Wizara ya Mifugo na Uvuvi yaomba bajeti ya Sh476.65 2025/26
- Bajeti yaongezeka licha ya changamoto ya ucheleweshaji wa fedha.
- Programu ya BBT yaimarishwa kwa ajira za vijana.
Dar es Salaam. Wizara ya Mifugo na Uvuvi imeomba kuidhinishiwa Sh476.65 bilioni kwa mwaka wa fedha 2025/2026 ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuongeza uzalishaji, kuimarisha rasilimali, na kuhamasisha ajira na uwekezaji katika sekta hiyo.
Pendekezo hilo la bajeti ni ongezeko la Sh16.3 bilioni au asilimia 3.6 kutoka bajeti ya mwaka unaomalizika Juni 30, 2025 ya Sh460.3 bilioni.
Akiwasilisha bajeti ya wizara hiyo Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Dk Ashatu Kijaji kwa mwaka wa fedha utakaoanza Julai, 2025 bungeni Dodoma leo Mei 23, 2025 Dk. Kijaji ameliomba Bunge kuidhinisha kiasi cha Sh101.5 bilion kwa ajili ya matumizi ya kawaida.
“Sh375.13 bilioni ni kwa ajili ya miradi ya maendeleo,katika matumizi ya kawaida, Sh47.26 bilioni zimetengwa kwa ajili ya mishahara, huku Sh54.25 bilioni zikiwa ni kwa ajili ya matumizi mengineyo ya kawaida,” ameeleza Dk Kijaji katika taarifa yake.
Kwa upande wa miradi ya maendeleo, Sh227.99 bilioni zinatoka ndani ya nchi, na Sh147.14 bilioni ni fedha kutoka nje.
Waziri huyo pia ameeleza kuwa Programu ya Jenga Kesho iliyo Bora (BBT) imeendelea kuwa kichocheo cha ajira kwa vijana katika sekta ya mifugo.
“Kupitia programu ya BBT, vikundi 20 vya vijana 106 vimepewa jumla ya ekari 1,761 katika Ranchi ya Kagoma na kupatiwa mkopo usio na riba wa Sh934.2 milioni kupitia Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) kwa ajili ya unenepeshaji wa ng’ombe,” amesema Dk Kijaji.
Aidha, kufuatia ufunguzi wa Ziwa Tanganyika kati ya Septemba na Desemba 2024, mavuno ya samaki yaliongezeka kwa asilimia 55.3 na kufikia tani 38,999.82 zenye thamani ya Sh324.85 bilioni, kutoka tani 13,886.39 zenye thamani ya Sh166.47 bilioni zilizovunwa katika kipindi kama hicho mwaka 2023.
Hadi Aprili 2025, wizara ilikuwa imekusanya maduhuli ya Sh56.07 bilioni, sawa na asilimia 97.94 ya lengo la Sh57.59 bilioni.
Katika mwaka wa fedha 2024/25, Sh97.2 bilioni ziliidhinishwa kwa matumizi ya kawaida, amesema Sh53.27 bilioni zilikuwa zimetolewa kufikia Aprili, sawa na asilimia 54.79 ya bajeti hiyo.

Kwa upande wa miradi ya maendeleo, bajeti ya mwaka 2024/25 ilikuwa Sh363.1 bilioni, lakini hadi Aprili 2025 ni Sh86.56 bilioni tu sawa na asilimia 23.84 ndizo zilizotolewa.
Ufinyu wa fedha hizo umesababisha ucheleweshaji wa utekelezaji wa miradi mbalimbali.
Akiwasilisha maoni ya kamati, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo, Deodatus Mwanyika Mbunge wa Njombe, ameonya kuwa hali ya kutotolewa kwa fedha kwa wakati inaweza kuathiri ukuaji wa sekta hizo.
“Kwa mwenendo huu wa upatikanaji wa fedha, haitarajiwi kuwa wizara itaweza kukamilisha majukumu yake yaliyopangwa kwa mwaka wa fedha 2024/25. Kamati inashauri fedha zinazopitishwa na Bunge zitolewe kwa wakati ili utekelezaji wa majukumu ya wizara uwe wa ufanisi na kuleta tija iliyokusudiwa,” amefafanua Mwanyika.

Sanjari na hilo Dk Kijaji amesisitiza kuwa katika mwaka wa fedha 2025/26, wizara yake itaendelea na utekelezaji wa miradi ya kuwainua vijana, ambapo zaidi ya vijana 440 wanatarajiwa kunufaika kupitia mitaji na uwezeshaji katika shughuli za ufugaji na uvuvi.
Pia wizara inatarajia kuimarisha masoko, kuongeza uzalishaji na thamani ya mazao ya mifugo na uvuvi, pamoja na kuhamasisha uwekezaji zaidi katika sekta hizo.
Kwa mujibu wa taarifa ya wizara, mwaka 2023 sekta ya mifugo ilichangia asilimia 6.2 ya pato la taifa na ilikua kwa asilimia 5.
Hata hivyo, changamoto ya kutopatikana kwa fedha za maendeleo kwa wakati inaendelea kuwa kikwazo kikubwa katika utekelezaji wa miradi.
Katika mwaka 2024/25, wizara pia ilipanga kukamilisha ujenzi wa mabwawa saba, visima virefu vitatu, bandari ya uvuvi ya Kilwa Masoko, pamoja na kuanza maandalizi ya ujenzi wa bandari ya uvuvi Bagamoyo, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuboresha miundombinu ya sekta ya uvuvi nchini.
Latest



