Tanzania mbioni kufungua shule za msingi, awali

Daniel Samson 0643Hrs   Juni 05, 2020 Habari
  • Serikali imesema inaangalia mambo yanavyokwenda na hivi karibuni itazifungua shule hizo.
  • Yasema ugonjwa wa virusi vya Corona umepungua nchini. 
  • Walimu wahakikishiwa kuendelea kulipwa mishahara yao hata kama corona itakaa miaka 10.  

Dar es Salaam. Rais John Magufuli amesema Serikali iko mbioni kufungua shule za msingi na awali kwa sababu ugonjwa wa virusi vya Corona umepungua Tanzania ikiwa ni mwendelezo wa kulegeza masharti ya kudhibiti maradhi hayo. 

Juni mosi mwaka huu, Serikali ilifungua vyuo vyote na kuwaruhusu wanafunzi wa kidato cha sita wanaojiandaa na mitihani ya kuhitimu kurudi shuleni. 

Dk Magufuli amesema wanaendelea kutathmini hali ya ugonjwa wa virusi vya COVID-19 ili kuwaruhusu wanafunzi wa shule za msingi kurudi shuleni baada ya kukaa nyumbani kwa zaidi ya miezi miwili.

“Na mimi nina uhakika hivi karibuni baada ya kufungua vyuo tunaangalia mambo yanavyoenda na shule za msingi na chekechea nazo ziko mbioni tutazifungua ili walimu mkafanye kazi kwa sababu ninafahamu walimu wa Tanzania wanapenda kufanya kazi,” amesema Rais Magufuli. 

Amesema COVID-19 imepungua nchini kwa kiasi kikubwa ndiyo maana shughuli mbalimbali za kiuchumi zinaendelea ikiwemo za utalii na usafiri wa anga. 

“Ugonjwa huu umepungua na nina uhakika utaisha kwa sababu Mungu yupo pamoja na sisi," amesema Rais Magufuli  Ijumaa hii (Juni 5, 2020) wakati akifungua mkutano mkuu wa uchaguzi wa Chama Cha Walimu Tanzania (CWT) uliofanyika jijini Dodoma.


Zinazohusiana:


‘Walimu kuendelea kulipwa hata COVID-19 ikibaki miaka 1O’

Katika mkutano huo uliohudhuriwa na mamia ya walimu, Dk Magufuli amesema Serikali itaendelea kutekeleza maslahi ya walimu ikiwemo kuwalipa mishahara hata kama Corona itaendelea kuwepo kwa muda mrefu kwa sababu wanafanya kazi kubwa ya kuwaelimisha wanafunzi.

“Corona hata ikikaa mwaka mzima, hata ingekaa miaka 10, sitakosa mshahara wa kuwalipa walimu hata wakiwa nyumbani. Hili ndugu zangu lisitafsiriwe kama kampeni,” amesema mkuu huyo wa nchi. 

Licha ya shule kufungwa, amesema walimu ambao ni zaidi ya 266,905 wameendelea kulipwa mishahara yao takribani Sh300 bilioni kila mwezi.  

Walimu na watumishi wengine wa shule wamekuwa nyumbani kwa zaidi ya miezi miwili sasa baada ya Serikali kuzifunga shule zote nchini katikati mwa Machi 2020 ili kukabiliana na kusambaa kwa COVID-19. 

“Nataka niwahakikishie siwezi nikawatupa walimu wa Tanzania, tunajenga nyumba moja, ninafahamu shida za walimu kwa sababu hata mimi nimeyaishi. Kuwakana walimu ni kujikana nafsi yangu kitu ambacho siwezi nikafanya ndugu zangu walimu,” amesisitiza Rais Magufuli akibainisha kuwa Serikali itaendelea kushughulikia matatizo yao. 

Related Post