Utafiti gesi asilia ya kupikia majumbani Dar kukamilika Julai 2024

Mwandishi Wetu 0643Hrs   Aprili 04, 2024 Habari
  • Utafiti huo utaonesha maeneo yatakayopitiwa na mabomba ya gesi.
  • Utasaidia kuwapunguzia wananchi gharama za nishati ya kupikia. 


Dar es salaam. Serikali imesema utafiti wa kusambaza gesi asilia ya kupikia majumbani katika jiji la Dar es salaam utakamilika Julai 2024 ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kupunguza changamoto na gharama ya nishati ya kupikia kwa wananchi.

Naibu Waziri wa Nishati Judith Kapinga ametoa kauli hiyo leo Aprili 4, 2024 Bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Kawe, Askofu Josephat Gwajima.

Askofu Gwajima alitaka kujua ni lini Serikali itaweka bomba la gesi kila nyumba jijini Dar es salaam ili wananchi wapikie nishati kwa bei nafuu.

Kapinga akijibu swali hilo, amesema Serikali inaendelea na utafiti wa kubaini sehemu zenye changamoto katika usambazaji wa mabomba ya gesi na njia mbadala za kuhakikisha huduma iyo inawafikia wakazi wa jiji hilo linalokua kwa kasi Afrika. 

“Ili kuhakikisha wananchi wengi jijini Dar es salaam wanatumia gesi asilia, TPDC (Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania) kwa kushirikiana na kampuni ya TAQA - DALBIT inafanya utafiti wa mahitaji ya gesi asilia kwa njia za kusambazia utakaokamilika Julai 2024,” amesema Kapinga.


Soma zaidi: Biogesi inavyosaidia kudumisha ndoa Tanzania


Utafiti huo utaonesha namna bora ya kufikisha mabomba kwenye maeneo yenye changamoto na utabaini maeneo gani yanaweza kuwekewa mabomba na njia nyingine zitatumika kuhakikisha gesi inawafikia wananchi.

Kwa mujibu wa ripoti ya Utafiti wa Athari za Upatikanaji wa Nishati Endelevu 2021/22 iliyotolewa Novemba 2023 na Ofisi ya Takwimu ya Taifa (NBS) inaonesha asilimia 34 ya kaya katika Mkoa wa Dar es Salaam hutumia gesi kama chanzo chao kikuu cha nishati kwa ajili ya kupikia.

TPDC mpaka sasa imeweza kusambaza nishati ya gesi ya asili katika nyumba 880, hoteli 6 na viwanda 2  katika jijini Dar es salaam kwa kupitia bomba la kilomita 12.4 kutoka Mwenge hadi Mbezi Beach kama sehemu ya mkakati wa kuboresha huduma hiyo. 

Kwa mujibu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma ya Nishati na Maji (EWURA), Tanzania imekuwa ikifanya utafiti wa gesi asilia kwa zaidi ya miaka 50. 

Ugunduzi wa kwanza wa gesi asilia nchini ulifanyika mwaka 1974 katika Kisiwa cha Songo Songo kilichopo Mkoa wa Lindi na kufuatiwa na ugunduzi wa pili katika eneo la Mnazi Bay mkoani Mtwara mwaka 1982. 

Gesi asilia kutoka Songo Songo iliuzwa kwa mara ya kwanza mwaka 2004 na ya kutoka Mnazi Bay mwaka 2006. Ugunduzi huo umechochea kufanyika utafiti zaidi wa gesi asilia kwa maeneo ya nchi kavu na majini.

Hadi kufikia Machi 2016, Wizara ya Nishati ilithibitisha kuwa, hifadhi ya gesi asilia iliyogunduliwa Tanzania inafikia futi za ujazo trilioni 57.25.


(Habari hii imeandikwa na Thomas Kibaja na kuhaririwa na Daniel Samson)

Related Post