Viongozi wa dini waitaka Serikali kudhibiti manabii, wachungaji ‘feki’

November 14, 2024 4:12 pm · Mariam John
Share
Tweet
Copy Link
  • Wasema mafundisho ya wachungaji, manabii hao huwafanya wananchi wasifanye kazi na kutegemea miujiza.
  • Waitaka Serikali kuunda chombo maalum cha kudhibiti.

Mwanza. Viongozi wa dini nchini wameiomba Serikali kuunda chombo maalum kwa ajili ya kudhibiti manabii pamoja na wachungaji wanaotoa mahubiri ya uongo ambayo yamekuwa yakipotosha waumini na kusababisha matatizo mbalimbali ikiwemo vifo.

Miaka ya hivi karibuni Tanzania imeshuhudia ongezeko la makanisa yanayohusishwa na vitendo viovu ikiwemo utapeli wa pesa na migogoro katika jamii.

Viongozi hao wametoa ombi hilo kwa Serikali katika kongamano la ‘Kiekumene’ lililofanyika leo Novemba 14, 2024 likilenga kujadili mada ya imani moja na mafundisho sahihi kwa ustawi wa mwanadamu yaliyoandaliwa na Chuo cha Biblia Kilutheri Nyakato kwa ushirikiano na Chuo cha Mtakatifu Agustino (SAUT) Mwanza.

Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania Dayosisi ya Kaskazini Magharibi Dk. Abednego Keshomshahara amesema ni vema Serikali kuhakikisha suala la usajili wa makanisa linazingatia wale waliosoma masomo ya theolojia huku akiwataka waumini kuacha kutehemea miujiza.

“Wapo waumini wanaoona kuwa kuombewa kwa kila mtumishi ndiyo maisha, utaona kila anaposikia mahubiri yeye yupo anatumia zaidi fedha katika kutafuta kuombewa anasahau kuwa Mungu mwenywe amesema aombaye upewa na siyo aombewaye hupewa,” amesema Askofu Keshomshara.

Askofu Keshomshahara amesema janga la kutegemea zaidi miujiza ni upotoshaji na kuwataka waumini kutumia muda wao kufanya shughuli za kiuchumi na kuacha kutumia muda mrefu katika kutegemea mazingaombwe na miujiza ya upotoshaji.

Viongozi mbalimali wa dini wakiwa kwenye kongamano la kiekumene kujadili mada ya imani moja mafundisho sahihi kwa ustawi wa mwanadamu. Picha|Mariam John/ Nukta

Naye Padre Dk Innocent Sanga, Mhadhiri katika chuo cha SAUT amesema kwa sasa mafundisho potoshi yamezidi kukua kwa kasi hivyo Tanzania kwa kushirikiana na dini mbalimbali inatakiwa kuweka sheria za kudhibiti usajili wa dini mpya na wachungaji kwa kufuatilia nyenendo zao.

“Kwa Mchungaji yeyote anayeanzisha dini sheria hizo zimpime katika mambo mbalimbali ikiwemo vyeti vya elimu ya theolojia, uchunguzi wa afya ya akili…

…Zifuatiliwe taarifa zao za nyuma kupitia kwa wachungaji pamoja na maaskofu wa makanisa mama wanapotokea tutadhibiti wachungaji kama wale waliosababisha vifo nchini Kenya, na wengine,”amesema Dk Sanga.

Aidha amezishauri dini kuungana na kukemea mafundisho ya uongo kwa kuunda chombo cha kukemea mahuburi yasiyo sahihi, ushauri na chombo cha dini kitakachokuwa na utaratibu wa kupima watumishi wa afya ya akili kila mara ili kudhiti mambo hasi yanayoweza kujitokeza kutokana na ugonjwa huo kwa wachungaji.

Kwa upande wake  Dk John Njoroge, Padre wa Kithodokisia kutoka Mlima wa Kenya nchini humo, ambaye pia ni Mjumbe wa Shirika la Makanisa yote Afrika, amesema kutokana na madhara ya upotoshaji kidini yaliyotokea nchini humo sheria zimeanza kuwekwa kwa lengo la kudhibiti madhara yake.

Amesema shirika hilo lilifanya utafiti mwaka 2019 na kubaini chanzo cha mahubiri potoshi kuwa yanasababishwa na wahubiri kutafuta mali pamoja na utajiri.

Enable Notifications OK No thanks