Ulaji mzuri wa vyakula vya wanga unavyoimarisha afya ya mwili

July 25, 2020 7:01 am · Joshua
Share
Tweet
Copy Link
  • Ikiwa kazi zako zinahusisha nguvu sana basi ulaji wa wanga wa kutosha ni muhimu kwa afya yako.
  • Kama unafanya kazi za ofisini na kukaa zaidi, tumia vitamini na protini zaidi kuliko wanga. 
  • Usipozingatia ulaji mzuri wa wanga unajiweka katika hatari ya kupata magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo kisukari na shinikizo la juu la damu. 

Tunapoongelea wanga tunagusia aina ya vyakula ambavyo kila siku ni lazima tuvitumie. Vyakula vya wanga ni aina ya vyakula ambavyo huupa mwili nguvu yaani ni vile vyakula ambavyo mwili huvichakata na mwishoe kuupatia nishati. 

Kwa lugha iliyozoeleka ya kigeni, hivi ni vyakula vya “Carbohydrate”. Mfano wa vyakula hivi ni ngano na bidhaa zake zote, mahindi, ulezi, mtama, mchele nk. 

Hivi navyo huweza kuwa vile vilivyokobolewa ama visivyokobolewa na hutofautiana kwa kiwango cha madini na virutubisho. 

Wanga huwa na virutubisho ambavyo huingizwa ndani ya mwili na kuvunjwa vunjwa na hatimae kupata glucose (sukari). Mwili huihitaji glucose hii ili uweze kujizalishia nishati ya kuweza kuziwezesha seli zake kufanya kazi kwa ufasaha. 

Matumizi ya nishati hutegemeana sana na mahitaji ya mwili. Nishati ya msingi kwa ajili ya uendeshaji wa shughuli za mwili peke yake huwa katika kiwango cha kawaida ambacho mwili huwa umekiweka. 

Nani anapaswa kula vyakula vyenye wanga?

Lakini matumizi ya nishati ya ziada hutegemeana sana na aina ya shughuli ambazo mwili huo hufanya yaani mwili wa mtu husika.

Mtu anayefanya kazi zinazohitaji nguvu kubwa ya misuli yaani kazi za shurba kidogo huhitaji kiwango kikubwa zaidi cha nishati ya nguvu ili kuiwezesha misuli yake kufanya kazi. 

Mtu ambaye hufanya kazi za mezani au kazi zisizohitaji matumizi makubwa ya nguvu za misuli zaidi anahitaji kiwango cha wastani tu cha glucose kwa ajili ya mwili wake kufanya kazi. 

Usipokuwa makini katika ulaji wa vyakula vya wanga unaweza kupata matatizo ya kiafya. Picha| Mtandao.

Kwa misingi hiyo, ulaji wa wanga unapaswa kuendana na aina za kazi tunazofanya na namna tunavyofanya. Kwanini?

Mwili una tabia ya kutunza kile kinachobaki na kuwa na hazina kwa matumizi ya muda mwingine na matumizi ya dharula. Na hii ndiyo sababu kuna kiwango cha muda ambacho mwili waweza kukaa bila kula. 

Utunzaji huu wa hazina ya mwili hukuwezesha kuhimili nyakati ngumu na kuupa mwli nafasi ya kujiimarisha.

Katika utunzaji wa glucose, mwili hutunza nishati hii katika ini. Inapotokea uhitaji wa glucose mwilini wa dharula au wa ziada, mwili hufungulia glucose hii iliyotunzwa kwa mfumo wa “glycogen” na kuuchakata kupata glucose kisha kuupatia mwili nishati ya nguvu unayoihitaji. 

Iwapo kiwango cha glucose kinazidi hazina inayopaswa kutunzwa, basi haiwezi kutunzwa katika mfumo wa glucose tena bali mfumo wa mafuta ambao mwili huweza kutunza kwa kiwango kikubwa na urahisi zaidi. 

Kisha hutunzwa katika tissue mafuta au “adipose tissue” na kuwekwa katika maeneo tofauti  ya mwili kulingana na maumbile mfano makalio, mikono, mapaja, kifua na tumbo. Kiwango kikizidi hulazimika kutunzwa katika ogani za mwili kisha mishipa ambayo huongeza hatari za magonjwa ya moyo.

Watu wengi hujizuia ulaji wa vyakula vyenye mafuta na kusahau ulaji wa wanga ambao kwa kiasi kikubwa huchangia uwepo wa mafuta yaliyozidi ndani ya miili yao. 

Ikiwa kazi zako zinahusisha nguvu sana basi ulaji wa wanga wa kutosha ni muhimu kwa afya yako.


Zinazohusiana:


Wanga kwa wasiofanya kazi nguvu

Lakini iwapo wewe ni mtu wa kazi za kiofisi zaidi na hutumia muda mwingi ukiwa umekaa basi zingatia ufanyaji wa kazi zako katika mfumo wa lishe bora kwa sababu  unahitaji kiwango kidogo cha wanga kwa ajili ya ufanisi wa utendaji kazi wa mwili wako. 

Pangilia mlo wako kwa kuongeza zaidi vitamini na protini na wanga kidogo zaidi katika mlo wako wa siku nzima. Mfano unaweza kutumia chai na chapati asubuhi kisha kutumia matunda zaidi mchana na mboga mboga. Jioni pata chakula laini  na bado mwili wako ukawa na nguvu ya kujitosheleza.

Ni vizuri pia iwapo ukawa mdau mzuri wa matumizi ya nafaka zisizokobolewa dhidi ya zile zilizokobolewa. Mfano unga wa muhogo au mahindi yasiyokobolewa, ngano nk. Hii hukupatia virutubisho zaidi ya vile katika nafaka zilizokobolewa. 

Kutambua hili kutakuwezesha wewe kuwa na afya bora na kupunguza hatari ya magonjwa yaendanayo na mtindo wa maisha ikiwemo kisukari na shinikizo la juu la damu. Ni matumaini yangu sasa umeelewa namna wanga unavoweza kutumika katika mwili wako.

Dk Joshua Lameck Sultan ambaye kitaaluma ni daktari wa mafunzo ya mazoezi tiba ni Mshauri katika taasisi ya Nakua na Taifa Langu (NTL) na Mkurugenzi wa Indigo Afya. Hufanya semina mbalimbali kuhusu masuala ya afya akijikita katika magonjwa yasiyoambukiza (NCD) pamoja na yale yanayoendana na mtindo maisha. Anapatikana kwa namba: +255 789 311 481, Baruapepe: joshualameck9@gmail.com.

Enable Notifications OK No thanks