Unakunywa gongo, chang’aa au kachasu? Fahamu uhusiano wake na saratani
- Zinachangia kwa kiasi kikubwa saratani ya tumbo.
- Mwaka 2020 saratani ya tumbo ilisababisha vifo vya watu 544,076 duniani kote.
- Watafiti washauri watu kuacha kunywa pombe hizo kali.
Dar es Salaam. Matumizi ya baadhi ya pombe za kienyeji ikiwemo gongo ambayo kwa Tanzania ni haramu ni miongoni mwa vichocheo vikubwa saratani mbalimbali ambazo zimekuwa zikigharimu maisha ya maelfu ya watu katika nchi za Afrika.
Utafiti mpya uliofanywa na wanasayansi wa Shirika la Kimataifa la Utafiti wa Saratani (IARC) wakishirikia na watafiti kutoka Kenya, Tanzania na Malawi umebaini pombe ni kinywaji hatarishi na kichocheo cha saratani ya tumbo hususan miongoni mwa wanaume.
Ripoti ya utafiti huo uliochapishwa katika jarida la kitabibu la Lancet imetaja aina ya pombe kuwa ni zile kali za kisasa na zinazotengenezwa kienyeji kama vile gongo nchini Tanzania, Chang’aa nchini Kenya na Kachasu nchini Malawi.
Wanasayansi hao kutoka IARC, Chuo Kikuu cha Moi nchini Kenya, Taasisi ya utafiti wa Tiba Kilimanjaro nchini Tanzania na Chuo cha Tiba cha Malawi wamesema saratani ya tumbo inaweza kuzuilika kwa kuacha pombe hizo kali.
“hadi sasa mchango wa unywaji pombe katika saratani ya tumbo katika ukanda wa Afrika Mashariki hauko bayana, miongoni mwa sababu ikiwa ni ugumu wa kutambua wigo wa vinywaji vya kienyeji na vya kisasa kwenye ukanda huo,” amesema Mkuu wa utafiti huo Dk Valerie McComack kutoka IARC.
Kwa mantiki hiyo anasema utafiti huo mpya unazingatia kwa mapana unywaji wa pombe za kienyeji na unaonesha dhahiri mzigo wa saratani ya tumbo unaweza kupunguzwa Afrika Mashariki kwa kupunguza unywaji wa pombe.
Soma zaidi:
-
Pombe yatajwa kusababisha wagonjwa wapya wa saratani zaidi 700,000
-
Tabia zitakazokusaidia kuepuka madhara ya unywaji wa pombe uliopitiliza
Utafiti ulihusisha uchunguzi wa tabia za unywaji kwa watu 1,279 waliokuwa wamelazwa hospitali wakiugua saratani ya tumbo na wengine 1,346 wasiougua saratani ya tumbo, na ulifanyika Malawi, Kenya na Tanzania.
Kwa kina wahusika walichunguzwa aina za pombe za kienyeji walizotumia na kubaini viwango vyao vya unywaji kama ni cha juu au cha chini na wanakunywa mara ngapi kwa wiki na kwa kiasi gani.
Watafiti walibaini uhusiano wa kina kati ya hatari ya kupata saratani ya tumbo na unywaji wa pombe na hatari ilikuwa kubwa zaidi kwa wale wanaokunywa pombe kupindukia.
Hata hivyo, utafiti zaidi unahitajika juu ya uhusiano wa pombe kali na saratani ya tumbo.
Mwaka 2020 saratani ya tumbo ilisababisha vifo vya watu 544,076 duniani kote.
Takwimu zinaonesha saratani hii ya tumbo ni nadra sana Afrika Magharibi ilhali imeshamiri Kusini na Mashariki mwa Afrika.
Kando ya pombe, sababu nyingine ni unywaji wa vitu vya moto kupindukia, matumizi ya tumbaku, na afya duni ya mdomo.
Mwaka 2020, IARC imeeleza kuwa kulikuwa na wagonjwa wapya 3,000 wa saratani ya tumbo nchini Kenya, ilhali nchini Tanzania idadi ilikuwa 2,600 na Malawi 1800.