Tanzania kukamilisha majadiliano mradi wa LNG mwaka 2024-25

Mwandishi Wetu 1211Hrs   Aprili 24, 2024 Habari
  • Ni baada ya utekelezaji wake kuchelewa kutokana na kuwepo mazungumzo ya muda mrefu.
  • Kukamilika kwa mradi huo kutaifanya Tanzania kuwa moja ya nchi zinazochangia katika usalama wa nishati duniani.

Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imesema inatarajia kukamilisha majadiliano na wawekezaji wa mradi wa kuchakata na kusindika gesi asilia kuwa kimiminika (LNG) ili kuanza utekelezaji wake ambao umechelewa kutokana na kuwepo mazungumzo ya muda mrefu. 

Utekelezaji wa awali wa mradi huo unaotarajia kutumia gesi kutoka katika vitalu namba 1, 2 na 4 mkoani Lindi na kuuzwa katika masoko ya nje ulitarajiwa kuanza mwezi Julai 2023 baada ya kukamilika kwa mazungumzo yaliyokwama kwa miaka nane tangu yalipoanza rasmi Septemba, 2016.

Kukamilika kwa mradi huo utakaogharimu Dola za Marekani bilioni 42 sawa na zaidi ya Sh90 trilioni kunatarajiwa kuleta mapinduzi makubwa ya kiuchumi nchini kwa kuwa utaifanya Tanzania kuwa moja ya nchi zinazochangia katika usalama wa nishati duniani.


Soma zaidi:Utafiti gesi asilia ya kupikia majumbani Dar kukamilika Julai 2024


Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko ameliambia Bunge leo (Aprili 24, 2024) kuwa mradi huo ni miongoni mwa miradi ya kipaumbele iakayotekelezwa katika mwaka wa fedha unaoanza Julai 2024.

“Katika mwaka 2024/25 utekelezaji wa majukumu ya wizara utaongozwa na vipaumbele mbalimbali vinavyojikita katika kuendelea kutekeleza miradi ya uzalishaji…kuchakata na kusindika gesi asilia kuwa Kimiminika (LNG) na ujenzi wa bomba la kusafirisha mafuta kutoka Hoima, Uganda hadi Tanga, Tanzania (EACOP),” amesema Dk Biteko.

Awali Serikali ilieleza kuwa maamuzi ya mwisho ya uwekezaji wa mradi huo uliopo kusini mwa Tanzania yangefanyika mwaka 2025, hatua ambayo huwa ni taa ya kijani kuanza kutekelezwa kwa mradi. 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan(katikati) akishuhudia utiaji saini mkataba wa awali wa mradi wa kuchakata na kusindika gesi Asilia (LNG) kwenye hafla iliyofanyika tarehe 11 Juni 2022 Ikulu, Dodoma.Picha/Ikulu

Mei mwaka jana Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan ilifikia makubaliano muhimu kuhusu mikataba na kampuni zinazomiliki vitalu vya gesi asilia za Equinor, Shell na Exxon Mobil ikiwa ni moja ya hatua iliyokuwa ikisubiriwa na soko la nishati duniani. 

Hatua hiyo ilikuwa ikileta matumaini huenda makubaliano yangekamilika mwaka jana hasa baada ya aliyekuwa Waziri wa Nishati January Makamba kueleza kuwa rasimu za mikataba zilikuwa zikisubiria mapitio na baraka za baraza la mawaziri. 

Katika hotuba ya bajeti ya wizara yake leo, Dk Biteko ameeleza kuwa katika mwaka 2023/24 waliendelea majadiliano ya mikataba ya utekelezaji wa mradi huo ili kuboresha rasimu za awali za mikataba hiyo kwa kuzingatia maoni yaliyotolewa na wadau mbalimbali ikiwemo Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na taasisi nyingine za Serikali.

Related Post