‘Kiherehere’ kilivyomfikisha kijana wa Kitanzania kwenye ndoto zake

Rodgers George 2344Hrs   Mei 26, 2020 Ripoti Maalum
  • Kijana huyo aliyesoma shule anazoziita “za porini” sasa amefikia ndoto ya kuwa mtengeneza maudhui ya video.
  • Ameweza kuanzisha kampuni na wenzake wanne waliohitimu kwenye shule ya vipaji ya Multichoice.
  • Safari yake kufika huko itakufanya upende kushika kila fursa inayokuja mbele yako.

Dar es Salaam. Ni kawaida kwa baadhi ya vijana kupuuzia fursa ambazo zinakuja mbale yao licha ya fursa hizo kuwaandama zikiwaambia “Ni wewe” ninayekutafuta kwani wengi hudhani kuwa fursa hizo tayari zina watu wake.

Kati ya vijana hao alikuwa Wilson Nkya (25) ambaye mwaka 2019 alihitimu Shule ya vipaji ya (MultiChoice talent factory) inayoratibiwa na kampuni ya teknolojia ya MultiChoice ya nchini Afrika Kusini vilivyohusisha vijana 60 wa nchi mbalimbali barani Afrika.

Nkya ameiambia Nukta (www.nukta.co.tz) kuwa ilimchukua siku nyingi hadi kujaza fomu ambayo ilimpelekea kuingia kwenye shule hiyo licha ya kuwa alikuwa anapima kina cha maji kwa mguu mmoja.

“He! watu 60 Afrika nzima? Mimi nitatoboa? Nililiona lile tangazo mara nyingi lakini nilisema, Mungu awatangulie hao watu 60.

Kila nikienda nkirudi nalisikia ni kana kwamba Mungu ananiambia dogo hilo ni la kwako lakini nikiwaza 60, ninaona ni namba ndogo sana,” Nkya ameiambia Nukta.

Hayo yote yamepita. Sasa tugange ya sasa na yajayo.

"Sikupenda kupitwa. pale kitu chochote ninapotokea, lazima niwepo,"Picha| Wilson Nkya.  

Wilson Nkya ni nani?

Kama haumfahamu Nkya, kwa sasa ni mwanzilishi mwenza wa kampuni ya 4creations entertainment ambaye licha ya kuwa na Shahada ya Uchukuzi na usimamizi wa usafiri (Logistics and transport manangement) kutoka Chuo Cha Taifa Cha Usafirishaji (NIT), sasa ni “camera man” ambaye taaluma yake hajawahi kuitumia.

Kufika katika nafasi hiyo, kijana huyo amesema mafunzo ambayo ameyapata kwenye shule ya MultiChoice ambayo aliingia kwa kufanya majaribio kutokana na tangazo alilosema lilimuandama vimemsaidia kupata marafiki waliogeuka familia.

“Tulikuwa Watanzania wanne na baada ya kuhitimu shule ya MultiChoice, tumeamua kuanzisha kampuni pamoja,” Nkya ameiambia Nukta akiwataja wenzake kuwa Jamal Kishuli, Jane Moshi na Sara Kimario.

Kampuni ya 4Creations inajihusisha na kutengeneza maudhui ya kidijitali ambayo yanalenga kusimulia ukweli juu ya watu mbalimbali ambao wanaisukuma Tanzania na Afrika kuelekea kwenye mafanikio.

Hadi sasa 4 Creations imefanya mambo mengi yakiwemo kushiriki kwenye tamasha la JamaFest na miradi mingine ambayo Nkya amependa kuhifadhi kwani hayajafikia hatua ya kutangaza kwa umma yakiwemo filamu na miradi mbalimbali.

Hata hivyo, mbali na kuwa kigogo wa kampuni, Nkya anaamini katika mifumo mingi ya kungiza kipato hivyo hushiriki kwenye kazi binafsi za kuandaa maudhui akishirikiana na watu mbalimbali.


Zinazohusiana



Alichokipata baada ya MultiChoice

Hivi karibuni, kijana huyo aliyesoma kwenye shule alizoziita “zaporini” ameshiriki kwenye maandalizi ya vipindi vya masomo vilivyorushwa na chini ya Wizara ya Elimu vilivyokuwa vikifundisha masomo mbalimbali ya darasani.

Kwa mujibu wa Nkya, ni kupitia kuonekana kwenye harakati za DSTV ndipo watu walimtafuta ili aweze kufanya kazi hiyo.

Hata hivyo, vipindi hivyo vimesimama baada ya Janga la Corona (Covid-19) kuathiri utendaji kazi wake na hivyo kulazimika kusubiri hadi hali itakapokuwa shwari.

“Utafundishwa idara zote za filamu, utafundishwa utunzi wa nyimbo za filamu, utafundishwa uandishi na heshima ya hati miliki za wasanii, utafundishwa uandishi wa Script pamoja na uhariri na mambo mengine mengi. Hayo yote yamenifanya nijiamini katika kila ninachokifanya.

Kikubwa zaidi, nimejifunza kipengele cha biashara kwenye filamu kitu ambacho wachache wanaelewa,” anasema Nkya huku akijiamini. 

Zaidi, kupitia mafunzo hayo, Nkya amepata nguvu ya kufundisha wasanii wa filamu wa nchini juu ya kusimamia kazi za sanaa ambapo kupitia MultiChoice, yeye na wenzie walishiriki kwenye semina hiyo.

“Tanzania tuna changamoto nyingi zikiwepo za mtandaoni. Wengi hawafahamu hata jinsi ya kujiandikisha kunyakua fursa na tuzo mbalimbali za mtandaoni. Tuliwafundisha hayo.” Amesema Nkya.

Pia mbali na shughuli zake zinazohusisha tehama, Nkya hutengeneza “Bracelets” ambazo ni vionjo vinavyovaliwa mkononi na kazi hiyo humpatia hadi Sh300,000 kwa mwezi ambazo humsaidia kulipia kodi ya nyumba na gharama zingine.

Hata hivyo, bado anaendelea kujenga hadhira yake kwenye  mtandao wa YouTube ambapo huweka maudhuii mbalimbali.

Nkya alisoma masomo ya uchukuzi na hakuwahi kufikiria kama siku moja anaweza kuingia bungeni. Ndoto zake za kuwa "Camera man" zimemsogeza kwenye jengo hilo. Picha| Wilson Nkya.


Corona yaharibu mipango lukuki

Kwa kiindi hiki Nkya amesema changamoto kubwa ni Ugonjwa wa Corona ambao umeingilia mipango mingi kiasi cha kusimamisha baadhi ya kazi zake na hata kushindwa kuzitekeleza ambazo zinaendelea. 

Hata hivyo, kijana huyo amesema bado yupo kwenye mchakato wa kuangalia ni namna gani anaweza kuzitatua ikiwa ameshaanza kufanya mikutano kwa njia ya mtandaoni kama suluhisho moja wapo.

Zaidi, Nkya amesema anafanya kila analoliweza kwenye mitadao ya kijamii kuhamasisha na kuwasogeza vijana wengine karibu na fursa.

“Ninaamini vijana tunayo nguvu. Endapo kila mtu akiwa na utayari wa kufanya kitu na kuzitafuta ndoto zake, tunaweza fika tunapopataka,” amesema Nkya ambaye licha ya kufahamu hana talanta ya uimbaji, anatarajia kuingia studio aone muenendo wake.

Related Post