Viongozi, jumuiya za kimataifa wazungumzia watakavyomkumbuka Rais Magufuli

Daniel Samson 0428Hrs   Machi 18, 2021 Habari
  • Wamemtaja kama kiongozi shupavu aliyependa maendeleo ya Afrika.
  • Wataka mchango na kazi nzuri alizofanya ziendelezwe.
  • Watuma salamu za pole kwa familia, Watanzania na Serikali. 

Dar es Salaam. Viongozi mbalimbali duniani na jumuiya za kimataifa zimetoa salamu za rambirambi kufuatia kifo cha Rais John Magufuli kilichotokea Machi 17, 2021 katika Hospitali ya Mzena jijini Dar es Salaam alikokuwa akipatiwa matibabu.

Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan ametangaza kifo cha Rais Magufuli kimetokana na tatizo la moyo la mfumo wa umeme ambalo alikuwa nalo kwa zaidi ya miaka 10.

                 

Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta ametoa salamu za Taifa lake kufuatia kifo cha Magufuli huku akisema Tanzania imempoteza kiongozi muhimu kwa maendeleo.

“Nimempoteza rafiki wa karibu. Natoa pole kwa mama Janet, watoto na Taifa zima,” amesema Rais Kenyatta katika salamu zake zilizotangaza na kituo cha televisheni cha KTN.

Rais Kenyatta ambaye ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ambayo Tanzania ni mwanachama ametangaza siku saba za maombolezo na ameagiza bendera za nchi hiyo ikiwemo ya EAC kupepea nusu mlingoti.

Dk Magufuli ambaye alikuwa Rais wa awamu ya tano anakuwa kiongozi mkuu wa nchi wa kwanza kufariki akiwa madarakani nchini Tanzania. 

Naye Waziri Mkuu wa Uingereza, Borris Johnson ameandika katika ukurasa wake wa Twitter kuwa “Nasikitika kupata taarifa ya kifo cha Rais wa Tanzania, John Magufuli. Natoa salamu zangu kwa familia na watu wa Tanzania.”

Kutokana na kifo cha Rais Magufuli aliyefariki akiwa na umri wa miaka 61, Serikali imetangaza siku 14 za maombolezo ya kitaifa ambapo bendera zote zitapepea nusu mlingoti.

Viongozi wengine walioguswa na msiba huo ni Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa ambapo kupitia ukurasa wake wa Twitter amesema kuwa nchi ya Afrika Kusini inaungana na Serikali na Watanzania wote katika kuomboleza kifo cha Dk Magufuli.

“Nimezungumza na Makamu wa Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kutoa salamu zangu za pole katika kipindi hiki kigumu wanachopitia,” ameandika Ramaphosa.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP), Joyce Msuya amesema ni pigo kwa Taifa na Watanzania kumpoteza Hayati Rais Magufuli. 

“Ni wakati wa kuungana na kuwa pamoja. Kwa niaba ya @UNEP, naungana na ndugu, marafiki, na Watanzania wenzangu kumuomboleza,” amesema Msuya katika ukurasa wake wa Twitter. 


Kiongozi wa upinzani Kenya, Raila Odinga

Kiongozi wa upinzani nchini Kenya, Raila Odinga amesema kuwa Rais Magufuli alikuwa rafiki yake wa karibu na alimuonyesha ushirikiano mkubwa katika kipindi alichohitaji msaada wake.

“Nimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha Rais John Magufuli, yeye na familia yake walikuwa ni watu wa karibu kwa kipindi kirefu. Rais Magufuli amekuwa nami katika vipindi vigumu kwenye maisha yangu, ninatoa pole kwa familia na Watanzania kwa ujumla,” ameandika Odinga katika ukurasa wake wa Twitter. 


Soma zaidi


Rais Museveni wa Uganda atoa salamu

“Nimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya kifo cha Rais John Magufuli,” ameandika Rais wa Uganda, Yoweri Museveni katika ukurasa wake wa Twitter na kubainisha kuwa alikuwa kiongozi imara ambaye aliamini na kutenda ili kukuza uchumi wa Afrika Mashariki. 

Amesema nchi yake inaungana na Watanzania katika kipindi hiki kigumu ambacho Taifa limempoteza kiongozi wa nchi. 

Naye Rais wa Benki ya Maendeleo ya Africa (AfDB), Akwinumi Adesina amemtaja Dk Magufuli kama kiongozi makini ambaye alijitoa bila kuchoka kuboresha maisha ya Watanzania na kujenga uchumi imara wa Tanzania.

“Nitakukumbuka sana, hamasa yako katika maendeleo ya Afrika,” ameandika Adesina katika ukurasa wake wa Twitter. 

Related Post