Pombe yatajwa kusababisha wagonjwa wapya wa saratani zaidi 700,000
- Pombe imebainika kuwa kisababishi cha wagonjwa wapya 740,000 wa saratani duniani kwa mwaka 2020.
- Kati ya wagonjwa hao, wanaume ni robo tatu ya wagonjwa wote.
- Madaktari wasema kuna umuhimu kuongeza uelewa wa umma juu ya uhusiano kati ya unywaji pombe na hatari ya kupata saratani.
Dar es Salaam. Unywaji wa pombe umebainika kuwa kisababishi cha wagonjwa wapya 740,000 wa saratani duniani kwa mwaka 2020, ripoti imeeleza.
Takwimu hizo zimetolewa na Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti wa Saratani (IARC) ambayo ni taasisi tanzu ya shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani (WHO).
Kupitia chapisho la Lancet Oncology, wanasayansi wa IARC wametoa takwimu zinazoonesha kwamba ingawa mwenendo wa unywaji pombe kupindukia ambao ni sawa na zaidi ya chupa mbili kwa siku ulisababisha asilimia 86 ya wagonjwa wote wapya, unywaji wa kiwango cha kati ambao ni hadi chupa mbili kwa siku, nao pia ulisababisha zaidi ya wagonjwa wapya 100,000 wa saratani duniani kote.
Mtafiti kutoka taasisi hiyo, Harriet Rumgay amenukuliwa katika taarifa yao iliyotolewa Ufaransa Julai 14, 2021 akisema “makadirio haya yanatupatia taswira ya mzigo wa saratani utokanao na unywaji pombe, takwimu ambazo zimechambuliwa kijinsia, kinchi na kimaeneo.
Amesema wanaweza pia kupata idadi ya wagonjwa wapya wa saratani wakihusishwa na hata unywaji mdogo au wa kati wa pombe, jambo linalodhihirisha athari za pombe katika kuongeza idadi ya wagonjwa wa saratani.
Uchambuzi wa takwimu huo kijinsia unaonesha kuwa katika idadi hiyo, wanaume ni 567,000 sawa na robo tatu ya wagonjwa wote wapya.
Taasisi hiyo inasema kuwa unywaji wa pombe unaongeza hatari ya saratani katika maeneo saba ikiwemo mdomo, njia ya mfumo wa chakula, utumbo mpana na matiti kwa upande wa wanawake.
Ka mujibu wa takwimu hizo, saratani ambayo ilikuwa na wagonjwa wengi zaidi miongoni mwa ile iliyosababishwa na unywaji pombe ni saratani ya mfumo wa kupokea chakula, ikifuatiwa na ini na matiti.
Dkt. Isabelle Soerjormataram kutoka IARC, amesema unywaji pombe unaongeza kwa kiasi kikubwa mzigo wa saratani duniani.
“Lakini mara nyingi athari ya pombe kwa saratani inapuuzwa. Hii inaangazia umuhimu wa kutekeleza sera na hatua za kuongeza uelewa wa umma juu ya uhusiano kati ya unywaji pombe na hatari ya kupata saratani.”