Mkuu wa Chuo cha IRDP, Prof. Hozen Mayaya, ameishukuru Serikali kwa kufanya maboresho katika sekta ya huduma za jamii ikiwemo elimu ambayo imewezesha taasisi  za elimu ya juu kuwa sehemu bora ya kujifunzia.

Amesema tangu kuanzishwa kwa chuo hicho miaka 39 iliyopita, hakijaacha kusimamia ubora wa elimu kwa kuzingatia miongozo na kanuni zilizowekwa na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE).

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Dk Khatib Kazungu, ambaye alikuwa mgeni rasmi katika mahafali ya 32 ya Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini (IRDP) Kanda ya Ziwa Jijini Mwanza, amewataka wahitimu hao   kuchangamkia fursa zilizopo katika  mtengamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kupata ajira kwa kuwa wanavigezo vya ushindani wa ndani na nje ya nchi. Picha| Josephine Majura.

Mkurugenzi wa Chuo cha IRDP Kanda ya Ziwa Dkt. Benedict Kilobe, amesema kuwa mahafali hayo yamefanyika kwa mara ya sita katika kituo cha Mwanza, ambapo wanafunzi 1,203 wamehitimu mafunzo ya programu mbalimbali zinazotolewa na chuo hicho wakiwemo wanaume 519 sawa na asilimia 43.1 na Wanawake 684.

Mahafali ya 32 ya Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini (IRDP) Kanda ya Ziwa yalihusisha wahitimu wa ngazi ya Astashahada, Stashahada na Stashahada za Uzamili ambao walipata mafunzo kwa vitendo katika maeneo mbalimbali nchini ambayo yatawafanya kuwa chachu ya mabadiliko katika vituo vya kazi.

Naye Kaimu Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chuo hicho, Mugage Mtani amesema mafanikio ya chuo hicho yametokana na ushirikiano wa wadau mbalimbali ikiwa pamoja na Serikali kuu, mamlaka ya serikali za mitaa, asasi zisizo za Serikali, taasisi za mafunzo ndani na nje ya nchi na Shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) - Malawi na Tanzania.

Related Post