Serikali, wadau wa maendeleo wazindua kampeni ya Pika Smart

June 13, 2025 7:11 pm · Fatuma Hussein
Share
Tweet
Copy Link
  • Yalenga kuhamasisha matumizi ya kupika kwa kutumia nishati safi ya umeme
  • Ni katika kuhakikisha  asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ifikapo 2034.

Dar es Salaam. Huenda matumizi ya nishati safi ya kupikia yakapata msukumo mpya nchini Tanzania mara baada ya Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo kuzindua kampeni mpya ya Pika Smart inayolenga kuhamasisha matumizi ya kupika kwa kutumia nishati ya umeme.

Kampeni ya Pika Smart ni sehemu ya juhudi za kuongeza matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini ili kufikia lengo la asilimia 80 ya Watanzania kutumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034. 

Akizungumza katika uzinduzi wa kampeni hiyo leo Juni 13, jijini Dar es Salaam Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu kutoka Wizara ya Nishati, Mhandisi Innocent Luoga amesema kampeni hiyo inalenga kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia.

“Kampeni ya Pika Smart inalenga kufikia lengo la Serikali la kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2034, asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia,”ameeleza Luoga.

Aidha, Mhandisi Luoga ametoa wito kwa wananchi kutokuwa na hofu kuhusu matumizi ya umeme kupikia akibainisha kuwa ni salama, nafuu na rafiki wa mazingira. 

Ameongeza kuwa Tanzania kwa sasa ina uzalishaji mkubwa wa umeme, ukiwemo unaotokana na mradi wa Julius Nyerere ambao umekamilika na kuongeza uwezo wa kitaifa hadi kufikia megawati 4,031.

“Umeme huu umesambazwa hadi kufikia vijiji vyote 12,318 nchini, hivyo hakuna kisingizio tena cha kutotumia umeme kama nishati safi ya kupikia,” amesisitiza Mhandisi Luoga.

Baadhi ya wadau waliohudhuria uzinduzi wa kampeni ya Pika Smart leo. Picha/ Wizara ya Nishati.

Hata hivyo, huenda Serikali ikatakiwa kuongeza juhudi za kusambaza umeme mpaka vitongojini kwa kuwa licha ya umeme kufika vijijini bado baadhi ya maeneo hayana nishati hiyo kutokana na gharama za kuunganisha au kuwa mbali na makazi yao.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mipango na Uwekezaji wa Tanesco, Mhandisi Henryfried Byabato ameeleza kuwa shirika hilo linaendelea kuwahamasisha wananchi kutumia umeme kupikia kutokana na uwepo wa nishati hiyo kwa wingi nchini.

Mhandisi Byabato amesema kuwa teknolojia ya majiko ya umeme imeboreshwa na sasa yanatumia umeme kidogo kwa ufanisi mkubwa.

Kampeni ya Pika Smart imezinduliwa sambamba na utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Mawasiliano kuhusu nishati safi ya kupikia, ambao unatoa mwongozo kwa wadau mbalimbali kushiriki katika juhudi za kuhamasisha mabadiliko kutoka matumizi ya nishati isiyo safi kwenda nishati safi.

Kampeni hiyo imezinduliwa na Wizara ya Nishati kwa kushirikiana na Shirika la Modern Energy Cooking Services (MECS) na Shirika la Misaada la Uingereza UKAID.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks