Idrisa Magesa: Kijana aliyerithi mikoba ya kuuza uji kutoka kwa bibi yake

Rodgers George 0501Hrs   Oktoba 10, 2018 Ripoti Maalum
  • Ni biashara aliyoazimia kuifanya tangu akiwa mdogo ili kuendeleza wito walioitia kwenye familia yake.
  • Uji ni zaidi ya biashara ambayo inamuingizia mtu kipato bali inafungua fursa mbalimbali za maisha.  
  • Uji wa Wakanda Mix ni kivutio kikubwa cha wakazi wa Jiji la Dar es Salaam kutokana na sifa ya kuwa na vionjo adimu.

Dar es Salaam. Ni kawaida katika mitaa mbalimbali ya miji mikubwa kama Dar es Salaam, nyakati za asubuhi na jioni kuwaona akina mama wakiwa wamebeba vikapu vyenye chupa za uji na kuuza katika maeneo yenye mikusanyiko ya watu hasa katika vituo vya daladala, sokoni na hata vijiweni ambako huwakutanisha vijana wa rika tofauti. 

Licha ya biashara hiyo kuwa sehemu ya kuwaingizia kipato lakini ni nadra kukutana na wanaume wakitembeza uji mtaani, kutokana na watu wengi kuamini kuwa kazi hiyo inawafaa wanawake.  

Idris Magesa (26) amekataa mtazamo hasi wa jamii na kujitosa kuifanya kazi hiyo ya kuuza uji ili kujipatia kipato cha kuendeleza maisha yake.  

Tofauti na akina mama wanaotembeza uji mitaani, Magesa amefungua mgahawa Mwenge, Jijini Dar es Salaam. Alianza biashara hiyo mwaka 2017 akiamini ndiyo njia pekee ya kumtoa kimaisha. 

 Kuingia katika biashara ya kuuza uji haikuwa bahati mbaya kwa Magesa bali amefufua na kuendeleza kazi ambayo ana uzoefu nayo tangu akiwa mdogo ambapo ilianzia kwa bibi yake na baadaye kufanywa na mama yake.

“Mama yangu amelelewa kwa biashara ya uji. Bibi yangu aliuza uji maisha yake yote tangu ningali mtoto mdogo,” anasema Magesa.

Haikuwa rahisi kwa kijana huyo kurithi mikoba ya kuuza uji, lakini ugumu wa maisha na kukosa ajira ndiyo vilimlazimisha kuifanya biashara hiyo.

Baada ya kumaliza elimu yake ya kidato cha nne mwaka 2010 hakubahatika kujiunga kidato cha tano, alijihusisha na kazi mbalimbali ikiwa ni pamoja na ufundi gereji, udereva wa daladala na taksi katika Jiji la Mwanza.

Maisha magumu yalimrudisha shuleni tena akiamini elimu itamrahisishia maisha na baadaye kuhamia Dar es Salaam ambapo alijiunga na Chuo cha Royal College mwaka 2011 akisomea Diploma ya Uandishi wa Habari.

Mwaka mmoja baadaye alishindwa kuendelea na masomo kutokana na kukosa ada ya chuo. 

“Baada ya maisha ya mtaani kuwa magumu ilinilazimu kuachana na masomo ili nifanye kazi zingine,” anasema Magesa ambaye hakukata tamaa ya kutafuta hatma ya maisha yake bali akaanza kazi ya kupiga picha mtaani akiamini mafanikio ni mchakato unaohitaji uvumilivu na kujituma.


Tofauti na akina mama wanaotembeza uji mitaani, Magesa amefungua mgahawa Mwenge, Jijini Dar es Salaam. Picha| Idrisa Magesa.

Machungu ya maisha yaliongezeka zaidi alipofiwa na baba yake mzazi mwaka 2004 na baadaye mama yake mwaka 2017. 

Mwaka huohuo, wazo la kufanya biashara ya familia  ya kuuza uji likazaliwa tena na akaamua kufungua mgawaha wa uji wa Habpap na kuifanya biashara hiyo kuwa sehemu ya maisha yake, “Uji ni zaidi ya biashara.”

Magesa hatangaika tena kutafuta ajira, kwasababu uji anaouza ndiyo mkombozi wa maisha yake. 

Mpaka sasa ameajiri vijana wawili wa kumsaidia kazi na kila siku anauza vikombe visivyopungua 40 ambapo kila kikombe ni Sh2,000 kwa uji wa kawaida na Sh3,000 kwa uji uliowekwa vionjo kama matunda na chokoleti.

Ukiachana na matamanio ya kuona Habpap inakua biashara endelevu na yenye mafanikio, Magesa pia amedhamiria kutoa fursa za ajira kwa vijana wenye nia ya kuwekeza katika biashara ya uji.    

“Habpap itasambaa ndani na nje ya mipaka yetu, tunatarajia kuwa na stesheni karibu na wateja wetu na kutengeneza fursa kwa watu wengine,” anasema Magesa.


Zinazohusiana:  


 

Ni Nini kipya Habpap?

Mafanikio ya Magesa ni jinsi alivyongeza ubunifu na vionjo kwenye uji wa ulezi na mchele ambapo unakuwa na mchanganyiko wa matunda, chokoleti na karanga. 

Utofauti huo umepelekea hata wale wasiopenda uji na waliochukulia uji kama chakula cha watoto kubadilisha mawazo yao.

“Mimi sio mpenzi wa uji. Nilikuja mara ya kwanza kwa ushawishi wa rafiki zangu na tangu hapo nimekuwa nikija mara kwa mara,” anasema David Msia mkazi wa Kimara.

Ujio huo uliopewa jina la 'Wakanda Mix', ndio unaomtoa Msia kutoka Kimara hadi Habpap Mwenge kufaidika na faida mbalimbali za kiafya za uji huo. 

“Mchanganyiko wa matunda, chokoleti, karanga na vitu vingine vimenifanya kugeuza Habpap kama sehemu mojawapo ya starehe kwangu,” amesema Msia.

Uji wa 'Wakanda Mix' ndiyo kivutio kikubwa cha wateja kuingia katika mgahawa wa Habpap. Picha| Idrisa Magesa.

Ukiachana na mandhari nzuri na usafi wa mgahawa huo, wateja pia hupata burudani ya televisheni wakati wakinywa uji au wanaposubiria huduma.

Furaha ya Magesa ni kuona wateja wanaotoka maeneo mbalimbali ya Jiji kuja katika mgahawa wake wakipata huduma bora ili kuimarisha afya zao.  

Tayari biashara hiyo imesajiliwa na Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA) kuonyesha ubora wa chkula kinachotolewa mgahawani hapo.

 Magesa anaamini kuwa, “Hakuna mkato, maisha ya mtaani huhitaji mangangali ili “kuyahitimu”. Habpap inashikilia historia ya mama yangu na ndicho hunipa nguvu ya kuamka kila asubuhi kupambana zaidi ya jana.”  

Related Post