Safari bado ndefu mapambano ya Uviko-19 migodini Tanzania

September 16, 2021 2:02 pm · Mariam John
Share
Tweet
Copy Link

                           


  • Wachimbaji wa madini wapuuzia tahadhari ikiwemo uvaaji barakoa.
  • Ukosefu wa elimu na imani potofu zachangia.
  • Serikali kuendelea kuwahamasisha wajikinge ikiwemo kupata chanjo.

Mwanza/Geita. Kwilasa Senyi  ni  mchimbaji mdogo wa madini katika mgodi wa dhahabu  wa Stamico uliopo kijiji cha Nyarugusu mkoani Geita. Mgodi huo ndiyo chanzo kikuu cha kujipatia kipato kwa ajili ya familia yake.

Senyi (24), baba wa mtoto mmoja anasema maisha ya mgodi siyo mepesi inahitaji jitihada na uvumilivu  ili kuyapata madini.

“Kazi hii haihitaji vyeti ni nguvu zako tu ndiyo zitakufanya uishi hapa,  wapo waliojaribu  wakaona maisha ni magumu wakaishia mitini,” anasema Senyi.

Hata hivyo, Senyi na wenzake waliopo mgodini hapo wanajiweka katika hatari ya kutofikia malengo yao na kutunza familia kwa sababu ya kutozijali afya zao, mtaji namba moja wa mafanikio yao.

Hawachukuii tahadhari dhidi ya ugonjwa wa virusi vya Corona (Uviko-19).

Licha ya viongozi wa Serikali kusisitiza kuwa katika maeneo yenye mkusanyiko ya watu kuwepo na vifaa vya kunawia mikono, vitakasa mikono na uvaaji barakoa wakati wote, lakini ni wachimbaji wachache katika mgodi huo wanaozingatia tahadhari hiyo.

Mmoja wa wachimbaji katika mgodi huo uliopo kata ya Nyakafuru Wilaya ya Mbogwe, Frank Fidelisi  anadai kuwa hawachukuii tahadhari kwa sababu wanasikia kuwa ugonjwa wa Uviko-19 upo lakini bado haujafika katika maeneo yao.

“Ugonjwa wa Corona tunausikia huko kwenye nchi za jirani lakini katika maeneo haya haujafika ndiyo maana tunaendelea na shughuli zetu za kila siku,” anasema Fidelis.

Huenda Fidelis hana taarifa muhimu kuhusu ugonjwa huo kuwa uko Tanzania na Serikali imekuwa ikitoa maendeleo ya ugonjwa huo ikiwemo zoezi la utoaji wa chanjo linaloendelea nchi nzima.

Wachimbaji wadogo wa dhahabu wakisafisha dhahabu kwa kutumia maji katika mgodi wa Stamico mkoani Geita. Picha| Mariam John

Hali hiyo ya kutokuchukua tahadhari haitofautiani na mgodi wa dhahabu wa Chitongo-Ishokela hela uliopo Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza ambako Nukta Habari (www.nukta.co.tz) ilitembelea kuona namna wachimbaji wa madini wanavyojikinga na Uviko-19.

Huko nako, mwendo ni ule ule wa kupuuzia tahadhari, shughuli zinaendelea kama kawaida. Katika mgodi huo wa wachimabji wadogo, hakuna vifaa vya kunawia mikono wala uvaaji wa barakoa hauzingatiwi.

“Watu wa huku wanaimani kwamba wakimuona mtu amevaa barakoa wanajua ndiye ana Corona na amevaa ili asiambukize wengine..,” anasema Maulid Fundi, mkazi wa kata ya Buhunda anayefanya kazi karibu na mgodi huo. 

Fundi anasema anapata taarifa kuwa watu wanakufa kwa Uviko-19 na amekuwa akichukua tahadhari lakini changamoto ni wachimbaji wadogo wa madini bado hawana elimu ya kutosha kuhusu ugonjwa huo.

Jambo hilo limesababisha baadhi ya wajasiriamali waliokuwa wanauza barakoa katika wimbi la kwanza kukosa wateja kwa sababu uvaaji barakoa umekuwa kama ‘jambo geni’ kwa watu wanaofanya kazi migodini. 

Baadhi ya wachimbaji wadogo wameiambia Nukta Habari (www.nukta.co.tz) kuwa mara kadhaa wametembelewa na wataalam wa afya kuwahimiza kuvaa barakoa lakini wanadai ni ngumu kuzitumia kutokana na aina ya shughuli wanazofanya.

Kwa wachimbaji wanaovaa hulazimika kuzivua barakoa hizo pindi wanapoingia ndani ya mashimo (miduara) ili kuhakikisha wanapata hewa ya kutosha wanapoendelea na uchimbaji chini ya ardhi.

“Tunazingatia uvaaji wa barakoa nje ya maduara ingawa hatuvai tunapoingia ndani ya duara au wakati wa kupiga rola kwa kuwa kazi hizi hutumia pumzi nyingi na ndani ya duara kuna mgandamizo mdogo wa hewa hivyo ukivaa barakoa inaweza kuchangia tatizo la upumuaji,” anasema Jeremia Kondo mchimbaji katika mgodi wa Chitongo-Ishokela hela.

Anasema wakiwa ndani ya mduara wanapeana nafasi ya kutosha ili kuhakikisha hawaambukizani ugonjwa huyo na endapo ikitokea mwenzao anaugua humtoa nje.

Mchimbaji mwingine katika mgodi wa Stamico, Hoja Shikombe anasema wataalam wa afya walipita kwenye maeneo yao kuwapa elimu ya kujikinga na ugonjwa huo pamoja na matumizi ya barakoa lakini muitikio umekuwa ni mdogo. 

Hata hivyo, wataalam wa afya wamekuwa wakisisitiza uvaaji wa barakoa katika maeneo yote ili kujikinga na ugonjwa wa Uviko-19 na kuchukua tahadhari zote zinazopendekezwa ikiwemo kupata chanjo.

 

Wapo tayari kupata chanjo

Licha ya wachimbaji wa madini kupuuzia tahadhari ya Uviko-19, wanasema wapo tayari kupata chanjo ili wawe salama dhidi ya ugonjwa huo.

Hata hivyo, wanalalamika kuwa vituo vya kutolea chanjo hiyo viko mbalimbali na maeneo yao ambapo watalazimika kutembea umbali mrefu kwenda kufuata huduma hiyo.

“Tunatamani kupata chanjo ila ipo mbali mno tungeomba vituo viongezwe hadi maeneo ya migodini ili wachimbaji tupate huduma karibu,” anasema Shija Rafael, mchimbaji wa madini mgodi wa Stamico Nyarugusu.

Mchimbji mdogo wa dhahabu, Naomi Kulwa  akiwa anaponda kokoto katika mgodi wa dhahabu Stamico Nyarugusu ili zikasagwe kwenye karasha ili kupata unga wa dhahabu. Picha| Mariam John.

Elimu inaendelea kutolewa

Serikali inasema kinachofanyika ni kuendelea kutoa msisitizo katika maeneo ya migodi namna ya kuchukua tahadhari ya kujikinga na ugonjwa huo kama miongozo ya Serikali inavyoelekeza.

Afisa Uhusiano wa Wakala wa Usalama na Afya Mahala pa Kazi (OSHA), Eleuter Mbilinyi anasema wataalam wa OSHA wanapokuwa wanakagua migodi hufuatilia pia suala la kuchukua tahadhari dhidi ya Uviko-19.

“Sisi kama Osha hatuko mbali na Serikali, kinachofanyika ni kuhakikisha tunasisitiza hilo suala pia ili wachimbaji wanakuwa salama na wanazingatia miongozo yote ya afya kujikinga na ugonjwa huo,” anasema Mbilinyi.

Licha ya muitikio mdogo, viongozi wa maeneo hayo ya migodini hawajakata tamaa kuwaelimisha wananchi ili wajikinge na kuwa salama dhidi ya janga hilo.

“Tunaendelea kutoa elimu ya kujikinga na ugonjwa huo,  tunahamasisha watu kunawa mikono na kupaka vitakasa mikono,” Diwani wa kata ya Buhunda, Luzambya Simuda.

Mganga Mkuu wa Wilaya ya Misungwi, Dk Clement Morabu  anasema licha ya elimu ya kujikinga, wanatoa hamasa kwa watu katika wilaya hiyo kujitokeza kupata chanjo ya Uviko-19.

Anasema Wilaya yake  ilipokea  dozi 4,600 za  chanjo aina ya Johnson & Johnson ambazo zinatolewa katika vituo vitatu vya Hospitali ya Wilaya ya Misungwi,  Kituo cha Afya,  Bukumbi na Kituo cha afya Misasi.

Kwa sasa, Serikali inaangalia uwezekano wa kuwafikishia watu chanjo maeneo waliyopo ikiwemo sehemu zenye mikusanyiko ya watu ili kurahisisha zoezi la uchanjaji.

Makala hii imefadhiliwa na Shirika la maendeleo ya habari la International Media Support (IMS) na Umoja wa Ulaya (EU).

Enable Notifications OK No thanks