Tanzania yazindua filamu kutangaza utalii kimataifa

May 29, 2020 2:20 pm · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link
  • Imetafsiriwa katika lugha tano kikiwemo Kiswahili.
  • Itasaidia kuyafikia masoko ya utalii ya kimataifa na kuongeza mapato ya Taifa.
  • Watanzania watakiwa kuisambaza kwa kasi ili kuvutia watalii wengi.

Dar es Salaam. Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) imezindua rasmi filamu inayoitambulisha Tanzania ndani na nje ya nchi katika maeneo mbalimbali ya utalii ikiwa ni hatua ya kuongeza wigo wa masoko kimataifa. 

Uzinduzi huo ni miongoni mwa mikakati ya TTB iliyojiwekea hivi karibuni kukabiliana na athari za ugonjwa wa virusi vya Corona katika sekta ya utalii nchini.

Waziri Mwenye wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwangalla amesema lengo la filamu hiyo fupi ya “Tanzania Unforgettable” (Tanzania isiyosahaulika) ni kutambulisha vivutio vya utalii katika soko la utalii kimataifa.

Dk Kigwangala amewataka Watanzania kuisambaza  filamu hiyo kwenye mitandao yao ya kijamii ikiwemo Facebook, Twitter, Instagram, Telegram na mitandao mingine, ili iweze kuwafikia walengwa.

“Kwa hiyo ninaomba Watanzania wenzangu tuisambaze kwenye mitandao yetu ya kijamii kwa maana imetafsiriwa katika lugha ya Kiswahili, Kingereza, Kifaransa, Kihispania, Kiisrael na Kichina”, amesema Waziri huyo leo Mei 29.


Zinazohusiana: 


Huenda filamu hiyo ikasaidia kuongeza idadi ya watalii wanaotembelea Tanzania, ikizingatiwa kuwa idadi ya watalii wanaokuja nchini mwaka huu itashuka kutoka milioni 1.8 waliotarajiwa hadi kufikia watalii 437,000 kutokana n aathari za janga la Corona.

Mkurugenzi Mtendaji wa TTB Devotha Mdachi amesema kuwa Tanzania kwa sasa imejikita zaidi kutangaza vivutio vya utalii kupitia mitandao ya kijamii, kwa hiyo kuzinduliwa kwa filamu hiyo fupi kutawasaidia kuteka soko la ndani na nje ya nchi.

Amesema kupitia filamu hiyo fupi watalii watapata fursa ya kuona utamaduni na maeneo mbalimbali ya kuvutia na kuweza kuchagua sehemu sahihi ya kwenda kutembelea.

Filamu hiyo iko katika ukubwa wa dakika moja, dakika tatu, dakika saba na dakika 10 inapatikana YouTube na akaunti za mitandao ya kijamii ya TTB.  

Enable Notifications OK No thanks