Tumbaku inavyohatarisha maisha ya watu zaidi ya milioni 2 Tanzania

Rodgers George 0101Hrs   Julai 20, 2020 Ripoti Maalum
  • Watanzania zaidi ya 17,200 hufa kwa magonjwa yanayosababishwa na matumizi ya tumbaku kila mwaka.
  • Zao la tumbaku ni kati ya mazao yanayoingizia nchi ya Tanzania fedha nyingi katika pato la Taifa lakini ni hatari.
  • Wanaojitahidi kuacha, wanaishia njiani.

Dar es Salaam. Ni asubuhi ya saa 11, Jumanne Mtakashari (29) akiwa kwenye gari lake kuelekea kazini, anafungua moja ya droo zilizopo ndani ya gari lake na kuivuta pakti ya sigara ikiwa ni kitu cha kwanza kutia mdomoni kabla ya kifungua kinywa.

Licha ya pakti ya sigara aliloshika kuwa na maandishi "Uvutaji wa sigara ni hatari kwa afya yako, kijana huyo hajali. Jumanne, ambaye si jina lake halisi baada ya kuomba asitajwe, anaichomoa sigara moja na kuipiga kiberiti cha gesi ili apate ‘burudani’ ya asubuhi. 

Jumanne anavuta sigara yake taratibu, akipuliza moshi wake nje ambao kutokana na upepo unarudi ndani huku ukimtanda yeye na mdogo wake aliyekaa naye jirani ndani ya gari. 

“Kwenye sherehe ya mwaka mpya mwaka 2017, niliweka azimio kuwa mwaka 2016 ndio ulikuwa mwisho wa kuvuta sigara. Nilitupa sigara zangu zote,” anasema Jumanne ambaye baada ya kuivuta sigara hiyo huwa inamchukua dakika thelathini ‘kujiburudisha’ na sigara nyingine

“Mchana wa sikukuu hiyo, nilikaa ndani kwangu na kujizuia nisitoke ili nisishawishike lakini sikuweza. Ilipofika jioni, nilienda kutafuta sigara moja nikavuta na kuvunja azimio langu,” Jumanne ameiambia Nukta Habari (www.nukta.co.tz).

Jumanne ambaye azma yake ya kuacha kuvuta sigara ilimshinda ndani ya saa 12 ni kati ya watu wengi Tanzania wanaohangaika kuacha kutumia bidhaa hiyo ya tumbaku bila mafanikio. Kijana huyo kwa siku huvuta wastani wa sigara nane ambazo ni sawa na Sh60,000 kwa mwezi na Sh720,000 kwa mwaka. 

Kiwango hicho anachotumia kununua sigara kwa mwaka ni zaidi ya robo ya wastani wa pato la mtu kwa mwaka nchini Tanzania ambalo lilifikia Sh2.58 milioni mwaka 2019 kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya fedha na mipango. 

“Pakti moja inauzwa Sh5,000 na inakuwa na sigara 20. Ninawafahamu watu wanaovuta hadi pakti nne kwa siku,” ameieleza Nukta akisema tabia hiyo ya kuvuta sigara alianza nayo miaka 10 akiwa kidato cha sita na sasa anakabaliana na hali kuachana nayo. 

Matumizi ya bidhaa za tumbaku zikiwemo sigara, ni kati ya starehe ambazo ni ngumu kuacha huku yakiendelea kuathiri afya ya maelfu ya Watanzania kila siku.

Daktari kutoka kliniki ya kimataifa ya Dar es Salaam, IST clinic, Bernadette Kleczka ameiambia Nukta kuwa tumbaku ni kati ya vitu ambavyo humuwia vigumu mtumiaji wake kuacha hasa yule mwenye matumizi makubwa na ya muda mrefu.

"Tumbaku ina vitu vingi vikiwemo "nicotine". Dawa hiyo ikitumika kwa muda mrefu, inazoeleka na mtumiaji na hivyo kujikuta teja wa bidhaa ya tumbaku ikiwemo sigara," amesema Dk Kleczka.

Jumanne kwa siku huvuta wastani wa sigara nane ambazo ni sawa na Sh60,000 kwa mwezi na Sh720,000 kwa mwaka. Picha| Freepik.com.

Starehe yenye gharama

Tafiti mbalimbali zimezungumzia athari za matumizi ya bidhaa za tumbaku huku baadhi zikieleza kuwa ni moja ya vyanzo vya vifo vya watu wengi ulimwenguni. 

Utafiti wa Tumbaku kwa Watu Wazima Duniani kwa upande wa Tanzania (GATS) wa mwaka 2018 kwa upande wa Tanzania unaonyesha kuwa takriban nusu au asilimia 48.4 ya wavutaji wa sigara nchini walijaribu kuacha kutumia bidhaa za tumbaku miezi 12 kabla ya mwaka 2018 bila mafanikio.

Wakati wakihaha kuacha wapo ambao wanapoteza maisha kutokana na kutumia tumbaku hiyo ama kwa kuvuta au kunusa. 

“Kila mwaka, Watanzania zaidi ya 17,200 wanakufa kwa magonjwa yanayosababishwa na matumizi ya tumbaku.

Lakini bado watoto (miaka 10-14) zaidi ya  17,000 na watu wazima (miaka 15 na zaidi) 2.47 milioni wanaendelea kutumia bidhaa za tumbaku kila siku,” imesomeka sehemu ya ripoti ya utafiti wa GATS tolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) hivi karibuni. 

Kwa takwimu hizo za NBS kuwa zaidi ya watu 17,000 hufariki dunia kutokana na kutokana na matumizi ya tumbaku, ina maana kuwa kila siku Watanzania 47 hupoteza maisha kwa sababu tu walitumia bidhaa hiyo bila kujali afya zao. 

Watanzania hawa si tu ni idadi zilizopo kwenye takwimu bali ni baba, mama, kaka, dada zetu au wazalishaji wakuu nchini ambao walikuwa wakitegemewa na familia zao na Taifa kwa ujumla katika kukuza uchumi. 


Zinazohusiana



Ugumu wa kuacha tumbaku upo wapi?

Huenda umesikia mara nyingi juu ya tiba mbadala za kuacha matumizi ya sigara. Hata hiyo watumiaji wa  bidhaa hiyo wamesema kuacha kutumia bidhaa hizo “si rahisi kama inavyodhaniwa”.

“Niliwahi kwenda Kariakoo kuulizia dawa nikaambiwa dozi moja ni Sh160,000,” amesema Seba Paul mkazi wa Tabata Kimanga, Dar es Salaam ambaye amevuta bidhaa za tumbaku kwa zaidi ya miaka mitano na majaribio ya kuacha yameshindikana. 

“Wapo waliotumia dawa wakaacha lakini baada ya muda wakarudi kundini. Upweke, mawazo na mazowea ni sababu kuu ya kushindwa kuacha,” anasema Paul ambaye kumaliza pakiti mbili za bidhaa hiyo kwa siku ni jambo la kawaida kabisa.

Kulizungumzia jambo hilo kitaalamu, Dk Kleczka amesema, nicotine ambayo ipo kwenye bidhaa za tumbaku, husisimua mtumiaji wake kwa muda mfupi na hivyo kumfanya awe makini na kitu anachokifanya kwa wakati huo. Kwa kizungu inaitwa “Concentration”.

Naye Jumanne amesema, katika uvutaji wake wa sigara imekuwa ikimuongezea hali ya kujiamini na hivyo kumfanya kuitumia kila mara anapohitaji kujiamini.

“Nilipokuwa shule, nilikuwa siwezi kufanya mtihani bila kuvuta sigara. Ilinijengea kujiamini na kuweka umakini wangu katika mtihani huo,” anasema Jumanne huku akiamini kuwa sigara ilimfanya kuwa bora kwa wakati huo. 

Haja ya kutafuta umakini huo humpelekea mtumiaji kutaka zaidi na zaidi ya “nicotine” na kujikuta teja wa bidhaa ya tumbaku.

Licha ya kuwa baadhi ya wavutaji hawataki kuachana na tumbaku, matumizi ya bidhaa hizo yanazidi kuwaweka hatarini kiafya na kuhatarisha maisha yao. 

Magonjwa wanayopata huwa ni moja ya vyanzo vinavyowarudisha nyuma katika jitihada za kujikwamua na umaskini kwa kuwa fedha nyingi hutumika katika kujitibia badala ya kuendelea kuzalisha mali. 

Kwa mujibu Dk Kleczka, matumizi ya tumbaku ikiwemo sigara husababisha magonjwa ya kansa na hivyo kuwa hatari kwa watumiaji wake.

"Kwa wanaovuta sigara huku wakitumia pombe, wanaweza kupata kansa ya mdomo," amesema mtaalamu huyo wa masuala ya afya.

Wataalamu wanaeleza kuwa baadhi ya uchafu wa tumbaku hasa mtu anapovuta sigara hukwama kwenye mishipa ya damu na kufifisha ufanisi wa mzunguko wa damu mwilini.

“Kuta za mishipa ya damu zinapo jaa  “nicotine stains” (uchafu wa sumu ya nicotine) damu inakuwa haipiti kama kawaida. Badala yake, mwili unakuwa unatumia presha kubwa sana kusukuma damu ambayo awali ilisukumwa kawaida...hali hiyo inaweza kupelekea matatizo ya moyo,” anasema mtaalamu wa afya kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro, Dk Beno Nkwama. 


Tumbaku huathiri hata wasiotumia

Wakati madhara hayo yakimkuta mtumiaji, hata abiria anayekaa na mvutaji sigara kama Jumanne naye habaki salama. Ni sawa na kusema, kama Jumanne anavuta sigara tatu hadi mwisho wa safari yake, basi abiria wake naye anavuta sigara tatu bila kupenda.

Kwa mujibu wa utafiti huo wa GATS uliofanywa nchini, zaidi ya robo tatu (asilimia 77) ya watu wengi waliotembelea maeneo ya baa na klabu za usiku siku 30 kabla ya utafiti huo, walivuta sigara bila kupenda. 

Ukiachana na waathirika wanaokaa kwenye maeneo ya starehe, waathirika wengine huwa kwenye majukumu yao ya ofisini wakijitafutia mkate wa kila siku. 

Utafiti huo unabainisha kuwa mtu mmoja kati ya watatu au asilimia 32 ya wafanyakazi wa maofisini, wanavuta moshi wa sigara bila kupenda wakati wavutaji wakifanya starehe hiyo.

Zaidi ya robo tatu (asilimia 77) ya watu wengi waliotembelea maeneo ya baa na klabu za usiku siku 30 kabla ya utafiti huo, walivuta sigara bila kupenda. Picha| Dragon social.


Sheria kudhibiti matumizi ya tumbaku

Pamoja na baadhi ya wavutaji tumbaku kutafuta njia za kuacha, mamlaka nazo zinahaha kuliokoa Taifa na matumizi ya bidhaa hizo ambazo pia ni moja ya vyanzo vikubwa vya mapato ya Serikali. 

Mkurugenzi wa huduma ya Kinga kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dk Leonard Subi ameiambia Nukta kuwa  Wizara ya afya imefanya mambo mengi yanayolenga kupunguza matumizi ya tumbaku ikiwemo kutoa elimu kwa watumiaji juu ya madhara ya bidhaa hizo. 

Licha kuwa bidhaa za tumbaku kuwa mtambuka kwa kuhusisha wizara nyingi zikiwemo ya kilimo, viwanda na ya afya, kazi kubwa iliyofanyika ni kuelimisha wananchi juu ya matumzi ya tumbaku.

“Tumefanya mambo mengi, tumetunga sheria na pia tunaelimisha jamii juu ya matumizi ya tumbaku,” Dk Subi ameiambia Nukta.

Mbali na hayo, Sheria ya udhibiti wa bidhaa za tumbaku ya mwaka 2003 inazuia mtu kuvuta sigara maeneo ya umma huku ikiongelea matangazo ya bidhaa hizo, vifungashio na maudhui ya bidhaa za sigara.

Sheria hiyo inazuia watu kuvuta sigara katika maeneo ya umma ambayo ni pamoja na vituo vya afya, maktaba, sehemu za ibada, sehemu za umma za chakula, majengo ya ofisi na sehemu za usafiri za ardhini, majini na angani.

Kwa upande wa matangazo ya bidhaa za tumbaku, sheria hiyo imezuia bidhaa za tumbaku kufanyiwa matangazo kwa njia ya machapisho au mfumo wowote wa mawasiliano unaotokea nje ya Tanzania.

Yeyote atakaye tumia bidhaa za tumbaku katika meneo ya umma kinyume na sheria, sheria hiyo imeagizwa kupigwa faini isiyozidi Sh500,000 au kifungo kisichozidi mwaka mmoja jela.

Related Post